Shuka jeupe: Jinsi mila za ubikira zinavyoendelea kuwazonga maharusi wa leo

A bride looking sad on her wedding day, with three woman looking at her critically

"Alipoanza kuvua nguo mbele yangu baada ya harusi, nilijawa na woga moyoni," anakumbuka Elmira (si jina lake halisi).

"Japo nilijitahidi kuukubali uhalisia wa maisha ya baada ya kuolewa, haikunipoza woga wangu hata kidogo. Kichwani mwangu nikawa najiambia kuwa inanipasa nami nianze kuvua nguo."

Elmira alikuwa na miaka 27 alipoolewa, alikuwa mhitimu wa Chuo Kikuu na akifanya kazi kama mkalimani.

Alichaguliwa mume na wazazi wake. Alikubali kuolewa ili "kumfanya mama awe na furaha."

"Alikuwa ni jirani yetu, lakini tulikuwa ni watu tofauti kabisa; yeye hakuwa na elimu, hatukuwa na kitu chochote cha kutuunganisha," anakumbuka Elmira.

"Nilitambulishwa kwake na kaka zangu, na waliniambia kuwa alikuwa ni mtu mwema. Mama alijawa na furaha kuwa naolewa na jirani, na nitakuwa karibu naye kwa lolote lile."

Elmira lakini alijaribu kumwambia mama yake mara kadhaa kuwa hakuwa tayari kuanza maisha ya familia kwa muda huo. Mama yake akawaambia ndugu zake ambao nao wakaanza kumshinikiza, pia wakaanza kumshuku kuwa huenda akawa si bikira.

Hata hivyo, usiku wa harusi yake ndiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kufanya mapenzi.

Baada ya kugundua kuwa ni bikira, mumewe hakujali kuhusu hisia zake na kumvaa kwa nguvu zaidi.

Alipoanza kugonga kichwa huku na kule ikiwemo kwenye kabati, alisikia mlango ukigongwa na sauti ya mwanamke ikiwasemesha kutoka chumba cha pili: " Tunataka ukimya huko ndani!"

Nyuma ya mlango walikuwapo wanawake watano, mama wa Elmira, shangazi zake wawili, na ndugu mmoja wa mbali (ambaye ndiye aligonga mlango) - ambao uwepo wao wote ni wa lazima ili kuthibitisha iwapo tendo la ndoa limefanyika na pia ubikira wa biharusi.

"Ungeweza kusikia kila sauti, hata iwe ndogo," anakumbuka Elmira. "Nilikuwa natetemeka kwa woga na hofu, nikawa najiuliza, 'Je, ndoa kweli ndiyo huwa hivi?'"

Yule ndugu wa mbali ambaye kwa mila zao humuita "engi" hukaa nje ya mlango wa wanandoa usiku kucha. Moja ya majukumu yake ni kumpa ushauri biharusi. Mantiki ya jamii hiyo ni kuwa, biharusi ambaye hana uzoefu kabisa wa tendo la ndoa anaweza kutaka kukimbia 'majukumu.'

Jukumu lengine la engi ni kuchukua mashuka baada ya usiku wa kwanza wa ndoa.

Shuka jeupe hadharani

Kuoneshwa kwa shuka jeupe hadharani asubuhi baada ya usiku wa ndoa ni jambo la kawaida kwa mila za nchi nyingi za Ulaya Mashariki, ama nchi za Caucasus.

Damu kwenye mashuka hayo huchukuliwa kama alama ya kufanyika kwa tendo la ndoa. Baada ya hapo familia za pande zote mbili huwapongeza maharusi baada ya kuona matone hayo ya damu.

Na pale tu mashuka hayo yenye damu yanapooneshwa ndiyo ndoa huonekana kuwa imekamilika.

A group of relatives plant a flag of a bloodstained bedsheet

"Kutokana na hili ndio maana usiku wa ndoa unakuwa na mengi ya siri - ikiwemo swali endapo mashuka yataoneshwa asubuhi?" anasema Shakhla Ismail, ambaye amebobea katika haki za wanawake nchini Azerbaijan.

Na endapo mashuka hayo hayatakuwa na damu, biharusi anaweza kutengwa, na kurejeshwa kwa wazazi wake kwa kuwa 'ni mwenye kasoro'."

Baada ya hapo huwa anachukuliwa kama aliyepewa talaka, na yaweza ikawa ngumu sana kwake kuolewa tena - pia anaweza akakutana na manyanyaso makubwa ndani ya nyumba ya wazazi wake.

Wanaharakati nchini Azerbaijan wanasema kuwa kusimamia maharusi na kuoneshwa kwa shuka jeupe asubuhi bado ni mila inayoendelezwa kwenye maeneo mengi ya vijijini ya nchi hiyo.

Wakati mwengine, hata kabla ya ndoa, mwanamke huchunguzwa na mtaalamu iwapo bado ni bikira.

Mwaka jana Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika lake la Afya (WHO) mwaka jana walipinga vikali vitendo hivyo na kuzitaka nchi 20 ambazo mila hizo zingali zinaenziwa wakomeshe matendo hayo.

Tamko lao lilisisitiza kuwa, ubikra si hali inayotambulika kisayansi ya kitabibu bali kijamii, mila na kidini.

"Ni usiku wa maumivu na aibu"

Woga, machungu na aibu ndizo hisia ambazo Elmira anazihusisha na usiku wa ndoa.

"Nilijikunyata peke yangu, na nilikuwa na woga sikuweza kusema chochote. Sikupata hata lepe la usingizi usiku kucha. Lakini yeye wala hakujali, aliuchapa usingizi kwa amani kabisa."

Asubuhi mashahidi wakaja chumbani na kuchukua mashuka, "Lakini ilipofikia wakati huo sikujali tena - nilijuwa ni jambo baya sana, lakini woga wa kilichonipata ulifuta kila aina ya aibu niliyokuwa nayo," amesema Elmira.

Mwanasaikolojia Ellada Gorina anasema maumivu hayo huwapata wanawake wengi na huongezeka kila mwaka.

Three women listen with implements in their ears

Lakini katika dunia ya leo ambapo wanawake huolewa wakiwa kwenye umri mkubwa, na ni kawaida kwao kufanya ngono kabla ya kuolewa, wanawake hao wala hawahitaji ushauri wa engi ama kuwa na mashuhuda wa kuhakikisha ubikira wao.

Negar, ambaye pia amekulia Azerbaijan vijijini, anakumbuka kuwa kwake mashuhuda hawakuwa wawili ama watatu bali "kijiji kizima" kilijikusanya kushuhudia.

"Sijawahi kudhalilika kama siku ile, lakini nikaona labda ni jambo kawaida maana wazee ndio wanaoujua zaidi yangu."

Mila hizo haziishii Azerbaijan tu, bali hii leo zinaendelea kuenziwa vijijini nchini Georgia, Armenia na baadhi ya majimbo ya Urusi.

A man and a woman stand with an apple on the end of a knife

Katika maeneo hayo mabinti huozwa wakiwa wadogo, mara tu baada ya kutimiza miaka 18. Na majirani hualikwa kuthibitisha iwapo mabiharusi hao ni mabikira ama tayari "wameshachafuliwa."

"Kijiji chote hushiriki katika mila hiyo ya udhalilishaji," ameeleza mwanaharakati mmoja.

Na endapo binti huyo atakuwa si bikira, ama kwa lugha yao hatakuwa na tufaa jekundu, wazazi wake huenda wakamtimua nyumbani.

Ellada Gorina, anasema baadhi ya wanawake hupona kutokana na mateso hayo ya akili na wengine hubaki na makovu ya milele.

"Moja ya tukio la kusikitisha ni baada ya kukosekana kwa damu kwenye shuka familia ya bwana harusi katikati ya usiku ikaamua kumpeleka biharusi kwa daktari ili amchunguzi kama ni bikira ama la?" ameeleza Gorina.

Kuvunjiwa kwa faragha kwa namna hii kunaweza kumfanya mwanamke ajione kuwa ni mhanga wa vurugu, na kumfanya abaki na makovu ya ubongo kwa maisha yake yote, amesema Gorina.

Miezi sita baada ya ndoa, mume wa alifikwa na umauti. "Kwa miezi yote sita hatukuwahi kuuzungumzia ule usiku wa kwanza," amesema.

Baada ya kifo cha mumewe ameshindwa kuwa na mwanaume mwengine - anasema ana changamoto ya kisaikolojia.

"Nilikuwa tayari kuolewa tena ama kuanza mahusiano na mtu mwengine, lakini yaliyonitokea awali yananizuia. Kama inhgetokea leo, basi nisengekubali tena jambo kama lile."

***

Arif na Maleika (si majina yao halisi) ni wapenzi ambao waliunganishwa na jamaa zao.

Wamefunga ndoa, kwa mujibu wa tamaduni wamekaa pande mbili tofauti za meza, na meza yao pekee ndio haina kilevi.

Wamekaa wakiwaangalia wageni wao - kama watu 400 hivi - wakicheza na kufurahia. Maharusi hao hawaruhusiwa kupigana busu - haikubaliki kwenye jamii.

Illustration of three women in a car driving fast, two using binoculars

Lakini Maleika akaamua kunyanyuka, huku ndugu zake wakimshangaa, na kuanza kusakata dansi.

Wageni wakaanza kunong'onezana na kupiga umbea, wakimsema biharusi huyo kuwa hana aibu. "Hili si disko!" alilalama mwanamke mmoja.

"Anawezaje kuwa hivi! Haziheshimu kabisa mila zetu!" akalalama mwengine.

Wageni wanaonekana kutofurahia, lakini biharusi haoneshi kujali, anaongea na rafiki zake badala ya ndugu, na pia anaonekana kumchokoza mumewe kwa furaha.

Lakini hata Maleika hawezi kuikimbia mila ya kusimamiwa chumba cha pili kwenye usiku wa kwanza wa harusi.

Baada ya gari la wanandoa kutoka ukumbini, likafutiliwa kwa karibu na gari lengine lililobeba wanawake wanne.

Hata maharusi hawa vijana na wa kileo wanafahamu kuwa hawatakuwa faragha peke yao kwenye usiku wao wa kwanza kama wanandoa.

Picha na Magerram Zeynalov