DRC inaweza kukubaliwa kuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Image caption Rais wa DRC felix Tsishekedi amepokelewa na Magufuli hapo jana Jijini Dar Es Salaam

Rais wa Congo Felix Tsishekedi amefichua kuwa hivi karibuni DRC ilituma maombi ya uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo itaiondelea nchi hiyo vikwazo vya kibiashara, na kuongeza shughuli za kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama.

Tsishekedi amemaliza ziara yake ya siku mbili nchini Tanzania, huku akiweka wazi juu ya nia ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tsishekedi amesema kuwa tayari wametuma maombi kwa mwenyekiti wa EAC na Rais wa Rwanda Paul Kagame kujiunga na Jumuiya hiyo.

EAC kwa sasa ina nchi sita, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan Kusini.

Kama Congo ikikubaliwa itakua nchi ya saba.

Mbali na DRC, Somali iliomba pia kujiunga na jumuiya hiyo lakini bado suala hilo linajadiliwa.

Kwa mujibu wa Rais Tsishekedi, anataka kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu za maendeleo ya kiuchumi na usalama wa eneo hilo la Afrika.

"Tunataka kujiunga na tayari tumetuma ombi, itasaidia sana maendeleo ya Bara la Afrika na pia itasaidia kuleta amani upande wetu," amesema.

Kwa upande wa Rais wa Tanzania , amemsifu Tsishekedi kwa kufanya maridhiano na makundi kadhaa hasimu, na kuwawachilia wafungwa wa kisiasa waliokuwa mahabusu. Hiyo ni hatua muhimu katika kurejesha amani nchini DRC, alisema Magufuli.

"Tanzania inaunga mkono juhudi za amani kwasababu hazitasaidia tu katika kuleta hakikisho la amani na uthabiti ; amani pia itachochea maendeleo ya kiuchumi baina ya nchi za maziwa makuu na bara zima la Afrika kwa ujumla ," alisema.

Magufuli aliongeza pia nchi hizo mbili zina mahusiano ya kihistoria na ndio maana Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kusaidia katika utatuzi wa changamoto za DRC.

Image caption Tsishekedi akiangalia makontena katika Bandari ya Dar es salaam nchini Tanzania

Kwanini hasa DRC inataka kujiunga na EAC?

Jamhuri ya Congo ndio nchi yenye eneo kubwa na lenye utajiri wa maliasili mbalimbali ikiwemo madini, lakini changamoto kubwa ni usalama.

Kama nchi hiyo itajiunga na EAC wanaamini huenda usalama ukaimarika kwa nguvu za pamoja kutoka nchi wanachama.

Lakini pia DRC itafaidikia katika masuala ya ujenzi wa pamoja wa viwanda, miuondombinu ya pamoja na urahisi wa kupita kwa mizigo kuingia katika nchi wanachama.

Kwa sasa DRC ndio inaongoza kwa kuingiza makontena ya mizigo nchini Tanzania.

Toka ulipoanza mwaka huu mpaka sasa, DRC pekee imeingiza makontena milioni moja na laki tano.

Rais Tshisekedi amesema pia ziara yake nchini Tanzania ina lengo la kuzungumza na rais Magufuli juu ya namna ya kufikia amani ya kudumu nchini DRC.

Pia aliwashukuru walinda amani wa Tanzania wanaohudumu nchi yake chini ya mpango wa kikosi cha Umoja wa mataifa Monusco.

" Nimeongea na rais Magufuli kuhusu bandari ya Dar es Salaam port na Reli ya -Standard Gauge Railway (SGR) -ambayo imepangwa kufika Rwanda. Nilielezea kuhusu uwezekano wa kupanua zaidi mradi hadi DRC," alisema.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi wa mataifa ya Afrika utakaoleta maendeleo ya kudumu utafikiwa kupitia uwekezaji na utekelezwaji wa miradi ya miundombinu ,izikiwemo reli, barabara na nishati.

Mada zinazohusiana