Bobi Wine: je ni kwa nini mbunge huyu anataka kutekeleza sera za Museveni?

Bobi Wine akielekea gerezani Luzira Aprili 29 baada ya kukamatwana polisi siku mbili baada ya kutoka katika kizuizi cha nyumbani Haki miliki ya picha NICHOLAS BAMULANZEKI

Mbunge wa Kyadondo mashariki nchini Uganda Robert Kyagulani amesema kuwa atatekeleza ajenda 10 za rais Yoweri Museveni ambazo amekuwa akijaribu kuzitekeleza katika kipindi chake chote cha miaka 33.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, Kiongozi huyo amesema kuwa sera yake itakuwa utekelezaji wa ajenda hizo kwa kuwa hakuna hata moja ambayo imetekelezwa kufikia sasa.

Bobi Wine amesema kuwa utekelezwaji wa sera hizo umekumbwa na matatizo kutokana na ufisadi na ukosefu wa sheria uliopo nchini humo.

Amesema kuwa taifa hilo limekuwa na maono mengi kama vile Vison 2040 na mengine mengi ambayo yamewasilishwa na kuwekwa kando.

''Ndio tumekuwa na mipango mingi , ikiwemo ule wa Vison 2040 na mengine mengi . Haijatekelezwa kutokana na ufisadi mwingi. Hivyobasi lengo leti ni kutekeleza sera na mipango ambayo imependekezwa katika siku za nyuma'', aliambia gazeti la The Citizen nchini Tanzania.

Alisema: Lazima ifahamike kwamba Uganda haijakosa sera nzuri. Tumekuwa na mapendekezo chungu nzima na mengi yamefanyiwa utafiti wa hali ya juu na kuwasilishwa.

Uchaguzi mkuu 2021

Kyagulani ambaye ametoa ishara za kutaka kuwania urais nchini Uganda amesema kuwa ana matumaini ya upinzani kumshinda Museveni katika uchaguzi wa 2021 kwa kuwa vijana ni asilimia 85 ya idadi ya watu nchini humo.

''Na sio vijana tu, hata watu wazima pia wanatuunga mkono na kwamba watu wa Uganda sasa wameungana zaidi ya ilivyokuwa awali. Hivyobasi ndio nimesema awali na nasema tena sasa kwamba kundi langu nami tutakabiliana na rais Museveni katika uchaguzi utakaofanyika baada ya miaka mwili kutoka sasa'', alisema,

Ameongezea kwamba ijapokuwa hawajaafikia uamuzi wa mwisho amasema wanajaribu kuwaleta watu pamoja na nguvu zote zinazopigania mabadiliko kwa lengo la kuingia katika uchaguzi huo wakiwa kitu kimoja.

''Ndio tumezungumza lakini tuko wengi wanaotaka kuwania . Mmoja wetu kati yetu atachaguliwa na kupewa baraka kutuongoza na nasema iwapo kundi hilo litanipatia bendera mimi kuongoza niko tayari kushindana na Museveni''.

Alipoulizwa kuhusu kiwango cha wafuasi wake tangu aingie siasa alisema kuwa hakushangaa , kutokana na miaka mingi aliyohudumu kama mwanamuziki

Raia wanataka mabadiliko Uganda

Anasema kwamba katika mikutano yake na raia wengi -wamekuwa wakishinikiza mabadiliko ijapokuwa wanasiasa wengi ambao wamekuwa wakijitokeza wamekuwa wakinunuliwa, huku wengine wakitishiwa .

Amesema wengi wa wanasiasa hao vilevile wamekuwa wakijipandisha hadhi yao katika utawala huo wa kiimla bila ya kujali kuuzuia kupitia uchguzi.

Baada ya kuwaona raia wengi wakituunga mkono ni ishara cha kile ambacho kimekuwa kikijijenga miongoni mwao.

Alipoulizwa kuzungumzia kuhusu hali iliopo Sudan, Bobi Wine alisema kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kwamba raia wamechoshwa na uongozi wa kiimla.

''Ni sharti ikumbukwe kwamba Bashir alikuwa dikteta mkubwa , alikuwa na jeshi kubwa zaidi ya Museveni lakini aliondolkewa na uwezo wa raia.hivyobasi hilo linatupatia moyo wa kuamini na kuendelea kupigania demokrasia katika taifa letu''.