Shambulio la chuo kikuu cha Garissa Kenya: Mtanzania mmoja ni miongoni mwa washukiwa watatu waliopatikana na hatia

Washukiwa wanne wa shambulio la garissa wakisubiri hamta yao mahakamni. Sahal Diriye Hussein, kulia ndiye aliyeachiliwa huru

Chanzo cha picha, CGTN Africa

Maelezo ya picha,

Sahal Diriye Hussein, kulia aliachiliwa huru

Raia mmoja wa Tanzania ni miongoni mwa washukiwa watatu wa ugaidi nchini Kenya waliopatikana na hatia ya kutekeleza shambulio la mwaka 2015 katika chuo kikuu cha Garissa lililosababisha mauaji ya takriban wanafunzi 148.

Mtanzania huyo kwa jina Rashid Charles Mberesero pamoja na Hassan Edin na Mohammed Abdi jina jingine Mohamned Ali Abikar walipatikana na hatia ya kupanga shambulio hilo chini ya ushirikiano wa wanachama wa kundi la Al-Shabab.

Pia walipatikana na hatia ya kuwa wanachama wa kundi la al-shabab kutoka Somalia.

Mtu wa nne Sahal Diriye Hussein aliondolewa mashtaka.

Shambulio hilo lilitekelezwa na kundi la al-Shabab linaloshirikiana na lile la al-Qaeda katika Chuo hicho kikuu kilichopo kaskazini mashariki mwa Kenya.

Lilikuwa shambulio la pili baya zaidi katika historia ya Kenya , kufuatia shambulio la ubalozi wa Marekani nchini Kenya la 1988 ambapo zaidi ya watu 200 waliuawa.

Kwa kuwashambulia vijana na wataalam wa siku zijazo shambulio hilo lililenga kuathiri ukuaji wa uchumi na uthabiti wa taifa mbali na kuleta mgawanyiko wa kidini.

Wapiganaji wanne waliotekeleza shambulio hilo waliuawa katika eneo la mkasa huo huku mtu aliyepanga Mohammed Kuno akiuawa katika shambulio nchini Somalia 2016.

Mamlaka nchini Kenya ilikosolewa kwa kushindwa kuchunguza ripoti ya ujasusi uliotolewa kabla ya kufanyika kwa shambulio hilo , mbali na kuweka mikakati isiofaa wakati ilipokuwa aikijibu shambulio hilo.

Waathiriwa walisubiri haki kwa muda mrefu

Kulingana na mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza waathiriwa wa shambulio hilo kama Anastasia Mikwa wanaishi na makovu ya shambulio hilo.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 kutoka chuo kikuu cha Garissa alipigwa risasi mara kadhaa wakati wa shambulio hilo.

Licha ya kufanyiwa upasuaji mara 32 bado anategemea kuangaliwa na wazazi wake.

Maelezo ya video,

Shambulio la kigaidi Garissa: Mahakama Kenya yawapata 3 na hatia

Ijapokua uamuzi wa leo hautafuta ama hata kuwapatia nafuu waathiriwa kama yeye kuna matumaini ya kukamilishwa kwa kesi hiyo baada ya kuchukua takriban miaka minne.

Kesi hiyo ilikumbwa na mabadiliko ya mahakimu na mashahidi kutowasili mahakamani, hali ambayo ni kawaida katika mahakama za Kenya.

Uamuzi huo wa leo ni muhimu sana.

Uamuzi huo kwa njia nyengine pia ni ushindi kwa maafisa wa polisi wa Kenya na waendesha mashataka ambao wametuhumiwa kwa usimamizi mbaya kesi kama hizo.

Wakati wa shambulio hilo, wapiganaji walifyatua risasi kiholela mabali na kuwapiga risasi wale waliojitambulisha kuwa Wakristo.

Mohamed Kuno auwawa

Kiongozi wa shambulio la chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya ameuawa maafisa nchini Somalia wanasema.

Serikali ya Kenya ilisema kuwa Mohamed Kuno ndiye aliyepanga njama za shambulio hilo la mwezi Aprili 2015 ambapo takriban watu 148 waliuawa.

Vikosi vya Somalia vinasema kuwa ni miongoni mwa watu 16 waliouawa katika shambulio la usiku katika msafara wa magari mjini Kismayu ,mji wa Bandari uliopo kusini mwa Somalia.

Wanne ya wale waliouawa waliripotiwa kuwa maafisa wandamizi wa wapiganaji wa al-Shabab.

Mwandishi wa maswala ya usalama wa BBC barani Afrika Tomi Oladipo amesema kuwa habari hizo ni mafanikio makubwa kwa Somalia na washirika wake katika vita dhidi ya Alshabab.