Sheria ya Filamu: Manung'uniko kuhusu mswada wa mabadiliko ya sheria Tanzania

tasnia ya Filamu Tanzania

Manung'uniko yamezuka kufuatia kuwasilishwa kwa pendekezo la dharura la mswada wa mabadiliko ya sheria Namba 3 wa maka 2019 Tanzania unaotoa muongozo wa kazi katika sekta ya filamu.

Mswada huo unapendekeza kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya filamu na michezo ya kuigiza kudhibiti kazi zinazofanyika katika sekta hiyo nchini.

Mswada huo uliowasilishwa mwishoni mwa juma unapendekeza kuwa kampuni au mtu yoyote anayetengeneza filamu makala au matangazo ya biashara kwa kutumia picha za ndani ya nchi ya Tanzania anastahili kuwasilisha kanda zote zilizorekodiwa kwa bodi ya filamu nchini kabla ya uhariri wowote.

Kadhalika wahusika wanatakiwa kubaini maeneo yote ambayo wamerekodi na hatimaye kuwasilisha nakala ya mwisho ya makala, tangazo au filamu iliyotengenezwa kwa kutumia picha, za ndani au kuihusu Tanzania.

Mswada huo ambao ni mjumuiko wa mapendekezo ya maboresho ya sheria mbali mbali, ulibainishwa wiki iliyopita na kuwasilishwa kwa kamati ya bunge ya katiba na sheria kwa hati ya dharura - sasa mashirika yasio ya kiserikali kama vile la kutetea haki za binaadamu Amnesty International yanasema utakandamiza haki za kujieleza kwa kuidhinisha mchujo au uminywaji wa taarifa.

"Tanzania inastahili kuepuka kuchukua hatua nyingine ya hatari inayozidisha uchujaji wa taarifa kwa kulenga wazalishaji filamu wa nje ya nchi, baada ya kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari," amesema Sarah Jackson, mkuugenzi wa kieneo wa Amnesty International afrika mashariki, pembezoni mwa Afrika na katika eneo la ziwa makuu.

Kwa upande wake kituo na haki na sheria nchini Tanzania (LHRC) kinasema marekebisho hayo yanatoa mianya mipya ya kuchuja taarifa.

Maelezo ya sauti,

Sekta ya filamu imeendelea kukua kila kukicha nchini Tanzania

LHRC kimesema katika taarifa yake, kwamba mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ni mapana sana kiasi cha kuweka vikwazo hususani katika maudhui ya picha za video.

Majukumu ya Bodi ya Filamu (Marekebisho 18) ni mapana na yanajumuisha kudhibiti, kufuatilia, kutoa vibali, kuidhinisha na kusimamia.

Kituo hicho kimeeleza kwamba hayo yote hayajafafanuliwa kwa ufasaha hivyo kuishia kutoa mamlaka yasiyodhibitiwa kwa Bodi ya Filamu katika kusimamia maudhui.

'Pendekezo la 20 linatoa mamlaka yasiyo ya kawaida ya kudhibiti maudhui, ikisisitiza kwamba kila bango litakaloandaliwa na kubandikwa hadharani linapaswa kupitiwa na kuidhinishwa na Bodi ya Filamu' inasema taarifa ya LHRC.

Mswada huo unatarajiwa kuwasilishwa bungeni kujadiliwa kabla ya kupitishwa kuwa sheria Juni 27 wiki hii .