'Kiongozi wa mapinduzi' Amhara, Ethiopia auawa na polisi

Brigedia Jenerali Asaminew Tsige Haki miliki ya picha YOUTUBE/ALEM GENA TUBE
Image caption Jenerali huyo muasi aliachiwa kutoka jela mwaka jana

Kiongozi wa jeshi anayeshukiwa kuongoza jaribio la mapinduzi siku ya Jumamosi katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, ameuawa na polisi, vyombo vya habari vya taifa vinaripoti.

Brigedia Jenerali Asaminew Tsige aliuwa nje kidogo ya makao makuu ya jimbo la Amhara, mji wa Bahir Dar, ripoti zinaeleza.

Mkuu wa jeshi, Jenerali Seare Mekonnen pamoja na maaafisa wengine wanne waliuawa wakati wakizuia mapinduzi hayo, maafisa wameeleza.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametoa wito kwa raia wa Ethiopia kuungana dhidi ya nguvu za ''kishetani'' zenye nia ya kuigawa nchi yao.

Bendera zinapepea nusu mlingoti baada ya serikali kutangaza kuwa siku ya maombolezo.

Jenerali Saare na Gavana wa Amhara, bwana Ambachew Mekonnen ambaye pia aliuawa Jumamosi, walikuwa wakionekana kama washirika wakubwa wa Waziri Mkuu Abiy.

Vikosi vinavyounga mkono serikali vimepelekwa makao makuu ya mji wa Bahir Dar, pamoja na mji mkuu wa nchi Addis Ababa.

Kiongozi wa Jeshi nchini Ethiopia auawa

Jenerali Seare Mekonen aliyeuawa Ethiopia ni nani?

Mwasiliano ya intaneti yamezimwa nchi nzima, ikiwa ni siku chache tu toka mawasiliano hayo yaliporejeshwa baada ya kukatwa pasi na kutolewa sababu kwa wiki nzima.

Serikali ya Marekani imetahadharisha wafanyakazi wake mjini Addis Ababa kubaki majumbani.

Mapigano yameikumba Amhara na maeneo mengine ya Ethiopia miaka ya hivi karibuni.

Tangu kuchaguliwa kwake mwaka jana, Bwana Abiy amekuwa na nia ya kumaliza mivutano ya kisiasa kwa kuwaacha huru wafungwa wa kisiasa, kuondoa marufuku dhidi ya vyama vya siasa na kuwashtaki maafisa wanaoshutumiwa kukiuka haki za binaadamu.

Ethiopia ni nchi ya pili yenye watu wengi barani Afrika (baada ya Nigeria), ikiwa na watu milioni 102.5 kutoka kwa zaidi ya makabila 80.

Ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi , lakini idadi kubwa ya vijana nchini Ethiopia hawana ajira.

Brigedia Jenerali Asaminew Tsige ni nani?

Brigedia Jenerali Asaminew Tsige, alikuwa ni mkuu wa usalama wa jimbo la Amhara.

Alikuwa ni miongoni mwa maafisa wa juu wa jeshi walioachiwa huru mwanzoni mwa mwaka jana baada ya serikali iliyopita kuwaachia wafungwa wa kisiasa kutokana na msukumo kutoka kwa umma.

Jenerali huyo alikuwa gerezani kwa miaka tisa akishutumiwa kupaga mapinduzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza, la Reuters, maafisa wa juu wa Amhara walifanya mkutano siku ya Jumamosi kujadili majaribio ya jenerali ya kuwasajili wanamgambo.

Brigedia Jenerali Asaminew kwa wazi kabisa aliwashauri watu wa Amhara mwezi huu kujihami kwa silaha, katika video iliyosambaa kwenye mtandao wa Facebook na kushuhudiwa na mwanahabari wa Reuters.

Tunafahamu nini kuhusu mashambulizi?

Kiongozi wa jeshi la Ethiopia, Jenerali Seare Mekonnen, aliuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake siku ya Jumamosi jioni, mlinzi wake tayari anashikiliwa na polisi, idara ya habari ya ofisi ya waziri mkuu imeeleza.

Alikuwa kwenye makazi yake na Jenerali mwingine,Gezai Abera,ambaye aliuawa, iliongeza taarifa hiyo.

Haki miliki ya picha Ethiopian TV

Serikali imesema ilikuwa na sababu kufikiri kuwa mashambulizi hayo yana uhusiano na mauaji dhidi ya gavana wa Amharam Ambachew Mekonnen, yaliyotokea saa kadhaa mjini Bahir Dar kabla ya kuuliwa kwa mkuu wa jeshi.

Bwana Ambachew aliuawa akiwa kwenye mkutano ofisini sambamba na msaidizi wake mkuu, Ezez Wasie, huku mwanasheria akijeruhiwa.

Lake Ayalew kwa sasa ameteuliwa kuwa gavana wa eneo hilo.

Haki miliki ya picha Reuters

Watu wengi waliohusika katika jaribio la mapinduzi wamekamatwa na operesheni ya kuwatia mbaroni wengine inaendelea, Ofisi ya habari ya waziri mkuu imeeleza.

''Jaribio la Amhara ni kinyume cha katiba na lina nia ya kuvuruga amani katika mji huo,'' taarifa hiyo imeeleza.

Siasa mbaya

Hiki ni kipindi kigumu kwa Ethiopia na Waziri Mkuu Abiy, ambaye anakabiliwa na mizozo ya wenyewe kwa wenyewe.

Kiongozi wa kijeshi Seare Mekonnen alitumikia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja baada ya kuteuliwa na waziri Abiy, ambaye alifanya mabadiliko kwenye idara ya usalama alipoingia madarakani mwezi Aprili mwaka jana.

Ni wazi kuwa Waziri Mkuu anakabiliwa na upinzani kutoka ndani ya jeshi ambao wanapinga mtindo wake wa utawala.

Umuhimu wa Amhara

Ardhi ya jamii ya Amhara ni eneo la pili kwa watu wengi na umelipa Ethiopia lugha ya taifa hilo, Amharic.

Mapigano kati ya jamii ya Amhara na Gumuz yaligharimu maisha ya watu mwezi uliopita mjini Amhara na mji jirani wa Benishangul Gumuz.

Mapigano kati ya jamii hizo yalisababishwa na migogoro ya ardhi, takribani watu milioni tatu walikimbia makazi yao.

Suala jingine ambalo Waziri Mkuu anapaswa kukabiliana nalo ni kutokuwepo kwa hali ya utulivu ndani ya jeshi.

Mwezi Oktoba, alisema kuwa mamia ya wanajeshi ambao waliandamana kuelekea kwenye ofisi yake kudai ongezeko la mshahara walitaka kumuua.

Abiy alikoswakoswa na shambulio la guruneti katika mkutano mwezi Juni mwaka jana.Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu wawili na zaidi ya 100 walijeruhiwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii