Mbunge wa Kenya 'aliyetishia' Watanzania na Waganda akamatwa

jAGUAR Haki miliki ya picha Citizen TV

Maafisa wa polisi nchini Kenya wamemkamata mbunge wa jimbo la Starehe anayedaiwa kutoa kauli za chuki dhidi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda waliopo jijini Nairobi.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaripoti kuwa Charles Kanyi Njagua maarufu kama Jaguar amekamatwa mchana huu akiwa anatoka kwenye viwanja vya bunge.

Tayari ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai kupitia ukurasa wake wa Twitter imesema mbunge huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kuchochea ghasia.

Katika kanda ya video iliosambazwa pakubwa nchini Kenya na katika nchi jirani Tanzania, mbunge huyo alisema hawatokubali watu wa nje waje kuendesha biashara nchini.

''Wakenya ni sharti wafanye biashara zao bila kushindana na watu kutoka mataifa mengine. Raia wa Pakistan wametawala biashara za kuuza magari nchini humu, Watanzania na Waganda wanatawala katika masoko yetu. Tunasema imetosha iwapo hawatarajeshwa nyumbani katika saa 24 tutawashika na kuwapiga na hatuogopi mtu yeyote'', alinukuliwa akisema.

Licha ya Serikali ya Tanzania kuwaomba raia wake kuwa na utulivu na serikali ya Kenya kujitenga na matamshi ya mbunge huyo, bado gumzo linaendelea katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakimtaka mbunge huyo aombe radhi kwa matamshi yake.

Jaguar hii leo kwa kutumia mtandao wake wa Twitter amedai kuwa matamshi yake hayo yametafsiriwa vibaya.

"Nataka amani kwenye nchi na biashara ziendelee bila kuingiliwa na wageni wote wanakaribishwa nchini mwetu," ameandika Jaguar kupitia mtandao wa Twitter.

Soko kubwa la mitumba la jijini Nairobi la Gikombaa lipo ndani ya jimbo la Starehe.

Matamshi hayo yameibua mzozo wa kidiplomasia, huku Tazania ikimuita balozi wa Kenya nchini humo Dan Kazungu kujieleza juu ya kauli hiyo.

Waziri Mkuu wa Tanzania aliliambia Bunge kuwa Kenya imeihakikishia serikali ya Tanzania kuwa matamshi hayo ya chuki si msimamo wa serikali na kuwa Watanzania wataendelea kuwa salama nchini Kenya.

''Sisi kama Watanzania tuendeleeni kuishi na amani na Wakenya hatuna matatizo nao,'' alisema Majaliwa.

Tayari serikali ya Kenya kupitia msemaji wake kanali mstaafu Cyrus Oguna imetoa taarifa yake ikisema kuwa matamshi ya mbunge huyo ni ya kibinafsi na kwamba sio msimamo wa serikali ya Kenya.

'' Tungependa kusema kuwa huo sio msimamo wa serikali ya Kenya na tunashutumu matamshi hayo yaliotolewa katika kanda hiyo ya video. Matamshi hayo hayafai katika ulimwengu wa sasa'', alisema Oguna.

''Wakenya ni wapenda amani ambao kwa miaka mingi wameishi na raia wengine wa kigeni bila tatipo lolote. Hii ni thamani ambayo tunajivunia kama taifa na ni lazima tuendelea nayo'', ilisema taarifa hiyo iliotiwa saini na msemaji huyo wa serikali.

Mada zinazohusiana