Eric Trump anasema kuwa muhudumu alimtemea mate katika baa moja Chicago

Eric Trump, mwana wa rais wa Marekani Donald Trump ataembea nje ya jumba la Trump Tower mnamo mwezi Agosti 2017 mjini New York Haki miliki ya picha Spencer Platt/Getty Images
Image caption Eric Trump, akiwa mjini New York

Eric Trump, mwana wa kiume wa rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa alitemewa mate katika baa moja ya kifahari mjini Chicago .

''Kilikuwa kitendo cha kuchukiza na mtu ambaye ana matatizo ya kihisia'' ,bwana Trump aliuambia mtandao wa Breitbart wa mrengo wa kulia.

Mfanyakazi huyo alihojiwa na majasusi na baadaye kuachiliwa , kulingana na chombo kimoja cha habari.

Baa hiyo ilithibitisha kwamba kisa kisichokuwa cha kawaida kilimkumba mwana huyo wa Trump.

''Hatukushuhudia kisa hicho na ndio tunaanza kujua kilichotokea'', ilisema baa hiyo katika taarifa yake.

''Kile kinachojulikana ni kwamba hakuna mteja anayefaa kutemewa mate''.

Bwana Trump aliambia mtandao wa Breitbart kwamba alikataa kuwasilisha malalamishi dhidi ya mfanyakazi huyo ambaye amepewa likizo ya lazima na baa hiyo.

Msemaji wa idara ya polisi ya mjini Chicago amethibitisha katika mtandao wa Twitter kwamba maafisa waliwasaidia majasusi hao siku ya Jumanne jioni na kisa cha ukiukaji wa sheria lakini hawakuelezea zaidi.

Kisa hicho kilitokea katika baa ya Aviary, mgahawa maarufu ulioshinda tuzo la James Beard katika jimbo la Chicago eneo la West Loop.

Kulingana na chombo kimoja cha habari katika eneo hilo , bwana Trump alikuwa katika baa hiyo mwendo wa 01:30 GMT siku ya Jumanne wakati alipotemewa mate na mfanyakazi.

Mmiliki mwenza wa baa hiyo Nick Kokonas , aligonga vichwa vya habari mnamo mwezi Januari mwaka huu wakati alipoialika timu ya Clemson Tigers, mabingwa wa ligi ya soka nchini humo chakula cha jioni kusherehekea katika mgawaha wake wa Alinea baada ya ya rais kuwaalika na kuwapatia wachezaji hao chakula cha haraka katika ikulu ya Whitehouse.

Rais Trump ambaye alikuwa mwenyeji wa timu hiyo alitoa fedha zake binfasi kulipia maankuli hayo.

Bwana Trump ambaye ni naibu wa rais wa shirika la Trump alikuwa mjini Chicago kutembelea hoteli ya Trump.

Haki miliki ya picha Alex Wong/Getty Images
Image caption Eric Trump ni mwana wa tatu wa rais wa Marekani Donald Trump

Aliambia mtandao wa Breitbart kwamba anaamini tukio hilo lilishinikizwa kisiasa.

''Kwa chama kinachoeneza injili ya uvumilivu hiki chama cha Democrats hakina tabia nzuri,'' alisema mwana huyo wa tatu wa rais Trump akidai kwamba mfanyakazi huyo alikuwa mwanachama wa Democrat.

''Hatua hiyo inasisitiza kuwa wamekata tamaa kutokana na ukweli kwamba tutaibuka washindi''.

Madai hayo ya kutemewa mate ni miongoni mwa msururu wa visa ambapo mtu wa familia ya rais Trump amenyanyaswa ama hata kukaripiwa kutokana na sera tofauti wakati anapokula.

Mnamo mwezi Juni mwaka jana ,wanarahakati walimzoma katibu wa kampuni ya Homeland Security Kristjen Nielsen katika mgahawa mmoja mjini Washington DC .

Siku chache baadaye aliyekuwa katibu wa maswala ya vyombo vya habari Sarah Sanders alitakiwa kuondoka katika mgahawa wa Lexington , Virginia kwa kuwa alikuwa akiufanyia kazi utawala wa rais Trump.

Mada zinazohusiana