Utafiti waonyesha mchezo wa kamari unapopendwa na vijana unaenea kwa kasi

Vijana katika kituo cha kucheza kamari cha Betin jijini Nairobi, baadhi wanasema hawana ajira
Image caption Vijana katika kituo cha kucheza kamari cha Betin jijini Nairobi, baadhi wanasemaukosefu wa ajira ndio sababu inayowafanya wacheze

Mchezo wa kamari unaendelea kuenea barani Afrika haswa miongoni mwa mashabiki wa soka. Ni biashara sasa iliyo na thamani ya mabilioni ya dola kwa kampuni zinazoendesha biashara hii, lakini si vile kwa wanaocheza, amebaini mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi.

Alipotembelea Katika chumba kimoja katikati mwa jiji la Nairobi, aliwapata vijana kadhaa wakiwa wamesimama wakitizama televisheni kwa umakini, huku wakiwa wameshilia risiti mikononi. Walikuwa ndani ya chumba cha kucheza kamari, kwa ajili ya kujaribu bahari yao.

Mara nyingi mchezo wa kamari huchezwa kwa timu za kandanda za bara Ulaya , lakini kwa sasa msimu uko likizoni. Katika televisheni ni michezo ya kandanda bandia iliyotengenezwa kwa kompyuta, ambapo wachezaji wanakuwa ni vibonzo, lakini bado wanakamari wanacheza kutambua mshindi baina ya timu mbili bandia.

Katika televisheni nyingine kuna mashindano ya vibonzo vya mbwa , lakini wachezaji hawajali, wanaendelea kubahatisha, anasema Omondi ambaye alitembelea kituo kimoja cha Kamari jijini Nairobi.

Image caption Asilimia 75 ya wakenya walio na umri wa chini ya miaka 35 wamewahi kucheza kamari

Dommie, ni kijana ambaye hana kazi hufika kwenye kituo cha kamli kujaribu bahati yake: ''Sisi kama vijana tunajaribu kutafuta kazi hatuna, tumekuja kupata pesa ya rahisi hapa, sio eti nanajua nitapata nini, hii ni kubashiri tu''

Ahadi ya kupata ushindi mkubwa ndio kivutio kikubwa Zaidi kwa wachezaji hawa. Utafiti uliofanywa na kampuni ya Geopoll unaonyesha kwa taifa la Kenya ndilo linaloongoza barani afrika kwa wachezaji kamari. Asilimia 75 ya wakenya walio na umri wa chini ya miaka 35 wamewahi kucheza kamari.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa mujibu wa utafiti huo. Wengi wanacheza kwa urahisi kwa njia ya simu. Mmoja wao ni Justin Sanyo, ambaye anasema kuwa, japo ni mwanasayansi aliye na mshahara wake, hawezi akakosa kutenga kiasi cha mshahara wake kucheza kamari.

''Baadhi yetu wamechukua mchezo wa kamari kama kazi, na kwa wengine ni tabia ya kila siku. Ila tunafahamu kwamba kamari ni biashara, na wenye makampuni wanataka tupoteze fedha ili wapate faida. Kwa hivyo tahadhari ukiwa unacheza, uchague kwa makini sana timu utakazofanya nazo kamari''.

Kwa kuwa uwezekano wa kupoteza pesa ni mkubwa kuliko wa kuzipata, kwa wasio na kazi kama Dommie, ni kuhatarisha hela zao kidogo walizo nazo. Alipoulizwa ikiwa ataweza kuuacha mchezo huo alisema: '' Huu ni mchezo ambao nimejiingiza, lakini usipende mtoto wako ajiingize kwenye mchezo huu, au mtu wako. Mimi nimesoma niko na vyeti vyangu vimelala nyumbani, wakinipatia kazi mimi nitaacha, lakini sasa nitaachacje mchezo huu wakati ninakuja kubahatisha''.

Image caption Wachezaji kamari wameufanya mchezo huu kuwa biashara ya thamani ya mabilioni ya dola Afrika na ulimwenguni.

Wachezaji kamari wameufanya mchezo huu kuwa biashara ya thamani ya mabilioni ya dola Afrika na ulimwenguni. Sasa serikali pia zinataka haki zao kwa njia ya kodi.

Nchini Kenya makampuni ya kamari hutozwa asilimia 30 ya mapato kama kodi, lakini katika bajeti ya nchi iliyosomwa hivi karibuni, serikali imeongeza kodi nyingine ya asilimia kumi kwa kila hela ilayowekwa kama kamari ama dau.

Kumaanisha kuwa mchezaji atatozwa hata kabla hajashinda chochote. Ikiwa hatua hii itawavunja moyo wachezaji au la, ni swala la kusubiriwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii