Simu yako ya Smartphone huenda ni jasusi na huna habari

Nani anaweza kufikia data yako binafsi? Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Nani anaweza kufikia data yako binafsi?

Kwa watu wengi duniani kuwa na simu za kisasa za aina ya smartphone ni fursa ya kufikia ulimwegu lakini maswali yameibuliwa ikiwa fursa hiyo inatoa mwanya wa kufikiwa kwa maisha yao binafsi.

Hebu tafakari ikiwa wadukuzi watakuwa na uwezo wa kufikia simu yako na kuchukua kila kitu kilicho ndani yake ikiwa ni pamoja na ujumbe mfupi - na pia kudhibiti kinasa sauti na kamera yake?

Ukweli ni kwamba haya ni mambo yanayofanyika katika ulimwengu wa sasa japo huenda usiamini hilo linawezekana.

Lakini ni nani anayefanya hivyo na kwa nini?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kamera ya simu ni sawa na jicho la mwanadamu - inaona kila kitu mbele yake

Programu ya hali ya juu inayoorodheshwa kama silaha

Mike Murray, ni mtaalamu wa usalama wa kimtanda katika kampuni ya Lookout mjini San Francisco, inayosaidia serikali, biashara na watu binafsi kuhakikisha taarifa zao za kibinafsi ziko salama.

ANAelezea jinsi programu za udukuzi zinavyobuniwa na vile zinavyofanya kazi: programu hiyo imeorodheshwa kuwa silaha ya kiwango cha juu amabyo inauzizwa kwa udhibiti mkubwa.

"Wataalamu wa programu za ujasusi wanaweza kukufikia kupitia mfumo wa GPS," anasema Mike.

"Wanaweza kuwasha kipaza sauti na kamera wakati wowote na kurekodi kila kitu kinachofanyika katika mazingira yake.

Inaiba nambari ya siri ya kufikia app ya mitandao ya kijamii ulizo nazo; kuiba picha, nambari ya za watu ulizo nazo katika simu yako, taarifa zako za siri, barua pepe zako, nastakabadhi zingine muhimu ulizo nazo."

"Yaani inageuza simu yako kuwa kifaa cha uwizi ambacho wanaweza kukisikiliza wakati wowowte wanapotaka kukufuatilia - na kuiba klila kitu kilichopo ndani yake."

Programu za ujasusi zimekuwepo kwa miaka kadhaa, lakini hizi za sasa zimefikia kiwango cha juu zaidi duniani.

Programu hi ya sasa haifikii data ambayo imefichwa kwenye simu yako kupitia mfumu unaoziba mawasiliano maandishi kati ya watu wawili, lakini imekuwa ikishindana na mfumo huo kupitia teknolojia ya kisasa ambayo inaendelea kuimarishwa kila uchao.

Kukamatwa kwa mlanguzi mkuu wa dawa za kulevya Mexico

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mlanguzi mkuu wa dawa zakulevya"El Chapo"alijaribu sana kujificha lakini alisakwa na kukamatwa kupitia programu za ujasusi zilizotumiwa kudukua simu yake

Mlanguzi sugu wa dawa za kulevya nchini Mexican El Chapo alikuwa akimiliki himaya ya thamani ya mabilioni ya madola.

Baada ya kutoroka jela alienda mafichoni kwa miezi sita, kwa usaidizi wa mtandao wake wa wahalifu - na alikuwa akiwasiliana kupitia simu ambayo ilikuwa vigumu kudukuliwa na majasusi.

Lakini mamlaka ya Mexico iliponunua programu mpya ya ujasusi iliyoisaidia kufikia simu yake na ya washirika wake waliokuwa mafichoni.

Kukamatwa kwa El Chapo kunaashiria jinsi programu hiyo inavyoweza kutumiwa kama silaha ya kukabiliana na ugaidi na wahalifusugu kwa kushirikiana na makampuni ya simu.

Je simu ya mtu anayekosea serikali yake yuko hatarini kudukuliwa?

Mwanablogu wa Uingereza aliyelengwa

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Utajuaje uhalisia wa barua pepe unazotumiwa?

Rori Donaghy ni mwanablogu ambaye anaendesha shughuli zake za kimtandao Mashariki ya kati.

Kupitia mtandao huo alaikuwa akiripoti visa vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu vinavyotekelezwa na taifa la Falme wa Milki za kiarabu, kuanzia jinsi wafanyikazi wahamiaji na watalii wanaokiuka sheria za nchi hiyo walivyokuwa wakidhulumiwa.

Alipata wasomaji wengi waliokuwa wakifuatilia taarifa zake mitandaoni. Lakini haikuchukua muda mrefu alianza kupata barua pepe kutoka kwa watu asiowafahamu.

Rori aliwasilisha moja ya barua pepe hizo kwa kundi la utafiti linalofahamika kama Citizen Lab, lenye makao yake katika Chuo Kikuu cha Toronto, ambalo linachunguza jinsi ujasusi wa kidijitali unavyotumiwa kuwalenaga waandishi wa habari na wanaharakati wa kutetea haki zabinadabu.

Walithibitisha link zilizoambatanishwa katika barua pepe alizokuwa akitumiwa zilikuwa zitumiwe kudukua mitambo yake na pia kuwafahamisha wadukuzi hao ulizni anaotumia kulinda vifaa vyake vya kazi.

Watu waliokuwa wakimtumia Rori barua pepe hizo waligunduliwa kuwa majasusi wanaofanya kazi kwa niaba ya serikali ya UAE government mjini Abu Dhabi.

Serikali ilikuwa na hofu huenda mtandao unaoendeshwa na Bw. Rori huenda unashirikiana na makundi yenye itikadi kali ambayo huenda yakawa tisho kwa usalama wa kitaifa.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanaolengwa

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kuwa makini kuhusu vitu unavyobofya katika screen ya simu yako

Mwanaharakati maarufu ambaye pia alishinda Tuzo kwa kutetea haki za kibinadam, Ahmed Mansoor, amekuwa akilengwa na shirika la kijasusi la Falme za Kiarabu kwa miaka mingi.

Mwaka 2016 alipata ujumbe wa kutilia mashaka, ambao pia aliusambaza kwa The Citizen Lab.

Kwa kutumia simu aina ya iPhone ambayo haina programu yoyote, timu ya utafiti ilibofya linki na kile walichokiona kiliwashangaza: ilikuwa ni simu ya smartphone inayoonesha data licha ya kwamba haina programu yoyote.

Simu aina ya iPhone imetengenezwa kwa kuzingatia usalama lakini programu moja ya kisasa zaidi iligundua shimo lililotokana na mdudu kwenye mfumo wa simu ya Apple.

Kampuni ya Apple ililazimika kumfahamisha kila moja duniani kote.

Bado haijafahamika ni taarifa gani zilizopatikana kwa simu ya Mansoor lakini alitiwa mbaroni na kufungwa kifungo cha miaka kumi gerezani.

Kwa sasa amezuiliwa katika eneo ambalo hawezi kutangamana na wengine.

Balozi wa Falme za Kiarabu nchini London ameiambia BBC kwamba taasisi zao za usalama zinatimiza viwango vya kimataifa na sheria za ndani ya nchi lakini kama nchi zingine haiwezi kuzungumzia chochote kuhusu masuala ya kiusalama.

Wanahabari wanaolengwa

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Nini kinachofanyika mtu usiyemjua akifuatilia mawasiliano yako ya simu?

Mwezi Oktoba mwaka 2018, mwanahabari Jamal Khashoggi aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul na hakuwahi kuonekana tena, baada ya madai kuibuka kuwa aliuawa na maajenti wa utawala wa nchi hiyo.

Rafiki wa mwanahabari huyo, Omar Abdulaziz, alidai kuwa simu yake ilidukuliwa - na watu aliosema ni - maafisa wa serikali ya Saudi Arabia.

Omar anaamini kuwa udukuzi huo ulichangia pakubwa mauaji ya mwanahabari huyo maarufu ambaye alikuwa akilengwa na serikali.

Anasema walikuwa wakiwasiliana sana na katika mazungumzo yao waliangazia siasa za taifa lao pamoja na miradi ya maendeleo waliokuwa wakishirikiana kufanya.

Kwa muda mrefu serikali ya Saudia ilikuwa ikifikia mawasiliano hayo na hata nyaraka walizokuwa wakitumiana kupitia simu zao.

Serikali ya Saudi Arabia katika tamko lake kuhusu madai hayo ilisema japo kuna programu za zinazotumika kudukua simu za watu kisiri hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa ilihusika na madai yanayotolewa dhidi yake kuwa ilidukua simu ya mwanahabari huyo aliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha.

Udukuzi unavyozidi kukukaribia

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption "Zero click technology" huenda ikawa jia rahisi ya kufikia programu katika simu yako

Mnamo mwezi Mei mwaka huu, kulikuwa na udukuzi wa hali ya juu wa mtandao wa kijamii wa WhatsApp, app ambayo watu wengi duniani hutumia kuzungumza na marafiki na familia karibu kila siku.

Kama ulidhani udukuzi huo ulimaanisha tu kuwa mtu anaweza kusikiliza mawasiliano ya simu kupitia Whatsapp basi itabidi utafakari upya.

Udukuzi wa mtandao huoo ilikuwa na uwezo wa kuvuruga program nzima ya simu, punde ukishafunguliwa, mdukuzi ana uwezo wa kupakua programu ya kuweza kufuatilia kila kitu katika simu ya muathiriwa.

Aliyeathirika na udukuzi hakuhitaji hata kubofya kiunganishi chochote, simu yake iliweza kudukuliwa kwa yeye tu kupiga simu na kisha kuikata.

Hii inajulikana kama teknolojia ya pasi kubonyeza. Whatsapp ilichukua hatua za dharura kuwalinda watumiaji wake bilioni 1.5 lakini hakuna ajuaye nani alihusika na udukuzi huo.

Whatsapp ililengwa kipindi hiki lakini suali ni je, ni App ipi itakayolengwa katika siku zijazo?

Kukabiliana nao

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Watengenezaji wa programu kama hii ya ujasusi, huhitaji leseni maalum ya kuuza programu yao katika mataifa ya ng'ambo

Programu ya ujasusi huchukua muda gani kabla kugunduliwa?

Watengenezaji wa programu kama hii ya ujasusi, huhitaji leseni maalum ya kuuza programu yao katika mataifa ya ng'ambo, sawia na ilivyo na kandarasi za kijeshi.

Programu hiyo inauzwa kwa minajili ya kuwazuia wahalifu. Lakini mahabari hiyo ya Citizen Lab, wamegundua kile wanachoamini kuwa ni utumizi mbaya wa programu hiyo na serikali zilizoinunua.

Je waundaji wa programu hii wanapaswa kuwajibishwa kuhusiana na utumizi mbaya?

Tofauti na silaha zingine kama bunduki, mfumbuzi wake amesalia katika secta ya huduma na pia kutoa muongozi na ufundi baada ya kuuza programu hiyo.

Lakini je wao watahusika ikiwa programu hiyo itatumia vibaya baada ya kuiuza?

Kampuni inayoongoza katika sekta ya udukuzi halali na unaoruhusia na kampuni moja ya Israeli inayoitwa NSO Group.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Usibonyeze link ya barua pepe usiokuwa na hakika imetumwa na nani

Kampuni hiyo imekuwepo kwa takriban muda wa muongo mmoja na hupata mamilioni ya madola kila mwaka.

Wakili wa Bwana Abdulaziz ameishtaki kampuni hiyo mahakamani kwa madai ya kudukua simu ya mteja wake.

Ni wakati muhimu sana na itasaidia kubainisha majukumu ya kampuni za kutengeneza programu za udukuzi baada ya programu zao kuuzwa.

Kampuni ya NSO imekataa kutoa tamko lolote lakini kwenye taarifa kampuni hiyo imesema kuwa teknolojia ya inazipa tasisi za serikali zilizopewa leseni vifaa wanavyohitaji kuzuia na kuchunguza uhalfu na kuwa teknolojia yao imeokoa maisha ya watu wengi.

Wakili huyo sasa amedai kuwa ameanza kupokea simu kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kutoka watu wasiojulikana.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii