Lissu: Tunaenda Mahakama Kuu ili iseme kama kweli sijulikani nilipo

Lissu akihojiwa na BBC

Mwanasiasa mwandamizi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Antipas Lissu anapanga kwenda Mahakama Kuu nchini Tanzania kupinga kuvuliwa ubunge.

Lissu ameiambia BBC kuwa ataenda mahakamani muda mfupi baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kulitangazia bunge la nchi hiyo Ijumaa Juni 28 kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kuileleza kuwa jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na Lissu kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema lipo wazi.

Mwanasiasa huyo pia ameiambia BBC kuwa yeye si mtoro bungeni na yungali anapokea matibabu barani Ulaya.

Spika Ndugai ametaja sababu kuu mbili zilizomsukuma kuiandikia tume ya uchaguzi barua hiyo, mosi ni kutokana na Lissu kutokuhudhuria bungeni kwa muda mrefu na pili kutokuwasilisha fomu ya tamko la mali na madeni kwa sekretari ya maadili kwa mujibu wa sheria.

Lakini Lissu amezipinga hoja zote mbili, akisema hashangazwi na tamko la Spika Ndugai.

"Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa," amesema Lissu na kuongeza, "Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge... kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu."

Japo inafahamika kuwa mwanasiasa huyo alilazimika kusafirishwa nje ya Tanzania awali nchini Kenya na kisha Ubelgiji kwa matibabu baada ya shambulizi dhidi yake, kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya kutokuwepo kwake bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Haki miliki ya picha Bunge, Tanzania
Image caption Spika Ndugai

Hivi karibuni ikiwa yungali ughaibuni amezuru nchi za Marekani, Ujerumani na Uingereza, kote huko, amehojiwa na vyombo vya habari za kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu juu ya hali ya haki za binaadamu Tanzania.

Hali hiyo iliibua hoja miongoni mwa wakosoaji wake kuwa tayari amepona na anastahili kurudi Tanzania.

Spika Ndugai mwezi Februari mwaka huu alikubali kufanyia kazi hoja ya kuzuia stahiki zake kama mshahara kwa madai hayo, na kusema kuwa hana taarifa rasmi juu ya alipo Lissu na hali yake ya kiafya, na amekuwa akimuona kwenye vyombo vya habari.

Na wakati akitoa taarifa juu ya kuvuliwa ubunge wake Spika Ndugai ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa bado hana taarifa rasmi ya alipo Lissu na anachokifanya kwa sasa huko alipo.

"Katiba yetu inasema, katika mazingira yote mawili (kutooneka bungeni bila taarifa rasmi, na kutowasilisha tamko la mali na madeni) ubunge wake unakoma na ataacha kiti chake, ndiyo lugha inayotumika na katiba…kwa hiyo unakuwa umejifuta mwenyewe ubunge, hujafukuzwa na mtu," amesema Spika Ndugai.

Lissu amesema nini hasa?

"Ni aibu kwa Spika wa Bunge kusema hajui nilipo, ilhali dunia nzima inajua nipo Ubelgiji na naendelea na matibabu. Kila siku mimi naenda hospitali kufanya tiba ya mazoezi, siwezi kutembea bila kufanya mazoezi hayo," amesema Lissu na kuongeza; "Ofisi ya bunge inajua fika niipo. Katibu wa Bunge ameshawahi kuwasiliana kwa barua na kaka yangu kuhusu matibabu yangu na nakala ya barua iliyotumwa na katibu ilinifikia nikiwa hospitali Ubelgiji. Wanajua nilipo."

Lissu amesema kufuatia kauli hiyo ya Spika, anawasiliana na mawakili wake nchini Tanzania ili wamwandikie kuomba nakala ya barua alotuma tume ya uchaguzi na pia kuiomba tume hiyo iwape nakala ya barua kutoka kwa Spika.

Hatua itakayofuata baada ya hapo ni kulifikisha suala hilo Mahakama Kuu.

"Tunaenda Mahakama Kuu ili iseme kama kweli Spika hajui nilipo, na kwa nini sipo Bungeni. Pia iseme kwa mazingira yangu na yaliyonikuta kama jimbo lipo wazi," amesema Lissu.

Lissu anaamini hatua ya Spika imekuja wakati huu kwa sababu ametangaza kuwa atarejea Tanzania mwezi wa tisa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Lissu amekuwa nje ya Tanzania kwa matibabu toka Septemba 2017, amsema tarejea nyumbani atakaporuhusiwa na madaktari wake.

"Hawa watu wana hofu juu yangu, wana hofu juu ya Septemba 7 siku nitakayorudi Tanzania. Siku ambayo itatimu niaka miwili kamili toka niliposhambuliwa. Hakuna cha kunizuia kurudi," amesisitiza.

Lissu alikuwa miongoni mwa wanansiasa wa upinzani waliopendelea kumuita Magufuli kuwa 'Dikteta Uchwara' ama kwa lugha ya kingereza'Petty Dictator'.

Baada ya shambulio hilo, alikimbizwa Nairobi kwa matibabu kisha Brussels Ubelgiji toka mwezi Januari mwaka 2018.

Huko kote aliendelea kusisitiza kuwa serikali ya Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Hata hivyo, katika miezi ya hivi karibuni Lissu ametoka Ubelgiji na kuzuru nchini Uingereza na kufanya mahojiano na runinga ya BBC, Kisha akazuru Ujerumani na kufanya mahojiano na runinga ya DW.

Kote huko, Lissu ambaye ni mbunge kupitia chama cha upinzani cha Chadema ameendelea kusisitiza kuwa serikali ya rais John Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Pia amelishambulia Bunge chini Spika Job Ndugai kwa 'kumtelekeza' na kushindwa kulipia matibabu yake nje ya nchi.

Lissu pia amekuwa akilituhumu bunge chini ya Spika Job Ndugai kwa 'kumtelekeza' na kushindwa kulipia matibabu yake nje ya nchi.

Gharama za matibabu

Spika Ndugai aliliambia bunge kuwa si kweli kuwa chombo hicho kimtelekeza Lissu.

Ndugai alidai dai kuwa hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu yake na wabunge wenziwe na kufanya jumla kuu ya fedha alizolipwa kuw Sh250milioni.

Hata hivyo, Lissu alimjibu Ndugai na kunukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema bunge la Tanzania halijawahi kutoa hata senti moja kugharamia matibabu yake.

Lissu amekiri kulipwa Sh43 milioni zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao na kwamba kiasi kingine alicholipwa kinachofanya jumla ya fedha hizo kufikia Sh250 ni mishahara na stahiki zake, lakini siyo gharama za matibabu.

Huwezi kusikiliza tena
Tundu Lissu: Kushambuliwa kwangu kulichochewa na siasa Tanzania

Uchunguzi wa polisi

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi aliingia kwenye majibizano na Lissu baada ya mbunge huyo kutoa matamko yake nchini humo, kwa kumtaka Lissu kurejea Tanzania kutoa ushirikiano na polisi.

Dk Possi alisema Serikali inafuatilia suala hilo ndiyo maana Rais John Magufuli alishatoa tamko kulaani tukio hilo na kutuma baadhi ya viongozi kumjulia hali jijini Nairobi na hata ughaibuni alipo kwa sasa.

"Rais alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kuagiza uchunguzi wa kina wa haraka. Kwa nyakati tofauti Rais amemtuma makamu wake, Rais mstaafu na viongozi wengine wa Serikali kumtembelea Lissu akiwa hospitali akiwa Dodoma, Nairobi na Brussels," alisema Dk Possi katika tamko lake.

Aliongeza kuwa uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya kutokea tukio hilo lakini umeshindwa kuendelea kwa sababu ya kutopata ushirikiano kutoka kwa mbunge huyo.

Lissu aliiambia BBC na DW kuwa atarejea Tanzania pale tu madaktari wake watakapomruhusu na kudai serikali ya Magufuli itawajibika kumhakikishia ulinzi wake.

Akimjibu balozi Possi Lissu amesisitiza kuwa hakuna uchunguzi uliofanyika wa kushambuliwa kwake.

Kuhusu kutoa ushirikiano kwa polisi amesema sheria za Tanzania zinaruhusu kuomba msaada wa kupatikana kwa ushahidi iwapo mtuhumia yupo nje ya nchi, na kudai serikali ya Tanzania haijawahi kuwasiliana na serikali ya Kenya na ya Ubelgiji ili kupatiwa msaada wa kuhojiwa yeye na dereva wake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii