Bob Collymore: Ipi siri ya ufanisi kwa mtendaji mkuu wa Safaricom?

BOB COLLYMORE
Maelezo ya picha,

'Nina nidhamu, sikwamilii katika makosa yaliopita badala yake, najifunza kutoka kwayo na nasogea mbele' Bob Collymore afisa mkuu mtendaji wa Safaricom Kenya.

"Bob Collymore" na "Pumzika kwa amani" ni maneno ambayo yanatumika pakubwa katika mitandao ya kijamii leo nchini Kenya kama Twitter wakati raia wakipokea taarifa za kuaga dunia kwa mkurugenzi mkuu mtendaji wa kampuni ya mawasilano Safaricom.

Collymore amefariki leo Julai mosi nyumbani kwake akiwa na miaka 61 baada ya kuugua saratani ya damu.

Wakubwa kwa wadogo wakituma risala zao za rambirambi na baadhi hata kuonyesha picha na ujumbe wa kumkumbuka Collymore kwa mchango wake nchini.

Collymore ni nani?

 • Bob Collymore au Robert Bob Collymore alizaliwa mnamo Januari 13 Januari 1958.
 • Yeye ni Raia wa Uingereza aliyezaliwa Guyana, Amerika kusini.
 • Alilelewa na bibi yake huko Guyana.
 • Akiwa na umri wa miaka 16 alielekea Uingereza kuishi na mamake.
 • Alisoma shule ya upili huko na kupata kibarua chake cha kwanza akiwa na umri wa miaka 16.
 • Alipenda sana muziki na kusafiri kwa ndege.
 • Tangu miaka ya 90 Collymore aliwahi kufanya kazi katika kampuni tofuati na katika nyadhifa mbalimbali kwenye sekta hiyo ya mawasiliano ya simu.
 • Alichukua usukani wa kampuni ya Safaricom mnamo Septemba 2010 baada ya kuondoka kwa mkurugenzi mtendaji Michael Joseph na ameshikilia wadhifa huo mpaka kufa kwake hii leo.
 • Mnamo 2012 alituzwa tuzo katika ofisi ya rais nchini Kenya ijulikanayo the Moran of the Burning Spear (MBS) katika kutambua mchango wake kwa taifa.
 • Mnamo Aprili 2016 Bob Collymore alipata mchumba nchini kenya na kufunga ndoa katika sherehe iliyohudhuriwa na nyota na wageni wa kiwango cha juu.
 • Desemba 2018, Rais Uhuru Kenyatta alimteua Collymore kuwa mwanachama wa boda ya malengo ya ya maendeleo nchini Kenya Vision 2030 kwa kipindi cha miaka mitatu.
 • Mnamo Mei mwaka huu, waziri wa afya Kenya Sicily Kariuki alimteua Collymore kuwa katika bodi ya kitaifa ya kupambana na saratani nchini.

Alitarajiwa kuondoka katika kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano ya simu mwakani - baada ya mkataba wake kuongezwa muda wa mwaka mmoja.

Hii ilidhamiriwa kutoa nafasi kulipiza muda ambao hakuwepo kazini alipokuwa amesafiri kwenda kupokea matibabu kwa saratani aliyokuwa akiugua.

Collymore alielekea Uingereza mnamo 2017 kwenda kutibiwa saratani ya damu au leukemia. Alirudi mwaka uliofuata 2018 Julai kuendelea na kuhudumu kama afisa mkuu mtendaji wa Safaricom wakati bado akipokea matibabu.

Mwezi uliopita hali yake ilizidi kuwa mbaya na alifariki nyumbani kwake leo Julai mosi.

Siri ya ufanisi wake?

'Nilianza kazi yangu ya kwanza ya 'kweli' nikiwa na miaka 16. Nilifanya kazi dukani nchini Uingereza na niliifurahia sana' amesema Bob Collymore kuhusu safari yake katika ajira.

Shinikizo kubwa anasema alililipata kutoka kwa mamake kuingia kwa mara ya kwanza katika kazi ya mawasiliano ya simu. Anasema mamake alimfunza mengi kuhusu umuhimu wa kuwa mvumilivu.

Alipokuwa kijana Collymore anasema alikuwa akipenda sana kuchora na mamake alikuwa akimsumbua kila mara akimwambia atafute 'kazi ya maana'.

Katika mahojiano na BBC, Collymore alieleza kuwa siri ni kwamba kampuni anayoisimamia iinawekeza katika nguvu kazi akiongeza kuwa makampuni yanahitaji "kuwapa watu maana na malengo".

Katika mahojiano mnamo 2012 na jarida la biashara 'How we made it in Africa' Collymore aliulizwa nini sababu ya ufanisi wake katika biashara/

Alijibu:

'Nina nidhamu, sikwamilii katika makosa yaliopita, badala yake najifunza kutoka kwayo na nasogea mbele.

Nafahamu pia kwamba kusoma hakwishi, na najifunza mara kwa mara kutoka watu walionizunguka. Naamini sana ushirkiano wa watu. Ufanisi wa mtu ni kutokana na kuwa na watu'.

Alipoulizwa ujumbe wake kwa vijana wanaoazimia kujitosakatika biashara na ujasiriamali, Collymore alisema:

'Kujibidiisha kazini na uwajibikaji kwa mambo yalio muhimu maishani. Ni lazima pia uwe na subira. Ufanisi ni safari ndefu na njia yake ina kukunguaa, maamuzi mabaya, utapata wa kukuvunja moyo na mara nyingine hata unaweza kufeli' ameeleza.

Collymore, ameiongoza kampuni ya Safaricom kupata ufanisi na faida ya mabilioni ya pesa na kujishindia sifa kimataifa kwa ubunifu wake.

Collymore amemuacha mjane Wambui Kamiru, na watoto wanne.