Tundu Lissu: Nitapoteza sifa kama nitakutwa na hatia na Mahakama au Sekretarieti ya maadili

Tundu Lissu anasema ana haki ya kugombea nafasi yeyote ya urais Haki miliki ya picha TUNDU LISSU

Aliyekuwa mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema licha ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kudai hakujaza fomu za mali na madeni za viongozi wa Umma bado ana sifa za kugombea nafasi yoyote ya uongozi.

Lissu aliyeko Ubelgiji kwa matibabu amenukuliwa na gazeti la Mwananchi ikiwa ni siku chache zimepita tangu alipopoteza sifa za kuwa mbunge.

"Ili upoteze sifa ya kugombea ubunge au urais sharti uwe na hatia, sasa mimi sijakutwa na hatia na mahakama au mahakama ya Sekretarieti ya maadili, Ndugai peke yake hawezi kunitia hatiani bila kunisikiliza."

"Kwa hiyo mimi naweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi iwe ubunge au urais. Kama wanataka nisigombee wanipeleke mahakamani au kwenye mahakama ya sekretarieti na wakiniuliza kwa nini sijajaza fomu nitawaambia nitawezaje kujaza nikiwa nje ya nchi," amesema Lissu

Amesema fomu hizo zinapaswa kujazwa na kuziwasilisha kwa njia ya mkono lakini zinapaswa kusainiwa na wakili wa Tanzania, "Sasa mimi niko hospitalini Ubelgiji, nawezaje kuzijaza, huku nampata wapi wakili, nawezaje kuzipeleka kwa mkono? Kwa hiyo walipaswa kuniuliza kwa nini sijajaza na si kuzungumza sijajaza bila kuwa na sababu."

Mvutano ulianzia wapi?

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alitaja sababu kuu mbili zilizomsukuma kuiandikia tume ya uchaguzi, mosi ni kutokana na Lissu kutokuhudhuria bungeni kwa muda mrefu na pili kutokuwasilisha fomu ya tamko la mali na madeni kwa sekretari ya maadili kwa mujibu wa sheria.

Lakini Lissu amezipinga hoja zote mbili, akisema hashangazwi na tamko la Spika Ndugai.

Tundu Lissu kufungua shauri kudai stahiki zake

Tundu Lissu atangaza siku ya kurudi Tanzania

"Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa," amesema Lissu na kuongeza, "Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge... kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu."

Japo inafahamika kuwa mwanasiasa huyo alilazimika kusafirishwa nje ya Tanzania awali nchini Kenya na kisha Ubelgiji kwa matibabu baada ya shambulizi dhidi yake, kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu kutokuwepo kwake bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Haki miliki ya picha BUNGE TANZANIA

Hivi karibuni akiwa yungali ughaibuni amezuru nchi za Marekani, Ujerumani na Uingereza, kote huko, amehojiwa na vyombo vya habari za kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu kuhusu hali ya haki za binaadamu Tanzania.

Hali hiyo iliibua hoja miongoni mwa wakosoaji wake kuwa tayari amepona na anastahili kurudi Tanzania.

Spika Ndugai mwezi Februari mwaka huu alikubali kufanyia kazi hoja ya kuzuia stahiki zake kama mshahara kwa madai hayo, na kusema kuwa hana taarifa rasmi juu ya alipo Lissu na hali yake ya kiafya, na amekuwa akimuona kwenye vyombo vya habari.

Na wakati akitoa taarifa juu ya kuvuliwa ubunge wake Spika Ndugai ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa bado hana taarifa rasmi ya alipo Lissu na anachokifanya kwa sasa huko alipo.

"Katiba yetu inasema, katika mazingira yote mawili (kutooneka bungeni bila taarifa rasmi, na kutowasilisha tamko la mali na madeni) ubunge wake unakoma na ataacha kiti chake, ndiyo lugha inayotumika na katiba…kwa hiyo unakuwa umejifuta mwenyewe ubunge, hujafukuzwa na mtu," amesema Spika Ndugai.

Mada zinazohusiana