Harry Maguire: Kitita cha pauni milioni 70 kumtoa Leicester City

Harry Maguire Haki miliki ya picha Getty Images

Manchester United imetuma maombi ya kumnasa beki wa Leicester Harry Maguire kwa dau la pauni milioni 70.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer ana mpango wa kumsajili Maguire ambaye anaelezwa kuwa na ubora ambao unatafutwa na kocha huyo.

Inaeleweka kuwa bodi ya Leicester imefahamishwa kuhusu nia ya Maguire na kuwa mchezaji huyo mwenye miaka 26, atakuwa radhi kupata nafasi hiyo ya kusonga kwenye hatua ambayo inatazamwa kuwa ya viwango vya juu.

Beki huyo wa England, ambaye pia aliwavutia mabingwa wa primia Manchester City, alitia saini mkataba wa miaka mitano mwaka jana mwezi Septemba na kocha Brendan Rodgers aliweka wazi mwishoni msimu kuwa anahisi Maguire anaweza akafanya vizuri zaidi kama atasalia kwenye klabu.

Neymar anataka kurudi Barcelona?

Wan-Bissaka ajiunga na Man Utd

Maguire ambaye kwa sasa yuko mapumzikoni, na Leicester imekuwa ikiweka dau kubwa ili aendelee kusalia King Power Stadium.

United tayari imewasajili wachezaji makinda Daniel James na Aaron Wan-Bissaka kutoka Swansea na Crystal Palace.Kumuongeza Maguire kutaifanya klabu hiyo kutumia pauni milioni 140.

Kwa muda mrefu United walikuwa na nia ya kumsajili Maguire lakini walijiondoa kwenye mchakato huo miezi 12 iliyopita kwa kuwa waliona kitita cha pauni milioni 70 ni fedha nyingi.