Uingereza yatoa msaada kwa sekta ya habari Tanzania bila masharti

Wanahabari wakiwa kazini Haki miliki ya picha Getty Images

Ubalozi wa Uingereza umeupigia chapuo uhuru wa habari Tanzania kutoa msaada bila masharti kwa vyombo vya habari nchini Tanzania.

Mwaka jana ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa waandishi wa habari duniani kote. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takribani waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari 99 waliuawa.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya waandishi wa habari 300 wapo kizuizini, na takribani 60 wanashikiliwa mateka.Mauaji, vifungo na kupotea vinazidi kuongezeka.

Takriban waandishi habari 95 waliuawa mwaka jana wakiwa kazini, kwa mujibu wa shirikisho la waandishi habari wa kimataifa (IFJ).

Mahakama yapinga sheria inayokandamiza vyombo vya habari Tanzania

Manung'uniko dhidi ya mswada wa mabadiliko ya sheria Tanzania

Idadi hiyo ipo juu zaidi ya ilivyoshuhudiwa 2017, lakini haipo juu sana kama viwango vilivyoshuhudiwa katika miaka ya nyuma wakati mzozo katika mataifa ya Iraq na Syria yalikuwa yakitokota.

Kiwango kikubwa cha vifo vya waandishi habari kilichowahi kunukuliwa ni waandishi 155 mnamo mwaka 2006.

Haki miliki ya picha Getty Images

Takwimu hizi zinajumuisha yoyote anayefanya kazi katika kiwango chochote katika shirika la habari.

Uhuru wa habari Tanzania

Nchini Tanzania changamoto za kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari bado ni lukuki.

Mwishoni mwa mwezi Machi, Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) ilitoa hukumu kuwa baadhi ya vipengele katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inakiuka uhuru wa kujieleza pia vinapingana na Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao Tanzania imeuridhia.

Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka 2017 na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wakilalamikia sheria hiyo kwa ukandamizaji wa uhuru wa habari.

Lakini, ni dhahiri kuwa itachukua muda na mapambano zaidi ya kisheria mpaka mabadiliko hayo yaliyopendekezwa na EACJ kufanyiwa kazi. Tayari serikali ya Tanzania imeweka wazi nia yake ya kukatia rufaa uamuzi huo katika mahakama hiyo ya EACJ.

Haki miliki ya picha Jamii Forum

Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), limetoa ripoti yake mpya mwezi Aprili ikionesha Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Tanzania iliporomoka hadi nafasi ya 118 kwa mwaka 2019 kutoka 93 mwaka 2018 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa tathmini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mambo yaliyochangia Tanzania kuporomoka kwa kiwango hicho ni, sheria za habari, tukio la kuvamiwa kwa Clouds Media Group mwaka 2017 na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari. Pia kutimuliwa nchini humo waandishi wawili wa Tume ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), Angela Quintal na Muthoki Mumo Novemba 2018 .

Tukio jingine lililotikisa sekta ya habari ni kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa kujitegemea, Azory Gwanda, zaidi ya siku 500 zilizopita.

Nini kinafanyika?

Serikali ya Uingereza imetangaza kuwekeza kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 7.8 ili kuboresha mazingira vyombo vya habari. Kupitia msaada huu , katika kipindi cha mwaka 2018/ 2019, zaidi ya wanahabari watanzania 250 wamepata mafunzo na kujengewa uwezo kwa ajili ya kuboresha taaluma ya waandishi wa habari na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Sarah Cooke anasema kuwa: ''Uingereza ina historia ndefu kuhusu vyombo vya habari mahiri na huru, ambavyo ni misingi ya demokrasia yetu. Vyombo vya habari vimeibua baadhi ya majadiliano magumu katika jamii yetu. Kwa kusaidia ukweli kujulikana, uhuru wa vyombo vya habari una nafasi muhimu kusaidia nchi kukua na kufanikiwa''.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii