Waziri Palamagamba Kabudi: 'Azory Gwanda alitoweka na kufariki'

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Tanzania Palamagambo Kabudi

Kutoweka kwa mwandishi mpekuzi nchini Tanzania Azory Gwanda hatimaye kumechukua mwelekeo mpya baada ya waziri wa maswala ya kigeni nchini humo kusema kwamba mwandishi huyo 'alitoweka na kufariki'.

Katika mahojiano na BBC katika kipindi cha FOCUS ON AFRICA mjini London waziri Palamagambo Kabudi alinukuliwa akisema kwamba visa vya watu kutoweka vimesababisha uchungu mwingi nchini humo.

''Wacha nikwambie unapozungumzia kuhusu kisa hicho, ni mojawapo ya visa ambavyo vimesababisha uchungu mwingi nchini Tanzania''.

Aliendelea: Katika eneo la Rufiji sio tu Azory Gwanda aliyetoweka na kufariki, nataka kukuhakikishia kwamba tunachukua kila hatua sio tu katika eneo la Rufiji bali pia maeneo mengine ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa watu wetu wako salama-sio tu waandishi , bali pia Polisi na raia wa kawaida.

Na baada ya mahojanio hayo wanaharakati wa haki za kibinadamu na raia walisambaza kanda ya video ya mahojiano hayo mitandaoni wakimtaka waziri huyo kuelezea familia ya mwandishi huyo ni wapi mwili wake ulipatikana.

Haki miliki ya picha HRW

Wakili maarufu nchini humo Fatma Karume maarufu Shangazi aliandika katika mtandao wake wa twitter: Mungu wangu Palamagamba amekiri katika BBC FOCUS ON AFRICA kwamba Azory alitoweka na kufariki. Je alijuaje kwamba amefariki?

Mwengine kwa jina Namdi aliandika: hakika hakuna likaalo gizani likadumu. Bila shaka sasa ni muda muafaka watuonyeshe kaburi lake

Hilda Newton naye aliandika: kabudi atuambie wamepeleka wapi maiti ya #AzoryGwanda lakini pia inawezekana hata alipo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa awali na kampuni ya magazeti ya mwananchi, mwanahabari huyo wa kujitegemea alitoweka tarehe 21 Novemba.

Bw Gwanda alikuwa anaishi na kuripoti kutoka mji mdogo uitwao Kibiti, ambao upo kilomita kama 130 hivi kusini mwa Dar es Salaam.

Bwana Gwanda ni mmoja wa waaandishi wa kwanza kabisa kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauwaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa mji huo.

Mauwaji hayo yalitia hofu kubwa mjini hapo.

Mke wake Anna Pinoni alisema watu wapatao wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walimchukua bwana Gwanda kutoka katikati ya mji huo, mahali ambapo hupendelea kukaa.

Anasema pia aliporudi nyumbani alikuta vitu vimezagaa, ishara kwamba inawezekana waliipekua nyumba yao.

Bw Azory aliwasiliana na ofisi za Mwananchi mara ya mwisho tarehe 20 Novemba kwa majukumu ya kikazi.

Anadaiwa kutekwa katika operesheni iliofanyika katika pwani ya wilaya ya Kibiti ambapo mauaji ya kiholela yalikuwa yakifanyika.

Mjadala kuhusu kutoweka kwa mwandishi huyo mpekuzi ulitanda kila sehemu nchini humo huku waziri wa habari wa Tanzania akiliambia bunge kwamba kesi yake ni hafifu kwa kuwa alipotea eneo ambalo mamia ya Watanzania walipotea.

"Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea, hawauliziwi hao ila mmoja huyo ndiyo dhahabu."

"Halafu inaulizwa Serikali ambayo imeshughulikia kwa kiasi kikubwa na maofisa wa Serikali wengi wamekufa pale, najua mnawalisha Wazungu na wafadhili matangopori, hatujakosa chochote acha tushushwe madaraja, sisi tunaheshimu uhuru wetu kwanza," alinukuliwa akisema.

Tayari muungano unaopigania umoja wa vyombo huru vya habari unaoshirikisha makundi 30 kote duniani umeutaka uatawala kuwajibika.

Serikali imedai kuchunguza kesi yake na za watu wengine waliotoweka lakini hakuna kilichoafikiwa hadi sasa.

Mada zinazohusiana