Azory Gwanda: Shinikizo dhidi ya serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi kuhusu 'kifo' cha mwandishi habari aliyetoweka

AZORY GWANDA Haki miliki ya picha AZORY/FACEBOOK

Wito umeendelea kutolewa kwa serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi kamili kuhusu hatma ya mwandishi habari Azory Gwanda baada ya waziri ya mambo ya nje nchini, Profesa Palamagamba Kabudi, kusema katika mahojiano na BBC kwamba 'sio Azory Gwanda pekee aliyetoweka na kufariki katika eneo la Rufiji'.

Raia nchini na nje ya Tanzania pamoja na wanaharakati wa kutetea haki, wamekuwa wakiuliza iwapo kauli ya waziri huyo ni thibitisho kwamba kweli Azory amefariki?

Kamati ya kuwalinda waandishi habari CPJ imeeleza kwamba tangu kutoweka kwa mwandishi huyo wa kujitegemea, serikali ya Tanzania haijatoa taarifa zaidi ya kuahidi kuchunguza mkasa wa kupotea kwake.

Gwanda alitoweka mnamo Novemba 21 2017, baada ya uchunguzi kuhusu mauaji ya kiholela na yasioeleweka na kupotea kwa watu katika pwani ya wilaya ya Kibiti.

"Kwa mwaka mmoja na nusu familia ya Azory Gwanda na vyombo vya habari Tanzania, wameiomba serikali kufafanua kilichomfika mpendwa na mfanyakazi mwenzao," amesema naibu mkurugenzi mtendaji wa CPJ Robert Mahoney kutoka New York. "Alafu ghafla, waziri wa mambo ya nje anataja, kama kwa kupitiliza, kwamba mwandishi huyo amefariki. Hili kwa jumla haliridhishi na linatia wasiwasi. Ni lazima serikali itoe taarifa nzima kwa umma kuhusu hatma ya Gwanda."

Kutoweka kwa mwandishi wa kujitegemea, Azory Gwanda ni mkasa ulioitikisa tasnia ya habari Tanzania tangu 2017.

Waziri wa Habari wa Tanzania nchini humo hivi karibuni aliliambia Bunge la nchi hiyo kuwa: "Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea, hawauliziwi hao ila mmoja huyo ndiyo dhahabu."

Kumekuwa na shinikizo kutoka kwa makundi ya haki za kibinaadamu, waandishi na mashirika ya habari ambayo yamekuwa yakitoa wito kwa mamlaka Tanzania kuipatia kipau mbele kesi ya Gwanda na kutoa majibu kuhusu hatma yake kupitia kampeni mbali mbali katika mitandao kama vile #WhereIsAzory na #MrudisheniAzory zikisambazwa pakubwa katika siku za nyuma kwenye mitandao ya kijamii.

Mwandishi huyo wa Tanzania alikuwa akiifanyia kazi kampuni ya Mwananchi wakati alipotekwa katika mazingira ya kutatanisha.

Alikuwa akiripoti kesi za mauaji ya kiholela katika eneo la kibiti katika mwezi uliopelekea kupotea kwake.

Serikali imedai kuchunguza kesi yake na za watu wengine waliotoweka lakini hakuna kilichoafikiwa hadi sasa.

Maswali yashamiri kuhusu Azory Gwanda:

Mjadala katika mitandao ya kijamii kuhusu kauli iliyotolewa sasa na waziri Palamagamba Kabudi imegusia maswali kama vile:

  • Kipi cha kuaminiwa?
  • Je ni vipi familia ya Gwanda itakavyoweza kupata ukweli na amani kuhusu kilichotokea?
  • Na kama Gwanda amefariki, nani aliyemuua na kaburi lake liko wapi?
Huwezi kusikiliza tena
Siku ya 100: Mwandishi Azory Gwanda yuko wapi?

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii