Wanafunzi wafikishwa mahakamani kwa kumkejeli rais Magufuli

Wanafunzi wa chuo kikuu wafikishwa mahakamani

Polisi wa upelelezi wa makosa ya mtandao, ameieleza mahakama ya Wilaya ya Ilala alivyowahoji wanafunzi watatu wa Chuo Kikuu cha Kampala (Kiu) waliokiri kusambaza mtandaoni picha za Rais wa Tanzania, John Magufuli ikimuonyesha amevaa hijab,gazeti la Mwananchi limeripoti.

Watuhumiwa hao Amenitha Konga (19), Mariam Tweve (20) na Agnes Gabriel (21) wanatetewa na wakili, Alphonce Nachipyangu.

Afisa Telesphory ambaye ni shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo alieleza mbele ya hakimu mkazi, Catherine Kihoja na wakili wa Serikali, Grace Lwila katika kesi ya jinai namba 65 ya mwaka 2016.

Kuwa majukumu yake ni kufanya doria mitandaoni na kuchambua data za kielektroniki.

Amedai kuwa Juni 13, 2016 akiwa ofisini kwake alipewa maelekezo kwenda katika chuo hicho na kuwa kuna mshtakiwa ametuma picha ya rais akiwa amevaa Hijab katika kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp la Human Resource Menagement.

"Tulikwenda hadi chuoni hapo tukaonana na mlezi wa wanafunzi, Herma Frank, tukamueleza tunawahitaji wanafunzi hao na alikiri kuwa wapo akatuitia," amesema shahidi huyo.

Amesema wanafunzi hao waliitwa na alifanya mahojiano na Amenitha aliyekiri kuifahamu picha hiyo na kwamba aliituma katika kundi hilo.

Amebainisha kuwa mwanafunzi huyo alipoulizwa alikoipata, alieleza kuwa ilitumwa katika kundi la mtandao la Empire na rafiki yake, Mariam.

Telesphory amesema Mariam alivyohojiwa alikoitoa picha hiyo alijibu kuwa aliipata katika kundi jingine la mtandao huo la Business Administration, na kwamba ilitumwa na Agnes.

Amesema pia walimhoji Agnes aliyekiri kuitambua picha hiyo na kueleza kuwa ilitumwa katika kundi la St Mary's Ulete lakini alishindwa kukumbuka nani aliituma.

Katika maelezo yake, Telesphory amedai baada ya kufanya mahojiano hayo walijaza hati za kushikilia mali ya kila mtuhumiwa kwa ajili ya kushikilia simu zao na kadi Herma akitia saini kama shahidi.

Katika kesi hiyo washtakiwa hao watatu na mwenzao, Anene Mwansasu (23) kwa pamoja wanadaiwa Juni 9, 2016 jijini Dar es Salaam walichapisha taarifa ya uongo kupitia mfumo wa kompyuta.

Walisambaza katika mitandao ya kijamii ya WhatsApp picha hizo zikimuonyesha Rais Magufuli akiwa amevaa vazi hilo linalovaliwa na wanawake wa dini ya Kiislamu.

Hakimu Kihoja ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 22 na 23, 2019 na kuutaka upande wa mashtaka kupeleka mashahidi wa kutosha ili kesi imalizike mapema.