Watanzania na Wakenya miongoni mwa waliouawa katika shambulio la Kismayo

Miongoni mwa waliouawa ametambuliwa mfanyabiasha maarufu wa Tanzania, Mahad A Nur Haki miliki ya picha Mahad A Nur /Tweeter
Image caption Miongoni mwa waliouawa ametambuliwa mfanyabiasha maarufu wa Tanzania, Mahad A Nur

Watanzania 3 na Wakenya 3 ni miongoni mwa watu wapatao 26 waliouawa katika shambulio linalodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Alshabab lililofanyika katika hoteli ya kifahari iliyopo kwenye mji wa mwambao wa Somalia wa Kismayo.

Watu 56 wameripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo la bomu la kujitoa muhanga amesema afisa wa ngazi ya juu wa jimbo la Kismayo katika mahojiano na shirika la habari la AFP.

Miongoni mwa waliouawa ni mfanyabiasha maarufu nchini Tanzania, Mahad A Nur.

Haki miliki ya picha Mahad A Nur /Twitter
Image caption Mahad A Nur

Taarifa ya kifo chake imepokelewa kwa masikitiko. katika Ukurasa wake wa Twitter Naibu waziri nchini Tanzania Faustine Ndugulile ameelezea maskitiko yake kufuatia kifo hicho na kusema Mahad Nur alikulia eneo la Kigamboni jijini Dar es salaam ambako aliishi na wazazi wake:

Utambulisho wa raia wengine wa Tanzania na Kenya bado haujafahamika.

Raia wengine wa kigeni waliouawa katika shambulio hilo ni pamoja na Wamarekani wawili, Muingereza mmoja na raia mmoja wa Canada, kulingana na rais wa Jimbo lililojitangazia uhuru wake la Jubaland Ahmed Mohamed Islam katika mkutano na waandishi wa habari.

''Raia wawili wa Uchina pia ni miongoni mwa waliojeruhiwa''

Majeruhi wamepelekwa katika hospitari mbali mbali huku wengine wakisafirishwa kwa ndege hadi nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi.

Makabiliano baina ya vikosi vya usalama na wanamgambo yalidumu kwa saa takriban 12 na kumalizika mapema asubuhi Jumamosi.

"Vikosi vya usalama kwa sasa vimedhibiti hali na gaidi wa mwisho amepigwa risasi na kuuawa ", amesema afisa wa usalama mjini Kismayo Mohamed Abdiweli.

Miili ya watu waliouawa imeondolewa kutoka kwenye hoteli hiyo huku msako ukiendelea kufuatia shambulio kubwa zaidi kuwahi kutokea mjini Kismayo kwa miaka kadhaa Kismayo kwa miaka kadhaa.

Walioshuhudia shambulio hilo wanasema washambuliaji walikuwa wanne, na kwamba mmoja wao alikuwa amevalia sare ya polisi wa Somalia.

Miongoni mwa watu waliouawa pia ni pamoja na mwandishi wa habari maarufu mwenye uraia wa Canada na Somalia Hodan Nalayeh na mumewe.

Walioshuhudia wanasema maafisa wa ngazi ya juu wa kisiasa akiwemo mgombea wa urais katika uchaguzi ujao katika jimbo la Jubaland pia aliuawa.

Hodan atakumbukwa kwa kazi yake katika kuwapa moyo vijana na kupigania amani na ujenzi upya wa nchi ya Somalia iliyokumbwa na vita.

Alianzisha Intergration TV -kipindi kilichopeperusha matangazo yake kwa lugha ya kiingereza kupitia mtandao ambapo alitangaza vipindi juu ya hadithi na taarifa kuhusu maisha nchini Somalia na wasomali wanaoishi nchi za kigeni.

Vyombo vya habari katika eneo hilo na muungano wa waandishi wa Somali unasema kuwa Nalayeh ,43, pamoja na mumewe ni miongoni mwa wale waliouawa.

Baada ya shambulio hilo wakazi wa mji wa Kismayo wameshuhudia uharibifu mkubwa, huku majengo ya hoteli ya Hoteli ya Asasey , magari na na majengo mengine vikiharibiwa vibaya.

Unaweza pia kutazama:

Huwezi kusikiliza tena
Huenda juhudi za Kenya zinachangia ugaidi

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii