al-Shabab Somalia: Kwanini wanamgambo huzilenga hoteli katika mashambulio ya kigaidi?

al shabaab Haki miliki ya picha Getty Images

Kundi la wapigajani jihadi nchini Somalia al-Shabab limekiri kuhusika na shambulio lililotokea mwishoni mwa juma katika hoteli moja kwenye mji wa bandari Kismayo Somalia.

Mtandao ulio na mafungamano na kundi hilo la al-Shabab- Shahada na Somali Memo, linalounga mkono kundi hilo - zimedai takriban watu 40 wakiwemo raia wa kigeni waliuawa.

Kwa mujibu wa maafisa nchini Somalia, takriban watu 26 walifariki katika shambulio hilo la wanamgambo. Mwanasiasa maarufu katika eneo hilo ameeleza kuwa wakenya watatu, raia wawili wa Marekani na Muingereza mmoja ni miongoni mwa waliofariki.

Shambulio hilo linaonekana kama jitihada za kutatiza uchaguzi wenye ushindani mkubwa wa katikaeneo la Jubbaland, unaotarajiwa kufanyika Agosti.

Lakini inadhihirisha hamu inayokuwa ya al-Shabab katika kushambulia hoteli, huku kundi hilo lenye mafungamano na al-Qaeda likionekana kuzidi kutoa ufafanuzi wa kidini na kimaadili wa kwanini wanatekeleza mashambulio hayo.

Image caption Wanamgambo wa Alshaabab wanasemekana kugonga gari lililokuwa limesheheni vilipuzi

Nini kilichotokea?

Mwishoni mwa Juma, mlipuaji wa kujitoa muhanga alililivurumiza gari lililokuwa na vilipuzi ndani ya hoteli ya Asasey huko Kismayo, kabla ya washambuliaji waliojihami kwa bunduki kulivamia jengo hilo na kuwafyetulia risasi wageni waliokuwepo.

"Shirika la habari" la Shahada lilidai kuwa wanamgambo wa al-Shabab walikuwa wameidhinisha "operesheni ya jihadi" kwa kuilenga hoteli, wakituhumu kuwa jengo hilo ni makaazi ya wanasiasa wa Kisomali, mawaziri, maafisa wa ujasusi pamoja na wageni.

Kituo hicho pia kilidai kwamba wanamgambo wa al-Shabab waliidhibiti hoteli hiyo kwa zaidi ya saa 16, na kutuhumu kwamba walifanikiwa kuzuia jitihada za vikosi vya serikali kuingia ndani ya jengo hilo.

Kwa mujibu wa Shahada, zaidi ya watu 40 waliuawa na baadhi ya manusura inaarifiwa ni raia kutoka Kenya, Tanzania, Marekani, Uingereza, Canada na China.

Hatahivyo maafisa wa serikali wametaja idadi ndogo ya waliofariki na kufafanua kuwa wageni waliouawa ni Wakenya watatu, Watanzania watatu raia mmoja wa Uingereza na mmoja kutoka Canada.

Upi umuhimu wa shambulio hili?

Inaarifiwa kwamba hoteli hiyo ni mojawapo ya inayolindwa pakubwa Kismayo. Ni shambulio la kwanza pia la kiwango cha juu la al-Shabab kuilenga hoteli katika mji huo.

Wanamgambo walitumia mbinu wanayoitumia kawaida wakati wa kushambulia hoteli katika mji mkuu Mogadishu ambapo mlipuaji wa kujitoa muhanga hujilipua katika lango kuu la kuingia katika hoteli na baada ya hapo washambuliaji waliojihami kwa bunduki wanalivamia jengo.

Mbinu kama hiyo ilitumika katika hoteli ya Dusit katika mji mkuu wa Kenya Nairobi mwaka huu.

Mara ya mwisho al-Shabab lilitekeleza shambulio kubwa la kujitoa muhanga huko Kismayo ilikuwa ni Agosti mnamo 2015 wakati mlipuaji wa kujitoa muhanga alilivurumiza gari lenye milipuko ndani ya kambi ya mafunzo ya jeshi mjni humo na kuwauwa wanajeshi kadhaa.

Shambulio hili linatokea pia wiki kadhaa kabla ya uchaguzi wenye ushindani mkubwa wa Jubbaland.

Wapiganaji jihadi kwa jumla hushutumu siasa za kisasa na mifumo ya kidemokrasia kama uchaguzi, na kuyataja kwenda kinyume na uislamu.

Image caption Hasara iliyosababishwa na shambulio katika mji wa Kismayo nchini Somalia

al-Shabab inajitetea vipi kwa mashambulio dhidi ya hoteli?

Al-Shabab bado halijatoa taarifa kamili kueleza ni kwanini limetekeleza shambulio hilo Kismayo.

Hatahivyo katika nyakati za nyuma, kundi hilo lilitetea vikali kulenga hoteli likidai kuwa zilitumika na maafisa wa serikali na wanasiasa, na ndio sababu ya kuzilenga.

Katika taarifa za hivi karibuni, kundi hilo la wanamgambo limekana kuwalenga raia na kudai kuwa linajihadhari katika kuepuka vifo visivyostahili kutokea.

Mnamo Machi kwa mfano, msemaji wa al-Shabab Ali Mahmud Raage (ajulikana pia kama Ali Dheere), alitaja baadhi ya hoteli kuwa "kambi za kijeshi na makao makuu ya waasi".

Katika mwezi uo huo, kundi hilo lilitoa taarifa likifafanua kwanini wanamgambo wake walivamia hoteli ya kifahari mjini Mogadishu mnamo Februari 28.

Taarifa hiyo ilidai maafisa wa juu wa serikali walifika katika hoteli hiyo mara kwa mara na kwamba raia wa kawaida "hawakuweza kuingia" ndani.

Mnamo Mei, naibu kiongozi wa al-Shabab, Abu Abdul-Rahman Mahad Warsame (Karate), alidai "muongozo" wa kundi hilo ulimuamuru 'kutahadhari pakubwa' kuhakikisha hakuna umwagikaji damu wa raia wa kiislamu unaotokea.

Kiongozi huyo wa jihadi alitoa wito kwa umma kuepuka "makao makuu ya maadui" na maeneo yanayozunguka sehemu hizo.

Haki miliki ya picha Somalia

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii