ATCL: Shirika la ndege Tanzania leo kuidhinisha safari za kwenda Mumbai India

Ndege ya Dreamliner ilipowasili Tanzania Julai 2018 Haki miliki ya picha IKULU TANZANIA
Image caption Ndege ya Dreamliner ilipowasili Tanzania Julai 2018

Shirika la ndege nchini- Air Tanzania leo linaidhinisha njia mpya ya usafiri - kwenda Mumbai nchini India, jambo linalotazamwa kuwa fursa ya ukuwaji linapokuja sula la usafiri wa abiria.

Rais John Pombe Magufuli aliahidi kwamba shirika hilo litaimarishwa na ndege mpya kununuliwa mara baada ya kuingia madarakani.

Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Zambia, Zimbabwe, Nigeria na Uganda, imelifufua shirika lake la ndege, ama kama lijulikanavyo, Air Tanzania.

Uwekezaji mkubwa umefanywa mpaka sasa katika kulifanikisha hilo.

"Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya sana, lilikuwa na ndege moja tu tena ilikuwa inafanyiwa matengenezo mara kwa mara, soko la ATCL lilishuka sana hadi kufikia asilimia 2.5.

Lakini sasa tumenunua ndege 7, na nyingine kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner itakuja mwaka 2020", alisema Rais Magufuli mwaka jana 2018 katika hafla ya kuipokea ndege mpya ya Tanzania.

Haki miliki ya picha IKULU
Image caption Rais Magufuli akiwa ndani ya Air Tanzania mnamo 2018

Mambo yako vipi kwa Air Tanzania hii leo?

Mkurugenzi mtendaji wa Air Tanzania Ladislaus Matindi anasema shirika la ndege linapanuka, lakini sio hilo tu ila pia linadhihirisha namna shirika hilo lilivyopiga hatua katika suala la hisa katika soko.

Wakati Air Tanzania likianza, Matindi anaeleza kwamba lilikuwa linadhibiti 2% pekee ya hisa hiyo ya soko.

Precision na Fast Jet zikishikilia sehemu kubwa ya soko wakati huo. Kufikia sasa mkurugenzi huyo mtendaji anasema shirika hilo limesogeza udhibiti kwa zaidi ya 75%.

Akizungumza na BBC, Matindi ameeleza kwamba ufanisi huo umetokana na namna washindani wao walivyokuwa wakihudumu.

Kampuni ya ndege ya Precision ilitumia ndege ndogo na kusafiri katika maeneo machache, Fast jet ambayo haipo sokoni kwa sasa, anasema mbinu waliokuwa wakitumia ya safari za gharama ndogo ni ngumu kuimudu katika mataifa ya Afrika.

Haki miliki ya picha AFP

Licha ya kwamba ni mbinu inayoonekana kulifaa soko la maeneo masikini, Matindi anafafanua kuwa kiwango cha watu wanaosafiri kutoka maeneo hayo haizidi 2% ya wanaosafiri kwa ndege.

Ili kupata ufanisi wa mbinu hiyo, 'ni lazima uwe na idadi kubwa ya wateja, ili ndege ijaye saa zote, na kuwe na mzunguko mkubwa wa safari hizo' anasema.

Anaeleza kwamba taswira nchini Tanzania ni kwamba idadi kubwa ya watu wako radhi kusafiri safari ndefu kwa basi, kwasababu hawawezi kumudu gharama za tiketi ya ndege.

Hatahivyo anatazama nafasi kwa shirika la ndege la Air Tanzania kutokana na kwamba idadi ya watu walio na kipato cha wastani inaongezeka nchini, na hilo anasema ni fursa kubwa kwa shirika hilo.

Hususan katika msimu kama huu wa sasa kunakoshuhudiwa wasafari wengi, hiyo inamaanisha kwamba shirika linafanikiwa kuuza tiketi za viti vyote katika ndege zinazosafiri za shirika hilo.

Air Tanzania ina ndege ngapi?

Shirika la Air Tanzania lina ndege saba, baada ya kununuliwa ndege sita chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.

Kuna Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Juni 2017; Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua Tanzania kati ya mei na Julai 2018.

Shirika hilo lilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011.

Air Tanzania inamilikiwa asilimia mia moja na serikali kama ilivyo kwa mashirika ya ndege kama Ethiopia.

Kama mashirika mengine ya ndege katika bara la Afrika yalioshindwa kupata ufanisi, Air Tanzania kadhalika iliathirika kutokana baadhi ya mengine, shinikizo la soko.

Afisa mkuu mtendaji wa Air Tanzania anaeleza kuwa kipindi hicho kigumu kilitokana na utovu wa nidhamu ya biashara, akitaja mfano wa wakati ndege ikiwa angani, waziri aliyetarajiwa kuabiri ndege hiyo akachelewa, ndege inalazimishwa kurudi.

Anasema ni jambo lililokuwa likifanyika na sio tu kwa Air Tanzania, kwahivyo anaeleza kwamba kuna suala la ushindani na nidhamu kwa soko.

'Fedha zilizokuwa zikiundwa, zilikuwa ni za watu binafsi katika kampuni hiyo na sio shirika la ndege'.

Haki miliki ya picha IKULU TANZANIA

Matindi anasema wakati wakiidhinisha kufufuliwa kwa ndege hiyo, katika mapato yanayotokana na usafirishaji mizigo, kipato kilikwea kwa kasi kutoka milioni mbili hadi milioni mia mbili kwa mwezi.

Jambo ambalo anasema linadhihirisha kuwa yote ni kutokana na nidhamu ya biashara ambayo haikuwepo katika siku za nyuma.

Ametaja mifano ya mashirika ya ndege yaliojaribu kufufuka kama Air Africa ilivyosambaratika, Air Tanzania ilivyoingia katika matatizo na hata Uganda Air, na kila mtu akiwa anajaribu kufufua mashirika hayo ya ndege pasi kutambua tatizo halisi ni lipi.

Kimsingi Matindi anasema siri ya Air Tanzania sasa, ni kukumbatia nidhamu ya biashara na kutambua kwamba mapato ya fedha ni ya shirika hilo la ndege.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii