Mtembo: Mti wa miaka 80 huko Mwika Kilimanjaro Tanzania uliosuluhisha migogoro

Mti wa usuluhishi una miaka 80 na unapatikana huko Mwika Kilimanjaro Kaskazini Tanzania
Image caption Mti wa usuluhishi una miaka 80 na unapatikana huko Mwika Kilimanjaro Kaskazini Tanzania

Ni kawaida kabisa watu kufikishana mbele ya vyombo vya dola na sharia pale tu kunapotokea msuguano au ugomvi hata na madhila na kutatuliwa kwa mujibu wa katiba na sharia za mataifa mbalimbali kote Ulimwenguni.

Lakini kwa jamii ya eneo la Mwika Mkoani Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania, hali huwa ni tofauti kwani pale wanapohitilafiana, na hata kugombana basi wao hupelekwa kusuluhishwa katika mti mkubwa wenye miaka zaidi ya 80.

Mti huo unaaminika kuwa ukifika hapo, basi tofauti zimekwisha.

Je usuluhishi hufanyika vipi hasa?

Katika eneo la Mwika katika kijiji cha tema ukanda wa moshi vijijini katika Mkoa wa Kilimanjaro unaopatikana kaskazini Mwa Tanzania.

Kuna mti ambao husuluhisha migogoro ya watu wa eneo hili.

Mti huo wameupa jina la Mtembo ambalo limetokana na ukubwa wake, mithili ya mnyama Tembo.

Na eneo linakopatikana mti huo linaitwa Kiunguni.

Kwa kuutazama mti huo, una ukubwa wa zaidi ya nyumba 3 za kisasa.

Ni wakati wa masika na mti huo wa Mtembo umechanua.

Wenyeji wanasema wakati wa kiangazi, mti huu hupukutika na ni marufuku tawi lolote kukatwa aidha kwa panga, shoka ama kitu chochote chenye makali.

Na kama tawi likivunjika basi tambiko hufanyika kwa kuchinjwa mbuzi.

Frank Gibson, ambaye zaidi ya miaka 25 iliyopita, alifikishwa katika mti huo kusuhulishwa alipogombana na mwenzake.

'Nililetewa hapa kwa kugombana, niliyegombana naye nikamshtaki kwa babake wakaamua tuje tuzungumzie hapa mtemboni kwa Wazee.

'Ukifanya kosa unalatewa hapa kama ni viboko unakuja kupigiwa hapa hapa' ameeleza Gibson.

'Unasuluhishwa, mnapatana hapa hapa, munasameheana kama ni kusameheane, kama ni faini unapigwa papa hapa' ameongeza.

Historia ya Mtembo ni ipi?

James Kashingo, ni mzee wa makamo, sasa ana miaka 86 anasema tangu utotoni mwake amekuwa akiuona mti huo kama ulivyo.

'Ukianguka tawi lake lazima wazee watafute mbuzi wachinjie hapa'.

'Ni mahali ambapo wazee walikuwa wanakutana kufanya mashauriano, labda mtu amegombana na ndugu yake wanakuja kufanya mashauri pale na kuamua'.

Huwezi kusikiliza tena
Majani yanavyotumiwa kuomba msamaha miongoni wa Wachagga

Je mti huo unatumika mpaka leo? Wilbard Mshanga ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa huu.

Anaeleza kuwa kesi kama za kupigana , ugomvi au uhalifu mdogo kama wizi wa ndizi shambani na kadhalika huwasilishwa mtemboni.

'Tunafuata sheria za serikali tukiongea ikishindikana nachukua waraka tulioandika naenda polisi'.

Vijana wadogo hasa waliozaliwa miaka ya 90 wanasema kua wamekua tu wakisikia historia ya mti huu, huku wengi wao wakiogofya kupita katika eneo hilo nyakati za usiku.

Wanasema watangulizi wao hasa babu na bibi zao huwaambia kuwa eneo hilo usiku mbuzi na kondoo hulia na hata wachawi waliaguliwa hapo.

Lakini wenyeji wanaoishi karibu kabisa na eneo hilo wanasema maisha ni shwari kwao na hawana hofu yeyote.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii