Sudan Kusini: Ni marufuku kuimba wimbo wa taifa bila uwepo wa rais Salva Kiir

Salva Kiir Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, amepiga marufuku mtu yeyote kuimba wimbo wa taifa bila uwepo wake, amesema waziri wa habari Michael Makuei ambaye pia ni msemaji wa serikali.

Bw. Makuei ameliambia shirika la Habari la AFP kuwa viongoz tofauti na wa kuu wa taasisi za umma wamekuwa wakiimbiwa wimbo wa taifa bila sababu zozote za msingi na kuongeza kuwa hatua hiyo ni ya kutumia vibaya wimbo huo ambao ulitungwa muda mfupi baada ya taifa hilo kupata uhuru wake mwaka 2011.

"Kwa taarifa ya kila mmoja wimbo wa taifa ni wa Rais peke yake, na utaibwa tu katika hafla inayohudhuriwa na rais, sio ya kila mtu," Makuei alisema.

"Tumeshuhudia wimbo wa taifa ukipigwa katika hafla zinazohudhuriwa na waziri, makatibu wakuu na hata magavana wa majimbo."

Ameongeza kuwa amri hiyo imetolewa na rais wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri siku chache zilizopita.

Makuei pia amefafanua kuwa wimbo wa taifa utapigwa katika ubalozi ya Sudan Kusini nje ya nchi kwa niaba ya rais na shuleni ambako watoto wanafunzwa kuimba wimbo huo bila uwepo wa Bw. Kiir.

Haijabainika ni adhabu gani itatolewa kwa yeyote atakaye kiuka amri hiyo ya rais.

"Hii ni amri ya rais na bila shaka ukiivunja utabeba msalaba wako mwenyewe," Makuei alisema.

Haijabainika kwa nini Kiir ameamua kuubinafsisha wimbo wa taifa kwasababu wimbo huo ni nembo ya taifa inayowaleta watu pamoja.

Amri nyingine iliyotolewa na rais Kiir, inalenga viongozi wa kijeshi ambao sasa wamepigwa marufuku kuhutubia mukutano wa hadhara wakiwa wamevalia sare zao za kazi.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudankufuatia kura ya maoni na Bw Kiir amekuwa akiliongoza taifa hilo tangu wakati huo.

Hatua ya hii inajiri wakati ambapo rais huyo amekubali kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi wa upinzani Riek Machar, katika kile kinachoonikana kuwa hatua ya kufufua upya mazungumzo ya amani ambayo yalikwama na kusababisha vurugu katika taifa hilo.

Haki miliki ya picha AFP

Katika barua iliyowasilishwa hivi karibuni na mshauri wa rais, Tut Gatluak, Bw Machar amesema yuko tayari kukutana na ra alimradi atakuwa huru kuzuru Sudan Kusini.

Utawala wa Bwana Kiir umemualika Machar baada ya serikali na makundi ya upinzani kushindwa kufikia muda wa mwisho wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ambao ulikuwa mwezi Mei.

Muda huo sasa umesongezwa mbele kwa miezi sita zaidi.

Muda mfupi baada ya pande zote mbili kukubaliana kusongeza mbele muda wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, utawala wa Rais Kiir uliahidi dola milioni 100 kufadhili miradi itakayosaidia kuimarishwa kwa serikali ijayo ikiwa ni pamoja na mipango ya usalama, japo haijabainika ikiwa serikali imetoa fedha hizo au la.

Machar kwa upande wake alimuomba Bw. Kiir "kuwasilisha ombi maalum" kwa baraza la jeshi mjini Khartoum, ambako anasema amewekwa kwenye kifungo cha nyumbani kuwa anaomba Mamlaka ya nchi hiyo kumsafirisha hdi Juba na kumrudisha Khartoum baada ya mazungumzo hayo.

Katibu uhusiano wa kimataifa wa chama SPLM-katika upinzani Stephen Par Kuol, amesma kuwa, Machar anatakiwa kuwa huru kwenda popote atakapowasili mjini nchini Sudan Kusini

"Tumekuwa tukishinikiza mwenyekiti wetu awachiliwe huru ili aweze kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa utekelezaji wa mkataba wa amani ," Kuol alikiambia chombo kimoja cha habari nchini Sudan Kusini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii