Henry Rotich: Waziri wa fedha Kenya aachiliwa kwa dhamana baada ya kukana mashtaka yanayohusiana na ufisadi

Henry Rotich aachiliwa kwa dhamana Haki miliki ya picha SIMON MAINA
Image caption Henry Rotich aachiliwa kwa dhamana

Waziri wa Fedha Kenya, Henry Rotich ameachiliwa huru kwa dhamana ya $150,000 baada ya kukana zaidi ya mashtaka 10 yanayohusiana na ufisadi.

Rotich, na mshtakiwa mwenzake katibu mkuu Kamau Thugge wameagizwa kuwasilisha pasipoti zao za usafiri kama sehemu ya masharti ya dhamana.

Hakimu Douglas Ogoti amewazuia wasifike katika makao ya wizara ya fedha, na kufafanua kwamba sasa eneo hilo linachunguzwa kwa uhalifu.

Mapema leo, Rotich amekanusha mashtaka ya ufisadi dhidi yake kuhusiana na kandarasi ya ujenzi wa mabwawa mawili siku moja tu baada ya kukamatwa na kuzuiliwa - hatua isio ya kawaida kwa waziri katika taifa hilo lenye kiwango cha juu cha ufisadi.

Waziri huyo na maafisa wengine wakuu wanatuhumiwa kwa ushirikiano kuwalaghai Wakenya , miongoni mwa mashtaka mengine.

Akiwa amevalia koti na tai na kusimama karibu na naibu wake katika wizara hiyo , Kamau Thugge, Rotich alikana mashtaka hayo wakati yalipokuwa yakisomwa na waendesha mashtaka katika chumba cha mahakama kilichojaa watu mjini Nairobi.

Mashtaka dhidi ya Rotich yanatokana na uchunguzi wa polisi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika miradi miwili ya mabwawa magharibi mwa taifa hilo ambayo yalikuwa yakisimamiwa na kampuni moja ya Italia kwa Jina CMC Di Ravenna.

Kenya pia itaomba kurudishwa nchini kwa Paolo Porcelli, mkurugenzi wa kampuni ya CMC di Ravenna, ili kushtakiwa, nchini mkurugenzi wa mashtaka aliambia chombo cha habari cha Reuters.

''Kuna huyu raia wa Itali, hakuweza kufikishwa mahakamani hivyobasi tutaomba ahukumiwe hapa nchini , Tutahakikisha kuwa kibali cha kimataifa cha kukamatwa kwake kimetolewa'', alisema Noordin Haji.

CMC di Ravenna amekana kufanya makosa. Katika taarifa siku ya Jumatatu, kampuni hiyo ilisema siku ya Jumatatu kwamba haijaelezewa kuhusu mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa mamlaka .

Mabwawa hayo mawili yalipangiwa kugharimu dola bilioni 46 lakini wizara ya fedha ilikopesha bilioni 63 badala yake , alisema Hajj siku ya Jumatatu hivyobasi kuongeza deni kubwa la Kenya ambalo linadaiwa kufikia asilimia 55 ya mapato ya taifa hilo.

Na huku hayo yakijiri mkurugenzi wa zamani wa shirika la kukabiliana na ufisadi nchini kenya John Githongo amesema kuwa raia nchini wana 'matumaini' baada ya waziri wa fedha Henry Rotich kukamatwa pamoja na viongozi wengine wakuu kuhusiana na mashtaka ya ufisadi.

Bwana Githongo aliambia kipindi cha BBC News Day kwamba ni mara ya kwanza kwa taifa hili ambapo waziri na katibu wake wamekamatwa na kuwasilishwa mahakamani.

Akielezea umuhimu wa kukamatwa kwake bwana Githongo amesema kuwa ni uwajibikaji ambao Wakenya hawajauzoea.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii