Kenya: Wanaume wasiotahiriwa watakiwa kujitokeza

Mkono Sweta

Serikali ya Kenya imeanza mpango wa kuwarai Wakenya ambao hawajatahiriwa kujitokeza kwa hiari.

Kulingana na gazeti la Taifa Leo nchini Kenya, Wizara ya Afya imesema uchunguzi huo unaoendeshwa na Shirika la Wanaume Kutahiri kwa Hiari (VMMC) unalenga kuimarisha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa hatari wa Ukimwi katika kaunti hizo.

Mpango huo ulioanza tarehe 22 mwezi Julai unalenga kuchunguza nyeti za wanaume iwapo wamepitia kisu cha ngariba katika kaunti nne za eneo la Nyanza.

Uchunguzi huo pia unalenga kufahamu idadi ya wanaume waliotahiriwa katika kaunti za Homa Bay, Kisumu, Siaya na Migori baada ya kuzinduliwa mjini Homa Bay siku ya Jumapili kwenye hafla iliyohudhuriwa na Afisa Mkuu wa Afya Gerald Akeche na Mkurugenzi wa idara hiyo Gordon Okomo Jumapili.

Kulingana na gazeti la taifa leo, uchunguzi huo wa miezi mitatu, utawapatia fursa wahudumu waliopokezwa mafunzo kukagua kibinafsi uume wa mwanaume iwapo anayechunguzwa atakubali na akikataa atajibu tu swali iwapo amepitia kisu cha ngariba au la.

Hata hivyo, mila na desturi za jamii huenda zikazuia baadhi ya wanaume kuhojiwa kuhusu iwapo wametahiriwa au la.

"Iwapo mwanamume atakataa tukitazama uume wake, maafisa wetu hawatamlazimisha lakini watakumbatia tu jibu lake," akasema Dkt Akeche.

Huduma za VMMC zilianza kutolewa katika eneo la Nyanza mwaka wa 2008 kabla ya kuenea hadi maeneo mengine ya nchi.

Lengo lake, kulingana na gazeti la taifa leo, ni kusaidia kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Ukimwi katika Kaunti za Nyanza ambazo zimekuwa zikisajili zaidi ya asilimia 20 ya maambukizi.

Utafiti unaonyesha tohara hupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa asilimia 60.

Kulingana na Dkt Akeche, utafiti wa kuchunguza nyeti za wanaume Nyanza umefadhiliwa na serikali ya Marekani pamoja na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa(CDC) na utasaidia kuamua iwapo rasilimali zaidi zitawekezwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi maeneo hayo.

"Wakati VMMC ilipoanzisha mpango wa tohara, idadi ya maambukizi ya HIV yalianza kupungua pamoja na idadi ya wanaume waliofika kutahiriwa. Utafiti huu utasaidia kufahamu iwapo bado kuna wanaume ambao hawajatahiriwa," akaongeza huku akisema wanaume kati ya umri wa miaka 19 hadi 29 ndio wamekuwa wakifika kwenye kliniki zao kutahiriwa, Dkt Akeche aliambia Taifa Leo.

"Wanaume wenye umri wa juu ambao pia wapo hatarini kuambukizwa ukimwi wamekuwa wakikwepa tohara.

Hii itakuwa fursa ya kufahamu idadi yao na kuwashawishi kukumbatia kisu cha ngariba," akasema.

Dkt Okomo naye alisema matokeo ya uchunguzi huo yatasaidia kukadiria bajeti ya kufadhili vita dhidi ya kuenea kwa ukimwi eneo la Nyanza hasa kaunti ya Homa Bay ambayo inaongoza katika orodha ya maambukizi nchini Kenya kwa asilimia 26.

Mada zinazohusiana