Kinyang'anyiro: Ni mpambano baina ya Boris Johnson na Jeremy Hunt

Boris Johnson Haki miliki ya picha EPA
Image caption Boris Johnson anapigiwa chapuo kuchukua madaraka Uingereza

Ni aidha Boris Johnson ama Jeremy Hunt hii leo Jumanne atatangazwa kuwa kiongozi wa chama cha Conservative baaada ya kinyang'anyiro kikali cha kumrithi Bi Theresa May ambaye amejiuzulu.

Matokeo ya kura ya wananchama 160,000 wa chama hicho ambacho ni maarufu pia kwa jina la Tory yatawekwa wazi kabla ya mchana wa leo.

Mshindi wa kura hiyo, atakuwa Waziri Mkuu rasmi kesho Jumatano baada ya kukutana na Malkia.

Bw Johnson, ambaye ni Meya wa zamani wa jiji la London, anapigiwa upatu kushinda ijapokuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho wameshaonya kuwa hawatafanya naye kazi endapo atashinda.

Bi May, ambaye amejiuzulu baada ya kushindwa kuwashawishi wabunge wa chama chake juu ya sera zake za Brexit. Na asubuhi ya leo ataongoza kikao chake cha mwisho cha baraza la mawaziri.

Kujiuzulu kwake kutakuwa rasmi baada ya kukutana na Malkia mchana wa Jumatano baada ya kujibu maswali bungeni.

Mrithi wake baada ya hapo ataenda kujitambulisha kwa Malkia katika kasri la Buckingham na kuchukua hatamu za uongozi rasmi.

'Ushindi usio wa kawaida?'

Hisia za wazi ndani ya chama cha Conservative na Bunge la Westminster ni kuwa waziri mkuu mpya ni Boris Johnson - ama labda iwe walikuwa wanajidanganya katika wiki za hivi karibuni ndiyo matokeo yatakuwa ya tofauti.

Na laiti kama Johnson atashindwa, basi utakuwa ushindi usio wa kawaida kwa Hunt.

Itakuwa ni jambo la kustaajabisha kwa kushinda Hunt sababu Johnson kwa miaka kadhaa sasa, sarakasi zake na ajali alizozipata katika siasa zimemfanya aonekane kama ndiye mwenye ushawishi mkubwa zaidi kwenye chama hicho.

Wafuasi wake wanaweza sema kuwa amekuwa akijikuta katika hali ya kubeba mzigo wa lawama na kusafisha taswira ya chama.

Lakini wapinzani wake wanaweza sema amefikia ngazi za juu za uongozi katika namna zisizofaa na kuweka maslahi yake mbele badala ya nchi.

Wakati Bi May akiingia madarakani, wapo waliomng'ata sikio kwamba asigombee kwa kuwa ameshindwa kutumia nafasi zake hapo kabla na kuwa ndoto yake ya uwaziri mkuu haitatimia.

Lakini yawezekana kuwa usuli wake kama kiongozi kinara wa kura ya kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) ama maarufu kama Brexit kutamfanya aongoze vyema.

Waziri wa Brexit Dominic Raab ameiambia Sky News kuwa Bw Johnson yupo katika nafasi nzuri ya kushinda baada ya kuungwa mkono na zaidi ya 50% ya wabunge wa chama hicho.

Waziri wa masuala ya kijamii James Brokenshire ameiambia Channel 4 Newskuwa Johnson ndiye mtu sahihi wa kushughulika na Ulaya juu ya namna ya kujiondoa kwenye umoja huo na kulishawishi Bunge ambalo lilikataa mpango wa Bi May mara tatu.

Kampeni za nafasi hiyo zilitawaliwa na suala la Brexit na wagombea wote wakijinadi kuwa wapo katika nafasi nzuri ya kuliendea kuliko mwengine.

Uingereza inatakiwa kujitoa EU kufikia Oktoba 31 mwaka huu.

Johnson ameahidi kuwa atatekeleza hilo kwa muda uliopangwa, lakini Hunt amedai atahitaji muda zaidi ili kufanikisha hilo.

Mawaziri kadhaa, akiwemo wa Fedha Philip Hammond, Sheria David Gauke na Maendeleo ya Kimataifa Rory Stewart wametangaza wazi kutokubaliana na msimamo wa Johnson na kuwa watajiuzulu nyadhifa zao endapo atachaguliwa.

Haitakuwa jambo la kustaajabu iwapo baraza la mawaziri litaundwa upya baada ya mshindi kutawazwa.

Mada zinazohusiana