Wakenya wakerwa na maamuzi ya mahakama

Wakenya wanailaumu mahakama kwa kutounga mkono juhudi za kukabiliana na ufisadi
Image caption Wakenya wanailaumu mahakama kwa kutounga mkono juhudi za kukabiliana na ufisadi

Raia wa Kenya wameelezea malalamiko yao kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya utendaji wa mahakama kufuatia visa vya kuwakamata na baadae kuwaachiilia washukiwa.

Wakitumia #MkishikaTunawachilia, baadhi wanasema, hatua ya kuwaachilia huru washukiwa inaonyesha kuwa mahakama haisaidii katika vita dhidi ya ufisadi nchini humo.

Malalamiko haya yanakuja baada ya Waziri wa fedha chini Henry Rotich kuachiliwa kwa dhamana ya dola 150, baada ya kukana mashtaka 20.

Mshtaka dhidi ya Rotich yanatokana na uchunguzi wa polisi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika miradi miwili ya mabwawa magharibi mwa taifa hilo ambayo yalikuwa yakisimamiwa na kampuni moja ya Italia kwa Jina CMC Di Ravenna.

Mabwawa hayo mawili yalipangiwa kugharimu dola bilioni 46 lakini wizara ya fedha chini ya usimamizi wa bwana Rotich ilikopesha bilioni 63 badala yake , alisema Noordin Hajj siku ya Jumatatu hivyo basi kuongeza deni kubwa la Kenya ambalo linadaiwa kufikia asilimia 55 ya mapato ya taifa hilo.

Baadhi ya Wakenya wanaona kuwa licha ya juhudi zinazofanyika kukabiliana na ufisadi nchini mwao, mahakama hazionyeshi ushirikiano katika kuwashughulikia kisheria wahusika.

Mfano katika ukurasa wa Twitter, Ali kere anasema mahakama nchini Kenya ni tatizo katika kukabiliana na ufisadi:

Nae Eique Cnyua amewataja Noordin Hajj Mkurugenzi wa mashtaka ya umma na mkuu wa upelelezi wa Idara ya upepelezi wa makosa ya jinai George Kinot kama nembo ya matumumaini ya kumaliza ufisadi nchini, lakini akasema kuwa kazi yao huwa inakwamishwa na mahakama kwa usaidizi wa mafisadi tajiri.

Wengine hawakusita kutoa mifano ya awali ambapo mahakama ilipokea dhamana kwa washikiwa wa ufisadi na kesi kuahirishwa.

Mfano ni kesi ya sakata ya wizi wa pesa katika mfuko wa kitaifa wa huduma kwa vijana nchini Kenya NYS.

Je ni kweli mahakama nchini Kenya zinakwamisha juhudi za kukabiliana na ufisadi?

Kulingana na katiba ya Kenya kila mtu ana haki ya kupewa dhamana anaposhtakiwa.

''Sheria za Kenya zinasema kila mtu hana hatia mpaka uamuzi juu ya kesi yake utakapotolewa, na kabla hajapatikana na hatia mahakama haina idhini ya kumyima dhamana hata kama anakabiliwa na shutuma za mauaji au uhaini,'' anasema wakili nchini Kenya Bi Joy Mdivo.

Kulingana na Bi Mdivo kuna sera za muongozo wa mahakama ambazo huwasaidia majaji kuweka kiwango cha dhamana anachopaswa kutozwa mshtakiwa na muongozo huo ndio uliotumiwa katika kumtoza dhamana Waziri Rotich.

''Dhamana hutolewa kulingana na uwezo au kipato cha mtu.'' Amesema wakili Mdivo katika mahojiano na BBC na kuongeza kuwa: ''Dhamana humshurutisha mshtakiwa kurudi mahakamani na kuendelea na kesi''

Haki miliki ya picha Joy Mdivo
Image caption Bi Joy Mdivo, wakili nchini Kenya

Hata hivyo amesema Wakenya wana sababu ya kulalamikia mahakama kwa kuchelewesha kesi, baada ya washtakiwa kutoa dhamana.

''Mtu akishapewa dhamana kesi zinazoroteshwa, kwa kweli hilo ndilo swala ambalo watu wengi wanalizungumzia, unakuta kesi inachukua muda mreefu, kiasi cha kumpa mshtakiwa muda wa kuvuruga ushahidi'' Amesema Mudivo.

Dhamana huambatana na masharti mengine yanayotolewa na mahakama kwa mshtakiwa, ili kumzuwia kuvuruga kesi, mfano kumzuwia asirejee mahala pake pa kazi, kumyang'anya paspoti, kumzuwia kukutana na watu wanaodhaniwa kuwa mashahidi, kuripoti polisi au mahakamani mara kwa mara na masharti mengine.

Bi Joy Mdivo anasema kwa upande mwingine mahakama hutoa maamuzi ya kesi au dhamana kulingana na ushahidi na mashtaka ambayo yamewasilishwa mbele yake na upande wa idara ya upelelezi na waendesha mashtaka.

Anasema maafisa hao wana jukumu la kuchunguza kesi vyema na kutoa ushahidi wa kutosha kwani wasipofanya hivyo mshtakiwa ataachiiliwa hata kama ana hatia.

''Kama hakuna ushahidi huwezi kumfunga mtu kwasababu anasemekana kuwa ni fisadi'' Amesisitiza wakili Mdivo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii