Kenya: Waziri wa Fedha Henry Rotich amefutwa au amesimamishwa kazi?

Henry Rotich Haki miliki ya picha AFP
Image caption Henry Rotich aliteuliwa kuwa waziri wa Fedha mwaka 2013

Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich amesimamishwa kazi siku moja tu baada ya kushtakiwa mahakamani kwa ufisadi.

Henry Rotich anatuhumiwa kuhusika katika kashfa ya ufisadi ya zaidi ya dola milioni 600 katika mradi wa kujenga mabwawa mawili, japo amekana kuhusika na uovu wowote.

Aliyekuwa Waziri wa Leba Ukura Yatani ameteuliwa na Rais kuhudumu kama kaimu Waziri wa Fedha.

Swali ni je Waziri Henry Rotich amefutwa kazi au amesimamishwa kazi?

''Ukidadisi swala hili kwa undani ni wazi Bw. Henry Rotich amefutwa kazi'' alisema mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi ambaye amekuwa akifuatilia taarifa hii.

Kwa mujibu wa Msemaji ya Rais Kanze Dena, Rais alichukua hatua hiyo ili kuhakikisha kuwa shughuli katika wizara ya fedha hazitaathiriwa kufuatia amri ya mahakama iliyotolewa dhidi ya Bw. Henry Rotich na katibu wake Kamau Thuge ambaye pia ameng'atuliwa.

Haki miliki ya picha YASUYOSHI CHIBA
Image caption Waziri wa fedha Kenya Henry Rotich

Siku ya Jumanne Mahakama iliwaachilia kwa dhamana wawili hao baada ya ya $150,000 baada ya kukana zaidi ya mashtaka 10 yanayohusiana na ufisadi

Rotich na mshtakiwa mwenzake katibu mkuu Kamau Thugge wameagizwa kuwasilisha pasipoti zao za usafiri kama sehemu ya masharti ya dhamana.

''Unavyojua Kenya kesi inaweza kuendelea kwa zaidi ya mwaka au miwili, hii inamaanisha muda huo wote hatakuwa akifanya kazi. Bila shaka kuna uwezekano huyu bwana amefutwa kazi'' alisema mwandishi wa BBC.

Hakimu Douglas Ogoti amewazuia washukiwa wasifike katika makao ya wizara ya fedha, na kufafanua kwamba sasa eneo hilo linachunguzwa kwa uhalifu.

Mashtaka dhidi ya Rotich yanatokana na uchunguzi wa polisi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika miradi miwili ya mabwawa magharibi mwa taifa hilo ambayo yalikuwa yakisimamiwa na kampuni moja ya Italia kwa Jina CMC Di Ravenna.

Kenya pia itaomba kurudishwa nchini kwa Paolo Porcelli, mkurugenzi wa kampuni ya CMC di Ravenna, ili kushtakiwa, nchini mkurugenzi wa mashtaka aliambia chombo cha habari cha Reuters.

''Kuna huyu raia wa Itali, hakuweza kufikishwa mahakamani hivyo basi tutaomba ahukumiwe hapa nchini , Tutahakikisha kuwa kibali cha kimataifa cha kukamatwa kwake kimetolewa'', alisema Noordin Haji.

CMC di Ravenna amekana kufanya makosa. Katika taarifa siku ya Jumatatu, kampuni hiyo ilisema siku ya Jumatatu kwamba haijaelezewa kuhusu mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa mamlaka .

Mabwawa hayo mawili yalipangiwa kugharimu dola bilioni 46 lakini wizara ya fedha ilikopesha bilioni 63 badala yake , alisema Hajj siku ya Jumatatu hivyobasi kuongeza deni kubwa la Kenya ambalo linadaiwa kufikia asilimia 55 ya mapato ya taifa hilo.

Swali linaloulizwa na baadhi ya wadadisi wa masuala ya kiuchumi ni ikiwa kaimu waziri wa Fedha Ukur Yatani ana uwezo wa kuendesha gurudumu la uchumi wa Kenya.

Kuna wale wanaosema kuwa uamuzi wa rais kumteua Bw. Ukur Yatani kushikilia wadhifa huo kwa muda umechangiwa zaidi na maslahi ya kisiasa.

Wakati wa kuunda serikali ya Jubilee Rais Kenyatta na naibu wake waligawana wizira katika baraza la mawaziri.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa kwa upande wao wanasema Bw. Kenyatta aliamua kuamteua mtu ambaye hataibua hisia za kisiasa kushikilia nafasi hiyo kwa muda ili aendelee na kazi akisubiri kesi kuamuliwa kwa kesi inayomkabili Henry Rotich.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii