Marekani kutekeleza adhabu kifo kwa mara ya kwanza tangu 2003

Mwanasheria Mkuu William Barr Haki miliki ya picha Reuters
Image caption “Idara ya haki inazingatia utawala wa sheria kwa sababu tunawajibu wa kuitendea haki familia ya wahasiriwa wa mauaji ," anasema mwanasheria mkuu William Barr

Serikali ya Marekani imeidhinisha adhabu ya kifo ianze tena kutekelezwa baada ya adhabu hiyo kusitishwa miaka 16 iliyopita, yasema Idara ya mahakama.

Katika taarifa mwanasheria mkuu William Barr amesema kuwa tayari ameiiagiza Halmashauri ya magereza kupanga siku ya kunyongwa kwa wafungwa watano waliopewa adhabu hiyo.

Bw. Barr amesema watano hao walishitakiwa kwa kuhusika na mauaji na ubakaji wa watoto na watu wazima.

Hukumu dhidi yao imepangwa kutekelezwa Decemba 2019 na Januari 2020.

"Kwa kuzingatia pande zote mbili husika, Idara ya haki imeomba kutekelezwa kwa hukumu ya kifo dhidi ya wahalifu sugu," ilisema tarifa ya Bw. Barr.

"Idara ya haki inazingatia kikamilifu utawala wa sheria - na ni wajibu wake kutekeleza hukumu iliyotolewa dhidi ya mshtakiwa kwa niaba ya wahasiriwa wa uhalifu na familia zao."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Chumba cha mauaji, Huntsville, Texas

Tangazo hilo limefutilia mbali makubaliano ambayo hayakuwa rasmi ya kusitisha adhabu ya kifo - hali ambayo ilikuwa inapinga uamuzi wa mahakama kuhusu adhabu ya kifo.

Adhabu hiyo ilitekelezwa mara ya mwisho mwaka 2003 dhidi ya Louis Jones Jr, 53, mbabe wa vita vya Ghuba aliyemua askari wa miaka 19 Tracie Joy McBride.

Adhabu ya kifo iliondolewa na mamlaka ya majimbo nchini Marekani mwaka 1972 lakini uamuzi huo ulibatilishwa na mahakama bya juu zaidi mwaka 1988.

Kwa mujibu wa data zilizokusanywa na kituo kinachonakili taarifa kuhusu adhabu ya kifo, watu 78 walihukumiwa adhabu ya kifo kati ya mwaka 1988 na 2018 lakini ni watatu kati ya waliouawa.

Kuna wafungwa 62 ambao wanakabiliwa na hukumu ya kifo kufikia sasa.

Br. Barr amesema kuwa ameiagiza Halmashauri ya magereza kubuni sera itakayoidhinisha utumizi wa dawa moja kumuua mtu badala ya kutumia aina tatuya dawa ambayo ilikuwa ikitumika hapo mbeleni.

Mtu anapodungwa sindano ya sumu ya dawa hiyo anapatwa na usingizi, baadae viungo vyake vya mwili hulemaa pole pole hadi mfumo wa neva unapoacha kufanya kazi taratibu akiwa bado usingizini hadi umauti unapomfika.

Idara ya haki imesema watu watano walio kwenye orodha ya kifo ni:

Daniel Lee Lewis, aliyeua familia ya watu watatu akiwemo mtoto wa kike wa miaka minane.

Lezmond Mitchell, aliyemuua mwanamke wa miaka 63 na mjukuu wake wa mwaka mmoja.

Wesley Ira Purkey,aliyembaka na kumuua msichana wa miaka 16 na pia kumuua mwanamkea wa miaka 80.

Alfred Bourgeois, aliyemnyanyasa na kumuua mtoto wake mdogo wa kike wa miaka miwili.

Dustin Lee Honken, ambaye aliwaua watu watano miongoni mwao watoto wawili.

Mauaji ya watu hao yatafanyika katika Jela ya Terre Haute linalowazuilia wafungwa wanaokabiliwa na uhalifu mkubwa, mjini Indiana, mauaji ya wengine yatekelezwa baadae, idara ya haki ilisema.

Adhabu ya kifo Marekani

  • Adhabu ya kifo imehalalishwa kisheria katika majimbo 29 nchini Marekani
  • Tangu mwaka 1976, Jimbo la Texas limetekeleza adhabu (561),ikifuatiwa na Virginia (113) na Oklahoma (112)
  • Kuna wafungwa 2,673 wanaokabiliwa na hukumu ya kifo nchini Marekani
  • California inaidadi kubwa ya wafungwa waliohukumiwa kifo - 733 - lakini ni wafungwa 13 pekee waliouawa tangu mwaka 1976
  • Idadi ya kila mwaka ya hukumu ya kifo kwa imepungua kwa 85% kati ya mwaka 1998 na 2018 - kutoka 295 hadi 43

Chanzo: Taarifa ya Kituo cha adhabu ya kifo

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii