Mkusanyiko wa habari za kandanda Ulaya: Sane, Origi, Trezeguet, Gareth Bale, Lookman, Ayew

Sane

Pep Guardiola amesema kuwa anamtaka Leroy Sane kusalia Manchester City lakini amekiri kwamba uamuzi huo hauko mikononi mwake.

Sane, 23, ana miaka miwili iliosalia katika kandarasi yake lakini bado hajaanza mazungumzo ya kuongeza kandarasi mpya

Winga huyo wa Ujerumani alifunga mara mbili katika mechi ya ushindi dhidi ya timu ya Hong Kong Kitchee katika mechi ya hivi karibuni ya maandalizi ya msimu ujao - Huku David Silva , Raheem Sterling na kinda wa Uhispania Nabil Touaizi pamoja na Iker Pozo wakifunga.

Bayern Munich inataka kumsaini Sane.

"Tunamtaka asalie na kuna ofa inayosubiri ya kuongeza kandarasi yake'' , alisema Guradiola. ''Hatma yake haipo mikononi mwetu ,Ameamua . Iwapo anataka kuondoka anaweza kufanya hivyo lakini hatutafurahia''

Gareth Bale alifunga katika mechi yake ya kwanza akiichezea Real Madrid, lakini hatma yake katika klabu hiyo haijulikani.

Bale aliingia kama mchezaji wa ziada baada ya kipindi cha mapumziko na kufunga huku Real Madrid ikijipatia ushindi wa 2-2 dhidi ya Arsenal katika kombe la kimataifa.

Baada ya mechi hiyo mjini Maryland, mkufunzi Zinedine Zidane alisema: Alicheza vyema na nafurahia. Lakini raia huyo wa Ufaransa aliongezea: Hakuna kitu kilichobadilika, munajua hali ilivyo.

Zidane amenukuliwa akisema kwamba Bale anakaribia kuondoka katia klabu hiyo na kwamba kuondoka kwake itekuwa vyema kwa kila mtu.

Mshambuliaji wa Liverpool na Ubelgiji Divock Origi anasema kwamba hisia fulani ilimwambia kiusalia Liverpool na mshambuliaji huyo yuko tayari kuendelea na ufungaji wa magoli yaliosaidia timu yake kutawazwa bingwa Ulaya.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 hakuanzishwa hata mechi moja ya ligi ya Uingereza msimu uliopita kabla ya mwezi Disemba na angeondoka Anfield mwezi Janurai.

Lakini sasa amesaini kandarasi ya mda mrefu. Anatarajiwa kuanza kucheza mbele msimu huu. Washambuliaji Sadio mane, Mohammed Salah na Roberto Firmino wote wamekosa michuano ya maandalizi ya timu hiyo baada ya michuano ya kombe la Afrika.

RB Leipzig wamekamilisha usajili wa mchezaji wa Everton na timu ya uingereza isiozidi umri wa miaka 21 Ademola Lookman katika mkataba ulio na thamani ya £22.5m.

Klabu hiyo ya Beundelsiga ililazimika kuimarisha ofa yao ya awali ili kumsaini mchezaji huyo wa miaka 21 katika mkataba wa miaka mitano. Lookman alihudumu kwa mkopo na klabu hiyo ya Ujerumani katika kipindi cha pili cha msimu wa 2017-18, akifunga magoli 11 katika mechi 11 za ligi.

Aston Villa Imemfanya winga wa Misri Trezeguet kuwa mchezaji wao wa tisa msimu huu kumsaini kwa dau la £8.75m .

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, ambaye alicheza mara nne na kufunga goli moja katika kombe la Afrika , anatoka katika klabu ya Uturki Kasimpasa.

Alianza kusakata soka na klabu ya Misri ya Al Ahly kabla ya kuelekea Anderlecht 2015, akijiunga na Kasimpasa miaka miwili baadaye.

Tunafurahia sana kufanya kazi na Trez , alisema Mkufunzi wa Villa Dean Smith.

Crystal Palace imemsani mshambuliaji wa Swansea Jordan Ayew kwa mkataba wa miaka mitatu.

Ayew, mwenye umri wa miaka 27 alihudumu msimu uliopita katika uwanja wa Selhurst Park kufuatia kushushwa daraja kwa Swansea katika ligi ya Uingereza.

Dau hilo linatajwa kuwa £2.5m kwa mchezaji huyo wa Ghana ambaye alifunga mara mbili katika mechi 25 akiichezea Palace katika misimu miwili iliopita.

''Nafurahia kurudi. Niliurahi sana msimu uliopita'', alisema.