Kushamiri biashara ya punda inaathiri uwepo wa wanyama hao

Punda
Maelezo ya picha,

Wanyama punda wako hatarini kutoweka nchini Kenya

Idadi ya Punda nchini Kenya imekuwa ikipungua, kwa mujibu ripoti iliyotolewa na wanaharakati wa wanyama.

Kundi hilo la mtandao wa watetezi wa haki za wanyama, (ANAW) limesema kuwa punda wamekuwa wakitoweka haraka sana.

Ripoti imesema tangu kufunguliwa kwa maeneo manne ya machinjio ya punda kwa ajili ya biashara mwaka 2016, ''idadi kubwa ya wanyama hao huchinjwa kila siku''.

Inakadiriwa kuwa punda 410 huuawa kila siku.

ANAW limesema kuwa ngozi ya punda inahitajika sana nchini China.

Ripoti imeongeza kuwa suala hilo lilishawekwa wazi mwaka 2017. Wakati huo BBC iliporipoti kuhusu madai ya watu kulalamika kuibwa kwa punda wao ili kupelekwa kwenye soko.

Lakini mkuu wa machinjio amesema: ''tunafurahia wachina, kwasababu awali tulikuwa hatupati chochote kutokana na punda, lakini watu wengi sasa wananufaika.''

Shirika la kuteteta haki za wanyama limetaka machinjio yote ya wanyama hao yafungwe.

Ripoti ya shirika hilo inakadiria uwepo wa punda 900,000 mpaka milioni 1.8 nchini Kenya.

Maelezo ya picha,

Baadhi ya nchi za Afrika zimepiga marufuku biashara ya punda

Uzinduzi wa kichinjio cha punda

Kichinjio cha kwanza cha Punda kilizinduliwa nchini Kenya mnamo 2014.

Ilitokanana ongezeko la visa vya wizi wa wanyama hao ambao hutumiwa kubeba mizigo na kuchinjwa kisiri huku nyama yake ikiuziwa wateja wasiokuwa na habari kuwa wananunua nyama ya Punda.

Kwa muda mrefu mizoga ya wanyama hao imekuwa ikipatikana kando ya barabara au msituni ambako wezi huificha baada ya kuwachinja.

Mradi wa ujenzi wa kichinjio cha Punda uliidhinishwa katika mji wa Naivasha nje kidogo ya mji mkuu Nairobi.

Kichinjio hicho ni cha kwanza Kenya cha nyama ya Punda.

Kushamiri kwa biashara ya punda

Shirika moja linalohusika na maslahi ya wanyama nchini Kenya, linasema bei ya Punda imepanda mara dufu nchini humo kwa sababu ya nyama ya mnyama huyo kuongezeka hasa katika taifa la china taifa ambalo hununua kwa wingi bidhaa ya mnyama huyo

Kwa mujibu wa shirika hilo, sababu ya bei ya Punda kupanda kwa karibu asilimia 200 ni kutokana na ongezeka la biashara ya bidhaa za mnyama huyo huko Uchina ambako nyama ya punda ni kitoweo kilicho na walaji wengi.

Mataifa kadhaa ya kiafrika yamepiga marufuku uuzaji ya nyama na bidhaa nyenginezo za punda, kwa ajili ya soko hilo la Uchina, kwa sababu punda ambao hutumiwa zaidi kwa ajili ya kusaidia kubeba mizigo mashambani, sasa idadi yao inapungua kwa kasi mno.

Kuna hofu kuwa huenda baadhi ya watu wanawasafirisha punda kimagendo hadi machinjioni kutokana na kupanda kwa bei yake.

Maelezo ya sauti,

Hospitali ya kipekee inayowahudumia punda Kenya

Mataifa mengi yamepiga marufuku uchinjaji wa nyama ya punda yakiwemo mataifa kadhaa ya Afrika kama vile Uganda, Tanzania, Botswana, Niger, Burkina Faso, Mali, na Senegal.

Mataifa hayo aidha yameipiga marufuku China kununua ngozi ya punda kwani huenda ikamaliza kabisa wanyama hao duniani.

Soko kubwa la ngozi ya punda pia imeongezeka nchini Afrika Kusini.