Rais wa Tanzania John Magufuli asafiri kwa Treni kwenda Rufiji

Rais wa Tanzania Dk John Magufuli
Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania Dk John Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza tangu awe rais anasafiri kwa Treni kuelekea Rufiji.

Aliingia kwenye moja ya mabehewa ya treni ya TAZARA kwa ajili ya safari ya kuelekea kuweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa kufua umeme katika mto rufiji utakaozalisha umeme wa kilowati 2115

Watu mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti kuhusu hatua ya rais Magufuli kusafiri kwa Treni badala ya usafiri ambao kwa maoni yao wanaona kuwa unamfaa zaidi kwa hadhi yake, wengine wakiona ni jambo jema na kuwataka viongozi wengine ambao hutumia usafiri wa hadhi ya juu kufuata mfano wa rais Magufuli.

Awali kabla ya kupanda treni, Rais Magufuli alizungumza na viongozi wa TAZARA na kuwataka kuwasilisha mapendekezo yao juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia TAZARA.Rais Magufuli amesema Serikali inatambua umuhimu wa shirika hilo.

Akizungumza kuhusu changamoto za wafanyakazi rais Magufuli ameutaka uongozi wa shirika hilo kutatua kero za wafanyakazi wa TAZARA kwa mazungumzo ya pande zote mbili.

''Hakikisheni wafanyakazi mnawasaidia hawa wafanyakazi wako frustrated,nimewauliza maswali hawakutaka kuzungumza kwa sababu wameogopa, hawataki kuongea chochote.Si kwamba hawana shida,wana shida kibao, ila wanawaogopa ninyi inawezekana mnawatishia kwamba mtu akizungumza anafukuzwa. Mkae na wafanyakazi mzungumze shida zao mzitatue, zile zinazoshindikana mzilete serikalini''. Alisema Magufuli.

Reli ya Tazara yenye urefu wa kilomita 1,860 ina uwezo wa kusafirisha tani milioni tano za mizigo kwa mwaka, lakini kutokana na upungufu wa injini na mabehewa ya kutosha, inasafirisha chini ya tani 300,000 kwa mwaka.

Reli hiyo ilijengwa kwa msaada kutoka China, ilianza huduma mwaka 1975 na inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 kwa 50 wa nchi ya Tanzania na Zambia.