Saudi Arabia yatangaza kusitisha zoezi la utoaji viza kwa mahujaji wa Drc

Mamilioni ya watu husafiri mpaka Makka kwa ajili ya ibada ya Hija
Image caption Mamilioni ya watu husafiri mpaka Makka kwa ajili ya ibada ya Hija

Saudi Arabia haitatoa viza ya kusafiria kwa mahujaji kutoka nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imeeleza wizara ya mambo ya nje katika taarifa yake.

Wizara imesema uamuzi ulifikiwa kutokana na uamuzi wa shirika la afya duniani, WHO kutangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC ni suala la dharura inayohitaji kushughulikiwa na jumuia ya kimataifa.

''Mpango wa kutoa viza kwa watu wanaoingia kutoka DRC umesimamishwa, kwa ajili ya usalama wa mahujaji,'' wizara.

Saudi Arabia awali ilisema takribani watu 410 kutoka nchini DRC wanatarajia kwenda kuhiji mjini Makka baadae mwezi huu, Kiongozi wa kiislamu nchini Drc, Imamu Djuma Twaha, aliiambia BBC.

''Kuna watu walikuwa wamejiandaa kwa miaka mingi, wakati mwingine miaka kumi wakijichanga kiasi cha pauni 3,400 kwa ajili ya kufanya safari kwa ajili ya hija,'' alieleza.

WHO ilitangaza hali ya dharura kutokana na mlipuko wa Ebola tarehe 17 mwezi Julai, lakini imezitaka nchi kutofunga mipaka yao dhidi ya watu wanaofanya safari au biashara.

Kwa nini wanaotoroka mapigano DRC wanaathiri 'juhudi za kudhibiti Ebola'

Zaidi ya watu 2,000 wameripotiwa kuugua Ebola nchini DRC

Hali ni mbaya kiasi gani nchini humo?

Mlipuko wa Ebola ni ugonjwa wa pili kwa ukubwa katika historia ya nchi hiyo, ulianza mwezi Agosti na inaathiri majimbo mawili nchini DRC, Kivu Kaskazini na Ituri.

Zaidi ya watu 2500 wameathiriwa na ugonjwa huo na theluthi mbili kati yao wamepoteza maisha.

Ilichukua siku 224 kwa idadi ya walioathirika kufika 1,000 , lakini ndani ya siku 71 zaidi idadi ilifika 2,000.

Watu takribani 12 huripotiwa kupata ugonjwa huo kila siku.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mwanamke akipimwa dalili za Ebola

Kwanini ugonjwa huu haujadhibitiwa?

Wafanyakazi wa afya wamekua wakipata vikwazo vya kutoaminika na machafuko nchini humo.

Watu wengine hawawaamini watoa huduma za afya, hivyo hufanya watu wenye dalili za ugonjwa huo kukwepa matibabu, hali hii inawia vigumu kuzuia kuenea kwa virusi vya ebola.

Ingawa zaidi ya watu 1,300 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti, Shirika la misaada la Oxfam linasema linakutana na watu kila siku ambao hawaamini kama kuna virusi vya ebola.

Tangu mwezi Januari kulikua na matukio 198 ya mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, na kusababisha majeruhi 58.