Mahakama: Ruhusa kwa Trump kutumia fedha za jeshi kujenga ukuta

Ukuta wa mpakani Haki miliki ya picha EPA

Mahakama kuu nchini Marekani imesema kuwa Raisi Donald Trump anaweza kutumia pauni bilioni mbili. fedha za idara ya ulinzi kwa ajili ya sehemu ya gharama za ujenzi wa ukuta wa mpaka wa kusini.

Mahakama imetoa uamuzi huo kwa ushindi wa kura tano kwa nne kuzuia hukumu ya jaji wa jimbo la California ambaye alimzuia raisi kutumia kiasi hicho cha fedha kwa kujenga ukuta.

Ukuta, unaotenganisha Marekani na Mexico, ilikuwa kampeni kubwa ya Trump, ahadi aliyoitoa kwenye wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2016.

Lakini mpango huo ulipingwa vikali na Democrats.

Marekani imesema imeidungua ndege isiyo na rubani ya Iran

Marekani yatoa dola $1b kujenga ukuta kati yake na Mexico

Uamuzi wa mahakama kuu unamaanisha kuwa fedha zitatumika kwa ajili ya miradi ya ukuta katika jimbo la California, Arizona na New Mexico.

Mahakama ya California ilidai kuwa bunge la Congress halikuidhinisha fedha hizo mahususi kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa ukuta.

Katika ukurasa wake wa twitter, bwana Trump amesema uamuzi huo ni ''ushindi mkubwa''

Raisi amedai kuwa ukuta mpya utasaidia kupambana na uhamiaji haramu, ambao amesema umekuwa mchango kwa kuchochea uhalifu na kuzorotesha uchumi.

Wabunge wa Democrat wamesema wanaunga mkono suala la usalama wa mipaka lakini ujenzi wa ukuta ni gharama kubwa na si njia ya kupata suluhu.

Siku ya Ijumaa, Marekani na Guatemala walitia saini makubaliano, ambayo yatafanya wahamiaji kutoka Honduras na El Salvador wanaopitia Guatemala kuanzia kuomba hifadhi nchini Guatemala kwanza, kabla ya moja kwa moja kuingia Marekani.

Uamuzi umepokewaje?

Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema: ''Jioni hii uamuzi wa mahakama ya juu kumruhusu Donald Trump kuiba fedha za jeshi na kuzipoteza kwenye ukuta, mpango ambao bunge halikuunga mkono ni jambo la udhaifu kabisa.Waasisi wetu waliweka misingi ya demokrasia ya watu- na si ufalme.''

Asasi ya kiraia ya The American Civil Liberties Union (ACLU) imeapa kupata uamuzi wa haraka kwenye mahakama ya rufaa ''dhidi ya mpango wa Trump''.

Gloria Smith, wakili wa wanaharakati wa mazingira ambao wamekuwa wakipinga mpango huo amesema: ''Uamuzi wa leo kuruhusu fedha za jeshi kujenga ukuta wa mpaka utatenganisha na kuharibu jamii, aridhi za watu na maji jimboni California, New Mexico na Arizona.''

Haki miliki ya picha EPA

Trump alitangaza hali ya dharura mwanzoni mwa mwaka huu, akisema anahitaji dola bilioni 6.7 kujenga ukuta kwa ajili ya ulinzi wa usalama wa taifa. Hatahivyo kiasi hicho ni kidogo sana ikilinganishwa na makadirio ya dola bilioni 23 kwa ajili ya mpaka wa umbali wa kilomita 3,200.

Wabunge wa democrat walidai kuwa uamuzi wa Trump kutangaza hali ya dharura alizidisha mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya Marekani.

Majimbo takriban 20, sambamba na wanaharakati wamefungua shauri kujaribu kumzuia raisi kutumia dharura kuruka mamlaka ya congress.

Makundi ya wanaharakati wa mazingira wamekuwa katika kampeni ya kupinga jitihada za Trump wakidai kuwa ujenzi wa ukuta utaleta athari kwa wanyama pori.

Bunge la wawakilishi pia linachukua hatua za kisheria kuzuia fedha zaidi kutolewa kwa ajili ya mradi wa ukuta.

Kinachoendelea mpakani.

Kwa mujibu wa mamlaka za nchini Marekani, watu 104,344 walikamatwa katika mpaka wa kusini magharibi mwezi Juni- idadi iliyopungua kwa asilimia 28 ikilinganishwa na mwezi wa tano.

Utawala wa Trump umedai kuwa kupungua kwa idadi hiyo ni kutokana na sera mpya zilizowekwa ili kupambana na uhamiaji, ikiwemo kuongeza ulinzi wa mpaka wa upande wa Mexico na mpango wa kuwasubirisha nchini Mexico watu wanaotafuta hifadhi wakati maombi yao yakifanyiwa kazi.

Ripoti ya Umoja wa mataifa kuhusu wahamiaji wasiojulikana walipo imeripoti kuwa wahamiaji 170 wamepoteza maisha au kupotea kwenye mpaka wa Marekani na Mexico mpaka sasa wakiwemo watoto 13.

Idara ya usalama imesema ''bado tunakabiliwa na changamoto ya usalama mpakani na masuala ya kibinaadamu''.