Sudan kuwashtaki maafisa wa jeshi waliotekeleza uhalifu dhidi ya binaadamu

Vikosi vya kijeshi vya Sudan Haki miliki ya picha AFP

Maafisa wa jeshi wanane watashtakiwa nchini Sudan kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binaadamu, wakidaiwa kushiriki vitendo vya mauaji ya waandamanaji tarehe 3 mwezi Juni.

Waendesha mashtaka wa serikali walitangaza hatua hiyo baada ya kufanyia uchunguzi vitendo vya mauaji, baada ya watu takribani watu 87 kupoteza maisha mjini Khartoum.

Wanaharakati wapinzani wanasema kuwa idadi ya waliopoteza maisha inakaribia 130.

Waandamanaji waliuawa mwezi Juni baada ya vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakilitaka jeshi kukabidhi madaraka kwa raia.

Kwa sheria ya kijeshi ya Sudan, hukumu ya uhalifu dhidi ya binaadamu ni adhabu ya kifo.

Mamluki katili wanaotawala nchi kwa dhahabu

Jeshi la Sudan lasaini makubaliano ya kugawana uongozi na upinzani

Fath al -Rahman Saeed, alikuwa kiongozi wa kamati aliyeteuliwa kuchunguza vitendo vya mauaji, hakutaja majina ya maafisa wanaoshutumiwa kutekeleza vitendo hivyo.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa maafisa watatu walikiuka amri kwa kupeleka vikosi vya usalama kwenye eneo ambalo waandamanaji walikuwa wamepiga kambi nje ya jengo la wizara ya ulinzi.

Haki miliki ya picha AFP

Vikosi vya usalama ''vilivunja sheria na kuingia kwenye eneo hilo'', alinukuliwa na shirika la habari la Ufaransa akisema ''Waliondoa vizuizi, wakafyatua gesi ya kutoa machozi kisha kufyatua risasi hovyo hovyo na kusababisha watu kupotea maisha na wengine kujeruhiwa, pia maturubai yao yaliungua moto.''

Mwenyekiti wa kamati pia ametetea uamuzi wa kusambarataisha makundi ya watu kwenye eneo jingine akisema: ''Baadhi ya watu waliunda mkusanyiko kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya uvunjaji sheria.

''Hali hiyo ilisababisha tishio la kiusalama, hali iliyolazimu mamlaka kuchukua hatua.''

Idadi yaa waliopoteza maisha imedaiwa kuwa 87 huku wengine 168 walijeruhiwa.

Athari gani zilizojitokeza baada ya mauaji ya tarehe 3 mwezi Juni?

Kulikuwa na hali ya taharuki miongoni mwa wapinzani, ambao walikuwa wamepiga kambi nje kwa miezi kadhaa na maandamano yaliyomuondoa madarakani raisi Omar al- Bashir mwezi Aprili

Hatahivyo, maelfu ya waandamanaji walirejea mitaani majuma machache baadae baada ya kung'oka kwa utawala wa Bashir. Maandamano hayo makubwa yaliwafanya majenerali kurejea mazungumzo kuhusu kugawana madaraka.

Hatimaye pande mbili zilikubaliana.

Siku ya Jumamosi, waandamanaji kadhaa waliimba nyimbo zenye maneno ya kuonyesha kutokubaliana na kamati ya uchunguzi katika wilaya ya Burri mjini Khartoum, mashuhuda waliliambia shirika la habari la Reuters. Magurudumuuu yalichomwa moto na waandamanaji hao.