Nicolas Pepe: Arsenal imeingia makubaliano ya dau la £72m kumnunua winga matata wa Lille

Nicolas Pepe Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Pepe alifunga magoli 23 katika mechi 41 akiichezea Lille msimu uliopita

Arsenal wameafikia makubaliano na klabu ya Ufaransa ya Lille kumsaini winga wa Ivory Coast Nicolas Pepe katika makubaliano yenye thamani ya £72m.

Arsenal italipa kitita hicho kwa awamu kadhaa kulingana na bajeti yao msimu mpya. Makubaliano kati ya Arsenal na wawakilishi wake bado yanasubiri kukamilishwa.

Lakini uhamisho huo unatarajiwa kukamilishwa katika kipindi cha saa 24 na 48. Klabu ya Itali Napoli pia ilikutana na Lille kuhusu bei ya mchezaji huyo lakini pendekezo lao likafutiliwa mbali na kambi ya mchezaji huyo.

Pepe hupendelea kucheza upande wa kulia na kuingia katikati ya uwanja kupitia mguu wake wa kushoto , lakini pia anaweza kutumika kama mshambuliaji katika mfumo wa 4-2-2.

Aliifungia Lille magoli 23 msimu uliokwisha na anaridhisha mahitaji ya Arsenal kwa mchezaji atakayecheza katika wingi kutokana na kasi yake na ufundi.

Arsenal ilitoa dau la £40m kumsajili winga wa Crystal Palace Wilfried Zaha mapema mwezi huu , lakini Crystal Palace inasema kwamba mchezaji huyo ana thamani ya £80m.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii