Mgogoro kati ya Uingereza na Iran: Uingereza yapeleka meli ya pili ya kijeshi Ghuba

Meli ya wanajeshi wa Uingereza HMS Duncan yawasili katika mkondo wa bahari wa Hormuz Haki miliki ya picha MINISTRY OF DEFENCE

Meli ya pili ya wanamaji wa Uingereza imewasili katika Ghuba ili kuzilinda meli za Uingereza huku kukiwa na hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

HMS Duncan ilijiunga na HMS Frigate Montrose kusindikiza meli za mafuta zinazobeba bendera ya Uingereza kupitia mkondo wa bahari wa Hormuz.

Waziri wa ulinzi Ben wallace amesema kuwa Uingereza itaendelea kusukuma mazungumzo ya kidiploamsia hadi suluhu itakapopatikana.

Alisema: Uhuru wa kusafiri katika mkondo wa bahari a Hormuz ni muhimu kwa Uingereza mbali na washirika wetu wa kiamatiafa.

Meli za biashara ni sharti ziruhusiwe kusafiri kihalali na kufanya biashara kwa njia ilio salama mahali popote duniani.

Bwana Wallace aliongeza kwamba wanamaji wa Uingereza wataendelea kuzilinda meli zinazopeperusha bendera za Uingereza hadi hali ya usalama itakaporudia ilivyokuwa awali.

HMS Duncan ni meli ambayo imetajwa na Uingereza kuwa ya kisasa zaidi kutengenezwa.

Kwa nini wasiwasi umeongezeka?

Mapema mwezi huu , wanamaji wa Uingereza walisaidia katika kuikamata meli ya mafuta ya Iran kwa jina Grace 1 karibu na Gibraltar ambayo ilishukiwa kuvunja vikwazo vya EU hatua iliokasirisha Iran.

Kwa kujibu Tehran ilitishia kuikamata meli ya mafuta ya Uingereza.

Mnamo tarehe 19 Julai , meli ya mafuta iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza kwa jina Sten Impero ilikamatwa na wanajeshi wa Iran katika mkondo huo wa Hormuz.

Meli nyengine ya Uingereza MV Mesdar pia ilikamatwa na walinzi waliojihami lakini ikaachiliwa. Tehran ilisema kwamba Stena Impero ilikiuka sheria ya kimataifa ya majini.

HMS Montrose iliarifiwa lakini ilikuwa mbali kuisaidia meli hiyo.

Vyombo vya habari vya Iran vinasema kuwa meli hiyo ilikamatwa baada ya kugonga boti ya wavuvi na kukataa kusimama.

Lakini waziri wa maswala ya zamani nchini Uingereza Jeremy Hunt alisema kuwa ilikamatwa katika maji ya Omani ikiwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa na baadaye kulazimishwa kuelekea Iran.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii