Takwimu rasmi za serikali: Uchumi wa Tanzania waanza 2019 kwa kuyumba

Dar es Salaam

Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2019 nchini Tanzania yaanza kwa kushuka ukilinganisha na mwaka 2018, takwimu rasmi za serikali zabainisha.

Shirika la Habari la Kimataifa la Reuters limenukuu taarifa ya kutoka kwa Ofisi ya Takwimu ya Tiafa (NBS) la Tanzania kuwa kwa miezi mitatu ya mwanzo ya 2019 uchumi wa nchi hiyo umekuwa kwa 6.6% year-ukilinganisha na kasi ya 7.5% kwa mwaka 2018.

Kwa mujibu wa NBS kushuka kwa kasi hiyo kumetokana na kuyumba kwa sekta za ujenzi, kilimo na uzalishaji wa viwandani.

Sekta ya ujenzi ambayo ndiyo huchangia pakubwa kukua kwa uchumi wa Tanzania imetanuka kwa 13.2%, ukilinganisha na 15.6% mwaka mmoja uliopita.

Sekta ya kilimo ambayo huajiri watu wengi zaidi nchini humo pia imeyumba kwenye miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu, kutoka 8.9% mwaka 2018 mpaka 6.0% kwa mwanzoni mwa mwaka huu, kulingana na NBS.

Kwa upande wa uzalishaji wa viwandani, kasi imeshuka kutoka 5.3% ya 2018 mpaka 4.8% mwaka huu.

Hata hivyo mambo yameenda vizuri kwenye sekta ya madini ambapo kasi ya ukuaji imeimarika takribani mara mbili zaidi ya mwaka jana. Kutoka 5.7% ya mwanzoni mwa mwaka jana mpaka 10.0% katika miezi mitatu ya awali ya mwaka huu.

"Ukuaji (wa sekta ya madini)umetokana na ungezeko wa uzalishaji wa dhahabu, makaa ya mawe na almasi," imesema NBS.

Uchumi wa Tanzania ulikua kwa 7% mwaka jana, na serikali ya chi hiyo ikaweka makadirio ya kukua kwa 7.1% kwa mwaka 2019.

Hata hivyo, ripoti iliyovuja mwezi Aprili ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) ilidokeza kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa hilo si kama vile ilivyotazamiwa na maafisa wa serikali.

Kwa mujibu wa IMF, kasi halisi ipo baina ya asilimia 4 na 5.

Haki miliki ya picha OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU TANZANIA/FACEBOOK
Image caption Albina Chuwa, mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS)

Serikali ya Tanzania kupitia waziri wake wa Fedha ilipinga vikali makadirio hayo na kutaka wananchi wayapuuze.

Serikali ilishikilia msimamo wake kuwa hali ya mambo inaashiria uchumi utaendelea kukua kwa 7%.

Wiki mbili zilizopita, Benki ya Dunia (WB) nayo ilitoa makadirio yake ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2018.

Kwa mujibu wa WB ukuaji wa uchumi Tanzania kwa mwaka jana ulikuwa ni 5.2% na si 7% kama ilivyoeleza serikali.

Albina Chuwa, mkuu wa NBS, amepinga vikali tathmini hiyo ya WB na kutetea njia zilizotumiwa na ofisi yake kufikia kiwango cha 7%.

"Tumekwenda kote nchini kukusanya data (takwimu) halisi , sio sawa na mtu ambaye anakaa Washington (Marekani, ambapo ni makao makuu ya WB) na kutengeneza sampuli za pato la ndani la nchi (GDP) kwa niaba yako,"alisema Bi Albina kulingana na Reuters

"Kwa madhumuni ya mipango ya taifa, tutaendelea kutumia data rasmi za asilimia 7.0."

Mada zinazohusiana