Takwimu zaonyesha 37% ya watoto wilayani Mpwapwa Tanzania wanakosa lishe bora

  • Aboubakar Famau
  • BBC Swahili, Tanzania
utapia mlo

Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma inaripotiwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye tatizo la utapia mlo.

Takwimu rasmi za wilaya hiyo zinaonyesha kuwa asimilia 37 ya watoto elfu sabini waliopo katika eneo hilo, wanakosa lishe bora.

Licha ya huduma na jitihada zinazofanywa kwa sasa na serikali, bado tatizo hilo linaonekana kujikita mizizi.

Kwenye wodi ya watoto katika Hospitali ya wilaya ya Mpwapwa, vitanda kadhaa vina watoto waliolazwa na wazazi wao.

Baadhi ya watoto hao wamelazwa kwa kuathirika kwa utapia mlo kama ilivyo kwa Margaret Ndemunuwinda na mwanawe.

'Tumelazwa hapa tangu Ijumaa, tumbo limejaa gesi alafu alikuwa amevimba usoni na miguuni...mpaka sasa hivi nipo ila bado hajapata nafuu... tatizo sina hela ya kumnunulia lishe' anaeleza Margaret kuhusu hali inayomkabili mwanaye mchanga aliyelazwanaye hospitalini humo.

Renatus Kombo, afisa lishe wilayani Mpwapwa anasema mara nyingi watoto wenye tatizo la utapia mlo, huathirika katika kipindi kama hichi ambacho baadhi ya wazazi wanatumia muda mwingi kuandaa mashamba huku wakiwaacha watoto bila lishe bora.

'Wengine hawafiki katika zahanati kwa wakati' anaeleza Renatus na kuongeza kwamba changamoto ni kubwa ya watu kutoelewa umuhimu wa lishe bora licha ya kwamba vyakula vipo.

'Wanategema sana kwenye (vyakula) vya uwanga. Kama ni ugali wa mtama basi ni ugali wa mtama mwezi mzima. Anasahau kwamba kuna matunda, ubuyu, ila hajui matumizi ya buyu ni nini ila ubuyu una faida kubwa sana. hajui pale nyumbani kuna mayai inabidi ayatumie' anafananua afisa huyo.

Utapia mlo ni nini?

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO hii ni hali inayogusia mapungufu, viwango vya ziada au ukosefu wa usawa wa virutubisho katika chakula anachokula mtu

Takriban watoto milioni 41 walo chni ya miaka mitano duniani wana uzito wa kupitiliza na hiyo ni sehemu ya athari ya ukosefu wa lishe bora, huku wengine milioni 159 wakiathirika ukuwaji kutokana na utapia mlo.

WHO linataja kwamba tatizo linatokana na familia nyingi kutoweza kugharamia chakula au kupata chakula chenye virutubisho vya kutosha kama matunda mboga, maziwa na nyama.

Chanzo cha picha, NICHOLE SOBECKI

Vyanzo vinavyochangia kukithiri utapia mlo:

Uelewa mdogo kuhusu lishe bora, umbali wa vituo vya afya na ugumu wa maisha vyote vimeelezwa kuchangia ongezeko la idadi kubwa ya watoto wenye tatizo hilo katika eneo hilo.

Katika ripoti hiyo ya 2018/2019 ya halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, watoto 485 walio chini ya miaka mitano walikuwa na utapiamlo mkali kwa robo ya tatu ya mwaka, na katika robo ya nne, watoto kulishuhudiwa wagonjwa wapya 230, kati yao 167 wametibiwa, wengine wakitoroka matibabu na 4 wakifariki kutokana na kuchelewa kufika kupokea matibabu.

Monica Chibaluo anasema alichelewa kumfikisha mwanawe aliye na miezi kumi hospitalini kutokana na kwamba nyumbani na hospitalini ni mbali.

'Tulikuwa tunatafuta hela ya kuja hospitalini, baba mtoto amemtelekeza, ...lishe hadi uwe una hela, kama karanga, mchele uwe unaweza kununua ili mtoto apate lishe, hizo hela sikuweza kuzipata'.

Kutokana na changamoto hiyo, maafisa wanaeleza kwamba jitihada zimeidhinishwa za kuwawezesha wauguzi kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi ambao wanaishi na tatizo hilo.Baadhi ya jitihada zinazohitajika kuiboresha hali kwa mujibu wa Renatus ni kuhakikisha miundo mbinu ya usafi na maji salama.

Jitihada za kubadili tabia ya watu kwa kutoa elimu na uhamasishaji kupitia mikutano na katika kliniki.

Kadhalika ametaja umuhimu pia kuwajengea uwezo wanaume kufahamu zaidi uzito na maana ya lishe kutokana na kwamba kama mtafutaj, baba ndiye mhusika, 'kama hawezi kutafuta , ina maana familia itaingia katika matatizo'.