Erick Kabendera: Polisi wa Tanzania wanasema walimkamata mwandishi huyo

kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar Lazaro Mambossasa

Polisi nchini Tanzania imesema kuwa mwanahabari wa Erick Kabendera aliyedaiwa kutoweka hakutekwa bali alikamatwa.

Erick Kabendera anayeandikia magazeti ya ndani na nje ya Tanzania anadaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.

Katika mkutano na vyombo vya habari kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar Lazaro Mambossasa amesema kuwa mshukiwa huyo alikaidi agizo la polisi la kufika mbele yao kwa ajili ya mahojiano

''Mwandishi huyu aliitwa hakutekwa lakini kwa ujeuri alikaidi wito huo.... kimsingi pengine iwapo angewasili angehojiwa na kuachiliwa'', alisema Mambossasa

Amesema kwa sasa polisi wanafanya uchunguzi kuhusu uraia wa mwandishi huyo kwa ushirikiano wa idara ya uhamiaji kabla ya kumwasilisha mahakamani.

''Sisi tunakamata mahali popote, tunaweza kukukamata katika gari , ndani ya msikiti tunasubiri ibada iishe tukuchukue lakini ukikataa kutoka msikiti tunaingia na kukutoa, kanisani hivyo hivyo na nyumbani kwako hata usiseme ni wakati wowote sisi tunakuja tunafanya kazi yetu ya polisi''

aliongezea afisa huyo wa polisi.

Afisa huyo aliwataka raia kuwacha kueneza uvumi kupitia mitandao ya kijamii akisema kuwa kuna utaratibu wa kufuatwa kupitia polisi.

Haki miliki ya picha @MARIASTSEHAI/TWITTER

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania likiwemo Gazeti la Mwananchi pamoja na televisheni ya mtandaoni Mtetezi TV vinadaiwa kuthibitisha taarifa ya kutoweka kwa Bwana Kabendera baada ya kuzungumza na ndugu jamaa na marafiki zake.

''Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kwa ndugu, watu ambao walimkamata walikuwa sita na walijitambulisha lakini hawakutoa vitambulisho vyao.

Watu hao walieleza kuwa wanampeleka mwandishi huyo kituo cha polisi Oysterbay''. Imesema taarifa ya Watetezi TV.

Tukio hilo sio la kwanza kwa kabendera kwani mamake aliwahi kukamatwa na maafisa wa polisi na kuhojiwa kwa saa 10 kutokana na hatua yake ya kabendera kuandika kuhusu ukweli uliokuwa ukifanyika serikalini.

''Kwa miaka mingi nilijaribu kumrai mamangu kwamba uandishi ndio kazi niliokuwa nikiipenda sana. Alinionya kuhusu hatari ya kuandika ukweli katika taifa ambalo lilikua na mfano wa kunyehsa kwamba uhuru wa kuzungumza hakupendwa sana'', kuhusu baadhi ya matukio yaliowahi kumpata.

Wanahabari wanasemaje?

Wakati huohuo Taasisi ya kimataifa ya uanahabari IPI pamoja na waandishi habari tofauti wameshutumu kukamatwa kwa mwandishi huyo wa tanzania.

''Kuzuiliwa kwa Kabendera hakutakubalika. Ni jaribio la kuwanyamazisha wanahabari ambao wamekuwa wakimkosoa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Swala la uraia wake lilichunguzwa na kusuluhishwa 2013, Hivyobasi kukamatwa kwake kunalenga kumtishia na'' , ilisema taarifa ya taasisi hiyo iliotumwa katika vyombo vya habari.

Kulingana na taarifa hiyo kabendera ambaye alitunukiwa tuzo ya david Astor 2009, alikamatwa na wazazi wake kuhojiwa kuhusu uraia wao mwaka 2013. Baadaye wizara ya maswalka ya ndani ilisema kuwa uraia wao hauna shaka.

Wizara hiyo pia iliendelea kwa kuagiza idara ya uhamiaji kuchukua hatua dhidi ya maafisa waliohusika kwa kumdhulumu mwandishi huyo na wazazi wake.

Kulingana na taarifa hiyo ya IPI uhuru wa wanahabari nchini Tanzania chini ya serikali iliopo umepata pigo baada ya magazeti kadhaa , vituo vya redio na runinga kupigwa marufuku .

Baadhi ya visa vya utekaji nchini Tanzania tangu 2015

1. Azory Gwanda, mwandishi aliyekuwa akiandikia gazeti moja nchini Tanzania,

Alitoweka tarehe 21 mwezi Novemba 2017 . Alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na kuingizwa katika gari jeupe aina ya Land Cruiser katika wilaya ya Kibiti

Azory alikuwa mwandishi wa kwanza kuripoti visa vya mauaji yaliotekelezwa na wapiganaji katika eneo la Kibiti ambayo yalionekana yakiwalenga viongozi wa serikali na maafia wa polisi.

Kufikia sasa Aziry hajapatikana

2. Mohamed Dewji alitekwa tarehe 11 Oktoba 2018

Alitekwa na watu waliojihami asubuhi ya tarehe 11 mwezi Oktoba 2018 mjini Dar es Salaam.

Ni bilionea mwenye umri mdogo zaidi kulingana na jarida la Forbes.

Sababu za kutekwa kwake hazijajulikana licha ya polisi kuwakamata watu kadhaa kuhusiana na tukio hilo.

Baada ya siku tisa Mo kama anavyojulikana nchini humo, alitupwa nje ya uwanja wa Gymkana katika barabara ya Ocean Road eneo linalolindwa sana kwa kuwa barabara hiyo inelekea ikulu ya rais nchini Tanzania.

3. Raphael Ongangi - Mfanyabiashara wa Kenya aliyetekwa tarehe 29 mwezi Juni 2019.

Mfanyabiashara huyo wa Tanzania mwenye uhusiano wa karibu na kiongozi wa upinzani Zitto Kabwe alikuwa akisimamia akaunti za mitandao ya kiongozi huyo .

Baada ya kukamatwa kwake habari za kutatanisha zilianza kuchapishwa katika akaunti ya Zitto kabwe.

Raphael alidaiwa kutekwa na watu waliojihami tarehe 24 mwezi Juni 2019.

Baadaye alipatikana tarehe 2 mwezi Julai mjini Mombasa.

4. Mdude Nyangali alitekwa tarehe 5 mwezi Mei 2019

Ni mwanaharakati ambaye amekuwa akimkosoa rais Magufuli na kukabiliana na serikali katika mitandao ya kijamii.

Aliripotiwa kupelekewa katika eneo lisilojulikana na watu wasiojulikana na kupigwa vibaya.

Baadaye alipatikana katika barabara ya Iringa Mbeya mnamo tarehe 8 mwezi mei 2019.

5. Leopold Kweyamba Lwabaje alitoweka wiki iliopita na kupatikana amefariki tarehe 29 2019

Alikuwa kiongozi wa Idara ya maswala ya muungano wa Ulaya katika wizara ya fedha.

Alitoweka muda mfupi alipokwenda kumuona jamaa aliyempigia simu wakati alipokuwa kazini.

Alitoweka kwa siku tatu kabla kupatikana karibu na nyumba yake ya Tabata Kinyerezi.

Alipoulizwa alipokuwa alisema kwamba amechanganyikiwa .

Mnamo tarehe 25 mwezi Julai alitoweka tena na akapatikana amenyongwa katika eneo la Mkurunga tarehe 29 Julai 2019.

6. Erick Kabendera mwandishi wa uchunguzi alitoweka tarehe 29 mwezi Julai 2019.

Erick ni mwanahabari mzungumzaji nchini humo akifanyia kazi kampuni tofauti nje na ndani ya taifa.

Kulingana na mkewe Erick alichukuliwa kwa nguvu na wanaume sita waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi lakini hawakutoa vitambulisho vyao.

Walimwambia mkewe kwamba wanampeleka katika kituo cha polisi cha Oyster Bay.

Hatahivyo jamaa na marafiki walimfuatilizia hadi katika kituo hicho cha polisi lakini hakupatikana.

Baadaye maafisa wa polisi walitoa ripoti kwamba anahojiwa na watakapokamilisha mahojiano hayo watatoa taarifa ya ni kwa nini alikamatwa.

Kabla ya kukamatwa kwake Vodacom iliagizwa na shirika linalodhibiti mawasiliano nchini Tanzania TCRA kufunga mawasiliano yake ya simu kulingana na gazeti la The East African.

Kamati inayolinda waandishi wa habari barani Afrika (CPJ) kupitia ujumbe huu wa Twitter ilisema inachunguza taarifa ya kukamatwa kwa mwandishi huyo wa wa habari za uchunguzi nchini Tanzania a aliyechukuliwa kutoka nyumbani kwake na "watu wasiojulikana .

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii