DR Congo: Joseph Kabila avuna pakubwa katika serikali ya muungano kati yake na Tshisekedi

Rais Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Jospeh kabila Haki miliki ya picha Getty Images

Rais wa DR Congo Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila wamekubaliana kuunda serikali ya muungano.

Tangazo hilo lilifanywa na wapatanishi moja kwa moja katika runinga siku ya Jumatatu usiku na kuthibitisha ripoti kutoka siku ya Ijumaa kwamba pande hizo mbili ziliafikiana.

Serikali hiyo itakua na mawaziri 66. Hao ni pamoja na waziri mkuu Sylvestre Ilinkumba ambaye alichaguliwa na bwana Kabila.

Mawaziri 42 watatoka katika chama cha kabila huku 23 wakitoka katika muungano wa bwana Tshisekedi.

Majina ya watakaoshikilia nyadhfa hizo bado hayajatolewa.

Hatua hiyo inajiri miezi saba baada ya muungano wa bwana Tshisekedi kwa jina CACH kushinda uchaguzi huo.

Maswali yaliulizwa wakati huo kuhusu matokeo hayo huku kukiwa na madai kwamba bwana Tshisekedi alifanya makubaliano ya kugawana mamlaka na bwana Kabila kabla ya uchaguzi huo.

Duru zinaelezea kwamba huenda Rais Tshisekedi atamteua waziri wa mambo ya ndani, waziri wa mambo ya nje, yule wa bajeti na uchumi na gavana wa benki kuu, huku Joseph Kabila akiteua waziri mkuu, wizara ya ulinzi, sheria, fedha na akiba.

Mgombea aliyechukua nafasi ya pili katika matokeo ya uchaguzi huo Martin Fayulu alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kutotambua matokeo hayo na kutishia kufanya maandamano.

Taarifa yake ilijiri baada ya ya mahakama ya kikatiba kuidhinisha ushindi wa mgombea mwengine wa upinzani , Felix Tshisekedi .

Muungano wa Afrika ulisema kwamba kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu matokeo hayo na kutaka matokeo rasmi kucheleweshwa.

Bwana fayulu sio mgombea pekee ambaye anaamini kwamba yeye ni muathiriwa wa wizi wa kura huku data ilioibwa ikionyesha kuwa alipata kura mara tatu ya kura alizopata Tshisekedi.

Mahakama ya kikatiba nchini humo iliidhinisha ushindi wa uchaguzi huo

Ilikataa ombi la rufaa iliowasilishwa na Martin Fayulu .

Licha ya uamuzi wa mahakama hiyo, bwana Fayulu alisema kuwa yeye ndio mshindi wa uchaguzi huo wa urais.

Bwana Fayulu pia alihoji kwamba jamii ya kimataifa haitambui matokeo rasmi ya uchaguzi huo.

Mahakama ilisemaje?

Mahakama ilisema kuwa bwana Fayulu alishindwa kuthibitisha kuwa tume ya uchaguzi ilitangaza matokeo bandia.

Iliendelea na kumtanagaza Felix Tshisekedi kuwa rais aliyechaguliwa kwa wingi wa kura.

Ghasia zimetokea kila kunapokuwa na mabadiliko ya uongozi katika taifa hilo.

Lakini thibtisho la matokeo rasmi ya uchaguzi huenda likaonyesha kubadilika kwa uongozi kihalali tangu DR Congo ijipatie uhuru wake kutoka kwa taifa la Ubelgiji 1960.

Bwana Fayulu alihoji kwamba Bwana Tshisekedi alikuwa amefanya makubaliano ya kugawana mamlaka na rais Joseph Kabila, hatahivyo upande wa Tshisekedi umekana hilo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii