'Yesu Kristo' azua gumzo Afrika kusini na Kenya

Screenshot of Micheal Job Haki miliki ya picha Michael Job/Facebook
Image caption Katika video aliyoipakia Job katika ukurasa wake wa Facebook mwishoni mwa juma, maduka ya kuuza bidhaa za ukulima na samani yanaonekana

Picha na video zinazomuonyesha mwanamume aliyevaa nguo kama Yesu kristo zimesambazwa pakubwa katika mitandao ya kijamii Afrika.

Lakini jamaa huyu ni nani na anafanya nini?

Ujumbe mmoja katika twitter, uliosambazwa zaidi ya mara 8,000 miongoni mwa wengine na mwanasiasa wa upinzain Afrika kusini Julius Malema, unasema "mchungaji kutoka Afrika kusini amemualika Yesu Kristu kutoka mbinguni kuhubiri kanisani mwake".

Lakini kwa uhalisi picha hizo zimetoka katika hafla iliyofanyika wiki iliyopita katika mji wa Kiserian kiasi ya kilomita 25 kusini magharibi mwa mji mkuu Nairobi nchini Kenya

Mwanamume huyo ni mhubiri kutoka Marekani na muigizaji anayeitwa Michael Job, aliyekuwa anahudhuria misa ya madhehebu mbalimbali ya kikristo ambako alialikwa kuzungumza.

Anaishi Orlando, Florida, ambako amekuwa akiigiza kuwa Yesu katika bustani maalum The Holy Land Experience theme park, inayojitambulisha kama "jumba halisi la biblia la ukumbusho".

Katika video aliyoipakia katika ukurasa wake wa Facebook mwishoni mwa juma, maduka ya kuuza bidhaa za ukulima na samani yanaonekana kwa nyuma - ambayo ndio yanayoonekana pia katika picha zilizosambazwa na kudaiwa kuwa zimepigwa Afrika kusini.

Watu wamekuwa wakifanya mzaha katika mtandao wa Twitter kuhusu picha hizo na namna wachungaji barani Afrika wanapenda kudai kufanya miujiza.

Mojawapo ya ujumbe uliosambazwa katika mablogu unatuhumu kuwa "mchungaji wa Kenya anadai amempata Yesu kristu akitembea mitaani Kenya".

Picha ilioambatana na ujumbe huo kwenye twitter ni ya Bwana Job aliyekuwa anahutubu wiki iliyopita katika kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (Pefa) lililopo mjini Kitengela nje kidogo ya mji mkuu Nairobi.

Katika video za mahubiri aliyokuwa anayotoa Kenya, mchungaji huyo wa Marekani anaahidi miujiza na uponyaji - mambo ambayo ameshtumiwa kwayo katika mitandao ya kijamii.

Hii sio ziara yake ya kwanza barani Afrika, mapema mwaka huu alikuwa nchini Togo, licha ya kwamba picha alizoweka kutoka huko hakuonekana akiwa amevaa mavazi ya kuiga - bali alikuwa amevaa suti.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii