Vijana wa 'panya road' waliokuwa tishio kwa vitendo vya uhalifu wajiajiri

Salum Kilango ni vijana waliokuwa wakijihusisha na kikundi cha uhalifu 'panya road'

Miaka 3 mpaka 10 iliyopita walikua vijana hatari, waliokuwa na uwezo wa kufanya uhalifu wowote, bila woga; kama kuiba, kukaba, kupora mpaka kuua.

Waliongoza kikundi kilichofahamika kama 'Panya Road' kilichotikisa Jiji la Dar es salaam kwa uhalifu.

Lakini leo wameamua kuachana na vitendo vya uhalifu kwa hiari na kuanzisha kijiwe chao cha kuosha magari na kupata fedha za kuendesha familia zao. Salum Kilango ni miongoni mwa vijana hao zaidi ya 30.

Yusuph Mazimu amemtembelea anapofanya shughuli na wenzake, katika eneo la Gongolamboto kando kando ya jiji la Dar es salaam

Kilango,anasimulia jinsi alivyoishi maisha ya hatari alipokuwa akijihusisha na uhalifu Ilikua ama zake ama za anayemkaba na kumuibia.

Kwa zaidi ya miaka 10, yeye na wenzake walikua wahalifu wa kuogopwa na jamii, lakini sasa ametubu: ''Baada ya kukutana na wenzangu majanga yaliyowakuta watu waliochomwa na moto waliingia jela kwa kweli ilinibidi ninyooshe mikono juu''. Anaeleza Kilango.

Kilango hivi sasa anafanya shughuli mbalimbali za kijamii katika mtaa anaoishi kwake na hata majirani zake ikiwa ni njia ya kurejesha uaminifu katika jamii yake ambayo ilikuwa ikimtenga au kumuogopa kutokana na historia ya maisha yake aliyoyaishi hapo kabla.

Image caption Vijana wameamua kujiajiri kujikimu na familia zao

''Sehemu nyingine napata ajira lakini nashindwa kuaminika na jamii kutokana na sura yangu, wale wote, jamii iliyokuwa pale mimi sifanani nao''. Alieleza Kilango

Lakini kutokana na changamoto ya ajira vijana kama Kilango wapatao 30 wameanzisha biashara ya kuosha magari, kazi ambayo huwapatia kipato si haba kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia zao.

Uhasama na Polisi haupo tena kwani ni sehemu ya wateja wao, anaeleza mmoja wa vijana hao.

''Hapa tupo kwa ajili ya kutafuta pesa, tunaaminika hata polisi wanatuachia magari yao tunaosha kuna vitu kama simu Flashi na vitu vingine vya thamani''.

Image caption Hivi sasa vijana hawa wanafanya kila jitihada kurejesha uaminifu kwa jamii yao

Bi Maryam ni mke wa Kilango, yeye alifichwa na mumewe kuhusu kazi anayofanya, alikuwa mtu wa kusikia mtaani tu, lakini kwa sasa ni familia moja yenye watoto wawili na yenye furaha sana.

''Mwanzoni sikujua lakini baadae tulipozoeana nikajua shughuli zake nikachukulia kawaida tu, nilikuwa na wasiwasi mwanzoni kutokana na maisha tuliyokuwa tunaishi, lakini kwa sababu nilimpenda nilichukulia kawaida.

Kujikwaa si kuanguka, Swali hapa ukianguka unachukua hatua gani?

Mada zinazohusiana