Dusitd2: Hoteli ilioshambuliwa na al-Shabab Kenya yafunguliwa rasmi

Hoteli ya Dusitd2 iliopo jijini Nairobi imefunguliwa

Hoteli ya Dusitd2 iliopo katika eneo la Riverside Drive Jijini Nairobi inafunguliwa rasmi leo Alhamisi , miezi sita baada ya kushambuliwa na magaidi na kusababisha vifo vya watu 21.

Sherehe ya ufunguzi wa hoteli hiyo iliadhimishwa kwa kubebwa kwa bendera tatu na mwanariadha David Rudisha pamoja na mkuu wa hoteli hizo.

Hoteli hiyo inayomilikiwa na raia wa Thailand ilifungwa kufuatia shambulio hilo la tarehe 15 mwezi Januari lililotekelezwa na wapiganaji wa al-Shabab ili kufanyiwa ukarabati.

Hoteli hiyo ilikuwa imefungwa hata baada ya afisi nyengine zilizopo katika barabara hiyo ya Riverside kufunguliwa.

Katika taarifa yake mwezi uliopita hoteli hiyo ilisema kwamba imeimarisha usalama wake na kuwapatia mafunzo mapya wafanayakazi wake.

Wakati wa kufungwa kwake tumechukua mda wa kuwafunza wafanyakazi wetu katika sekta mbalimbali ikiwemo ile ya wateja.

Ili kuimarisha usalama wa wageni wetu pia tumeweka mikakati ya kiusalama katika lango la hoteli hiyo , ilisema taarifa.

Wakati wa shambulio hilo la kigaidi hoteli hiyo ilipoteza wafanyakazi wake sita.

Ujasiri wa Wakenya

Kufunguliwa kwake kunaonyesha ishara na juhudi za Kenya kwamba haitaogopeshwa tena na magaidi.

Wakati wa shambulio hilo , mamia ya watu waliojitolea walifika katika hospitali mbali mbali kutoa damu ili kuwasaidia waathiriwa huku kampuni ya teksi ya uber ikitoa usafiri wa bure kwa vituo hivyo vya afya.

Mwanamke mmoja pia alijitolea kuwapatia waokoaji chakula na vikosi vya usalama kutoka katika gari moja lililokuwa nje ya hoteli hiyo.

Watu kadhaa walikamatwa kufuatia shambulio hilo na sasa wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Washukiwa

Wapiganaji wote watano waliovamia hoteli ya DusitD2 waliuawa na vvikosi vya usalama vilivyo saa kadhaa baada ya shambulio hilo.

Wakati huohuo washukiwa wanne walisimamishwa kizimbani katika mahakama kuu jijini Nairobi kuhusiana na shambulio hilo

Walikuwa washukiwa wa kwanza kuwasilishwa mahakamani wakihusishwa na shambulio hilo baya katika hoteli ya DusitD2 . Lakini hawakusomewa mashtaka yao.

Mkurugenzi wa mashtaka alitaka wapewa muda zaidi ili kufanya uchunguzi alioutaja kuwa mgumu na wa kimataifa.

Washukiwa wanne ni raia wa Kenya huku wa tano akiwa raia wa Canada mwenye mizizi ya Kisomali.,

Mapema maafisa wa polisi waliambia BBC waliwakamata watu saba.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii