Abdirahman Omar Osman, afariki baada ya kujeruhiwa katika shambulio la bomu Mogadishu

Meya wa Mogadishu Abdirahman Omar Osman Haki miliki ya picha Getty Images

Meya wa mji wa Mogadishu nchini Somalia ameaga dunia ikiwa ni juma moja baada ya kujeruhiwa katika shambulio la kujitoa muhanga ambalo liligharimu maisha ya watu sita.

Mwanamke mmoja alijilipua ndani ya ofisi ya meya Abdirahman Omar Osman wakati wa mkutano wa masuala ya usalama.

Bwana Osman, ambaye alikimbilia Uingereza wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 1990, alikuwa diwani wa London kabla ya kurejea mwaka 2008 kusaidia kuijenga upya Somalia.

Kundi la wanamgambmo wa al-Shabab lilisema kuwa lilitekeleza shambulio hilo.

Meya huyo amefariki dunia mjini Doha, Qatar, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Al-Shabab ilimlenga mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa nchini Somalia, James Swan, raia wa Marekani, ambaye tayari alishaondoka kwenye jengo hilo baada ya kukutana na meya tarehe 24 mwezi Julai.

Haikujulikana ni kwa namna gani mshambuliaji huyo aliweza kuingia ndani ya ofisi hizo zilizokuwa na ulinzi mkali.

Walioathirika kwenye shambulio hilo wengine ni maafisa wa juu.

Haki miliki ya picha Getty Images

Meya ni nani?

Bwana Osman alitoroka Somalia mwanzoni mwa miaka ya 1990 akiwa mkimbizi, kabla ya kupata stahada yake na uraia wa Uingereza. Pia alikuwa diwani kwa tiketi ya chama cha Labour .

Alirejea Somalia mwaka 2008, ambapo alilitumikia taifa hilo kwa nafasi ya waziri wa habari na kuwa meya wa Mogadishu mwaka jana.

Katika ukurasa wa twitter, ujumbe wa Marekani nchini Somalia umemtaja bwana Osman kuwa ''mshirika mzuri sana na aliyekuwa akiwatumikia raia wa Somalia bila kuchoka''.

Al-shabab inataka kuangusha utawala wa Somalia na imekuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara mjini Mogadishu, pamoja na uwepo wa vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Afrika na vikosi vya kijeshi vyenye mafunzo.

Kundi hili lenye mahusiano na kundi la wanamgambo wa al-Qaeda limekuwa na nguvu nchini humo.

Wanasiasa wachache wamehatarisha maisha yao

Katika mji ambao umekuwa na makundi ya hatari, alikuwa mstari wa mbele, mpole na mwenye maadili aliyekuwa akihakikisha mambo yanakwenda.

Jina lake la utani, Mhandisi Yarisow- Mhandisi mdogo- kutokana na kimo chake, sifa zake kielimu na utendaji wake.

Kama ilivyo kwa wasomali wengi, alitoroka kwenda ng'ambo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe akaishi London kwa miongo kadhaa.

Lakini aliyaacha yote hayo na kurejea Mogadishu muongo mmoja uliopita. Ilikuwa hatua ya kijasiri sana na alijua kuwa ni yenye kuhatarisha.

Tangu wakati huo, maelfu ya watu waliokuwa wakiishi nje ya Somalia walirejea kusaidia kuijenga Somalia, iliyokuwa imekumbwa na mashambulizi ya wanamgambo wa al-Shabab.

Safari ya Somalia kuelekea kuimarika imekuwa ndefu, na bado haijakamilika.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii