Eric Kabendera: Mama mzazi atofautiana na polisi kuhusu uraia wa mwanawe Tanzania

KABENDERA Haki miliki ya picha @MariaSTsehai/Twitter

Mama ya mwanahabari Eric Kabendera, Verdiana Mujwahuzi, 80 amezungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu mwanawe akamatwe Jumatatu wiki hii na maafisa ambao hawakuwa wamevalia sare rasmi za polisi.

Tayari kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar Lazaro Mambossasa amethibitisha kuwa mwandishi huyo alikamatwa kuhusiana na utata unaokumba uraia wake.

Lakini mama Mujwahuzi anapinga kauli ya polisi kuhusu uraia wa mwanawe.

''Kabendera ni mwanangu, nilimzaa hapa Tanzania na hapajawahi kuwa na utata kuhusu anakotoka, polisi iseme ukweli inamshikilia kwa nini'' aliliambia Gazeti la The Citizen nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Gazeti hilo mama huyo wa miaka 80 alikuwa nyumbani kwa mwanawe tukio la kukamatwa kwake lilipotokea.

''Nimejawa na wasiwasi na hakuna yeyote anayenipatia habari kumhusu'' alisema mama Mujwahuzi akihojiwa na The Citizen.

Mama huyo haelewi kosa alilofanya mwanawe ni lipi na haamini ikiwa suala la yeye kuwa Mtanzania au la.

Pia anataka kujua nia ya serikali kumhoji uraia wa mwanawe akisisitiza kuwa ni Eric ni raia wa nchi hiyo kwa kuzaliwa.

The Citizen liliripoti kuwa Siku ya Jumatano Mama Mujwahuzi alihojiwa na watu kumi amabo alifahamishwa baadae ni maafisa wa uhamiaji waliotaka kuthibitisha uraia wa mwanawe.

''Walinihoji kwa zaidi ya saa 10 na waliandika kurasa kumi ya kijitabu wachokuwa wakitumia'' alisema Bi Mujwahuzi ambaye ni mwalimu wa zamani katika eneo la Kagera

Kama mwalimu bado anakumbuka umuhimu wa kuweka nakala ya kumbukumbu- Licha ya umri wake mkubwa bado ana kumbukumbu nzuri.

Anasema kuwa mara ya kwanza aliwahi kuhojiwa kuhusu suala la uraia ilikuwa karibu miaka minne iliopita mjini Bukoba.

''Wakati huo waliandika nilichosema mbona hawaweki kumbukumbu?'' aliuliza mama Mujwahuzi

Mei 2013 serikali ilisema uraia wa Erick Kabendera na wazazi wake, Nolasco John Kabendera na Verdiana Protus Mujwahuzi haubishaniwi kwani wote ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa. (IBN TV Archives)

Julai 2019 Polisi wamesema wanamshikilia Erick kutokana na utata wa uraia wake.

Bi Mujwahuzi anaendelea na matibabu ya shinikizo la damu na anahofia kuendelea kuzuiliwa kwa mwanawe Eric Kabendera huenda kukaathiri hali yake.

Anamatumaini utata wa uraia unaomzunguka mwanawe utapata ufumbuzi na ataachiliwa hivi karibuni akiwa salama.

Uchunguzi wa uraia wake

Uchunguzi wa utata wa uraia umekuwa ukifanyika kwa watu mbalimbali wakiwemo watu mashuhuri katika jamii. Hivyo suala hili limeibua hisia huenda kwa kuwa muhusika ni mwanahabari.

Aidha baada ya kuulizwa kuwa kwa nini wanamkamata kwa mara nyingine kwa suala hilo hilo la uraia ikizingatiwa kuwa si mara ya kwanza kuwahi kuhojiwa kuhusu suala hilo, Kamishna Kihinga alikataa kuwa hawajawahi kumkamata kuhusu taarifa hizo,

"Hatujawahi kabisa kumkamata na kama kweli Basi mtusadie hizo taarifa ili zitusaidie kumuachia''.

Image caption Kamishna wa udhibiti wa pasipoti wa idara ya uhamiaji Gerald Kihinga

Mke wa mwandishi Erick Kabendera aliruhusiwa kumuona mume wake Erick Kabendera siku mbili baada ya kamatwa na jeshi la Polisi siku ya Jumatatu jioni nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaaam.

Polisi walimsindikiza Kabendera nyumbani kwake kwa ajili ya kupata nyaraka za uthibitisho wa uraia wake.

Wito wa kuachiliwa kwake

Kumekuwa na shinikiza la kutaka mwandishi Eric Kabendera kuachiliwa huru ndani na nje ya Tanzania.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wamewasilisha ombi la kutaka aachiliwa kwa Mahakama ya Hakimu mkaazi wa Kisutu jijini Dar es Salaam. Kesi hiyo itasikilizwa Jumatatu wiki ijayo.

Hapo jana Ijumaakulikuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu nani anayemzuilia mwandishi huyo kati ya Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii