Wakali Kwanza: Gengi linalowahangaisha wakaazi Mombasa

The injured were rushed to this local clinic for initial first aid
Image caption Baadhi ya waliojeruhiwa walipelekwa katika kliniki iliyokuwa karibu kupokea matibabu

Takriban watu wanane wamejeruhiwa baada ya vijana waliojihami kwa mapanga kuushambulia mtaa moja katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya katika kinachojitokeza kuwa ni uhasama baina ya makundi mawili hasimu ya magengi ya uhalifu.

Hofu ilitanda katika eneo la Bamburi Jumatatu usiku baada ya kundi la vijana wapatao 30 waliojihami kwa mapanga, visu na silaha nyingine butu kulivamia eneo hilo na kuanza kuwashambulia wakaazi waliopita njia.

Polisi iliarifiwa na wakafika katika eneo hilo - lililogeuka kuwa enoe la makabiliano baina ya maafisa wa usalama na wahaifu hao na palishuhudiwa ufyetulianaji risasi.

Washukiwa watatu wamekamatwa na maafisa wa usalama wanasema uchunguzi umeidhinishwa.

Picha za kuogofya zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii baada ya mkasa huo, zilizoonyesha baadhi ya manusura wakiwa na majeraha mabaya katika sehemu tofuati za mwili baada ya baadhi kupigwa kwa mapanga au kuchomwa visu.

Baadhi walifikishwa katika kliniki iliyokuwa karibu na eneo hilo, kabla ya kuhamishwa na kupelekwa katika hospitali kuu ya mkoa, Coast General kupokea matibabu zaidi.

Wakali Kwanza ni nani?

Kwa mujibu wa Johnston Kipara, kamanda wa polisi mjini Mombasa aliyezungumza na BBC, anasema ni kundi la vijana wahalifu.

'Lengo lao ni kuweka uoga na kutekeleza uporaji katika jamii' amefafanua.

Kwa baadhi ya wakaazi, Wakali Kwanza ni moja ya makundi mawili ya uhalifu yanayohudumu katika eneo hilo la pwani na yanafahmika kwa kujihusisha katika biashara haramu na matumizi ya madawa ya kulevya, uporaji na wizi wa mabavu.

'Jukumu letu ni kuhakikisha mji wa Mombasa unabaki salama na wanaohusika hatua zinachukuliwa wanapopatikana' amesema kamanda wa polisi Kipara.

'Inatusaidia kupanga mipango yetu kwa haraka na kuhakikisha kwamba tunakuwa macho kila wakati' ameongeza.

Mchambuzi wa masuala ya usalama Isaac Mwendwa, anayehusika na kampeni dhidi ya itikadi kali na ugaidi nchini Kenya anasema shambulio la Jumatatu usiku ni ushindani baina ya makundi hasimu ya uhalifu kila moja likitaka kujionyesha nguvu.

Amefafanua kuwa ni kuonyesha ushindani baina ya makundi hasimu yanayotaka kuonekana kuwa na ushawishi katika uhalifu kama biashara ya madawa ya kulevya, wizi na kadhalika.

Tathmini yake ni kwamba serikali haijaonesha kutilia uzito wa kutosha hatari ya inayotokana na magengi hayo japo ni madogo. Amekosoa mbinu inayotumika na maafisa wa utawala anayosema hairidhishi.

Amefafanuwa kwamba kuna haja ya kuwepo jitihada endelevu na za ushirkiano mkubwa wa pamoja na jamii katika Pwani ya Kenya ili kutatua kikamilifu changamoto hiyo na sio tu kwa kuwakamata wahalifu.

Wasiwasi wa jamii

Taarifa zilisambaa kwa kasi na baadhi ya raia waliingia katika mitandao ya kijamii kuelezea wasiwasi na hofu walionayo kutokana na uhalifu wa magengi hayo ya vijana.

Kuna na baadhi waliojipata katikati ya shambulio hilo wakati lililpotokea jana usiku na kutumia mitandao ya kijamiikuelezea kilichowakuta.

Serikali ilitoa makataa kwa wafuasi wa magengi hayo ya uhalifu kujisalimisha.

Aliyekuwa mkuu wa polisi katika kaunti hiyo Nelson Marwa, amesema makundi hayo ya vijana hufadhiliwa na baadhi ya matajiri wenye ushawishi katika eneo hilo la pwani.

Uchunguzi sasa unaangazia kwanini yamefanyika, na uhalifu ulitekelezwa kwa ushirikiano wa nani.

Maswali ambayo pia yameulizwa na baadhi katika mitandao ya kijamii, kwamba dhamira ya mashambulio hayo dhidi ya Wakenya wasiokuwa na hatia ni ipi? na ni nani mfadhili wa makundi hayo?

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii