Tanzania ina cha kuifunza Uganda kuhusu usajili wa wamiliki mitandao?

mitandao Uganda Haki miliki ya picha ISSOUF SANOGO

Tume ya mawasiliano nchini Uganda imeanza kuwasajili watu wanaotumia na kumiliki majukwaa mitandaoni kwa ajili ya mawasiliano na biashara.

Wamiliki blogu, na kurasa mbalimbali katika mitandao ya kijamii, wamiliki wa majukwaa mitandaoni, redio na hata televisheni Uganda sasa wanatakiwa kulipa ada ya $20 kupata kibali au leseni kuendeleza huduma zao.

Kwa mujibu tume hiyo UCC - hatua hiyo imenuiwa kudhibiti watumiaji mitandao.

Kutaiwezesha tume ya mawasiliano Uganda Kufuatilia, kukagua, kuangalia, kuthibiti na kurekebisha taarifa zinazo sambazwa na kundi la watu wenye ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na wanablogu.

Kila mtu aliye na ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na mnablogu anapaswa kujaza fomu inayoeleza taarifa kumhusu ikiwemo washirika wake na mipango yao ya kifedha.

Baada ya kujaza fomu hizo, kila mmoja atapewa kibali kitakachomruhusu kuendelea na kazi yake.

Baadhi ya watu walioitwa kujiandikisha wana kampuni ambazo zimesajiliwa na zinafanya kazi kisheria kama vile mashirika ya habari, lakini hata hivyo wanafaa kujiandikisha tena.

Wote hawa wanafaa kuandikisha shughuli wanazofanya kama biashara rasmi na wanafaa kufuatilia kanuni za maadili kwa waandishi wa habari, hata kama wengi wao si wanahabari.

Haki miliki ya picha UCC
Image caption Makao makuu ya tume ya mawasiliano Uganda

Pia wanapaswa kuwasilisha mikataba ya ajira inayo onyesha sharia na masharti ya kazi zao.

Mamlaka ya Uganda inasema atakaye kosa kufuata maagizo ya UCC hataruhusiwa kuendelea kutoa huduma za mawasiliano na huenda tovuti au kurasa wanazomiliki zikafungiwa.

Ibrahim Bbosa msemaji wa UCC nchini Uganda anasema sheria inawapa mamlaka kufuatilia huduma za mawasiliano hata zilizo kwenye mitandao ya kijamii.

"Watumiaji mitandao na washawishi katika mitandao ya kijamii waliofika kiwango cha kusambaza mawasiliano na wanaotumia mitandao kwa biashara wanahitajika kujisajili na mratibu ambaye ni UCC."

Mwaka jana serikali ya Uganda iliidhinisha kodi kwa mitandao ya kijamii iliyokumbwa na mzozo.

Makundi ya kutetea haki za binaadamu yanasema serikali nchini humo inaonekana kona mitandao ya kijamii kama tishio na inataka kuifuatilia na kubana matumizi yake.

Wamiliki wamepokeaje hatua hii?

Bettina Praise Tumuhaise, ni mmoja wa waganda walio na ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Anatumia mtandao wake kutangaza habari kuhusu ukulima na burudani, anasema huu ni mpango mpya wa serikali kuweza kulazimisha watu wanaolipa kodi kulipa ya ziada.

'Wajitokeze watueleze tu wanachotaka, wanajificha tu, au wanataka kututumia katika siku zijazo, hususan unafahamu kwanini... Na kama ni hilo, basi watupigie na watuambie,'jamani tunajua munafanya kazi nzuri, tunawahitaji' anaeleza Bettina.

Wengine wanasema serikali inajaribu kufukuza watu kwenye mitandao ya kijami na utumiaji wa intaneti kwa ujumla.

'Tunapata pesa kutokana na mitandao ya kijamii lakini tuna makampuni yaliosajiliwa. Na tunalipa kodi kwa makampuni hayo.

Kujisajili tena ni usajili wa mara ya pili. Wanataka tulipe pesa zaidi na zaidi na pengine kupunguza idadi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii Uganda.' Anasema Telma.

Mwaka uliopita watu wanaotumia in Intaneti inchini Uganda walipunguka kwa milioni 2.5, miezi mitatu baada ya serikali kuanzisha mitandao ya kijami ya kodi maarufu OTT.

Sheria yamaudhui mitandaoni Tanzania

Hatua kama ya Uganda iliidhinishwa katika nchi jirani mwaka jana baada ya serikali kushinda kesi iliofunguliwa na wadau wa habari kupinga kanuni za maudhui mitandaoni 2018.

Kanuni hizo zilizosainiwa na waziri mwenye dhamana ya habari ambazo pamoja na mambo mengine zilinuiwa kusimamia usajili na kuweka mfumo wa uwajibikaji na maadili kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii inayohusika na habari nchini humo.

''Kwa hukumu hiyo , tunatumia fursa hii kuutarifu umma kuwa sasa wamiliki wa mitandao ya kijamii inayohusika na usambazaji wa habari kama blogu, TV na redio za mitandaoni na wengine walioainishwa katika kanuni wanapaswa kuendelea kujisajili na kufuata maadili kwa mujibu wa kanuni husika'', ilisema serikali katika taarifa yake.

Wanaotuma maombi huhitajika kuwasilisha stakabadhi zao ikiwemo maelezo ya hisa, uraia, kibali cha kuonesha wanalipa kodi mbali na mipango ya mafunzo.

Sheria iliyopitishwa mwezi Machi inafanya kuwa lazima kwa wenye blogu na wamiliki wa majukwaa ya mtandaoni kama televisheni za mtandao wa Youtube kujiandikisha katika serikali na kulipa kiasi cha dola 900 ili kupata leseni.

Wanablogu ambao wanaopatikana na hatia ya kutoheshimu sheria hiyo, wanaweza kukabiliwa na faini ya hadi milioni 5 ama kifungo kisichopungua miezi 12 ama zote mbili kulingana na sheria hiyo iliyoidhinishwa mwaka jana.

Tangu kupitishwa kwake mwaka 2015, sheria ya makosa ya kimtandao imekuwa ikikosolewa na wanaharakati wa uhuru wa habari na kujieleza na kushutumiwa kuwa ni sehemu ya mpango wa serikali kukandamiza uhuru wa kujieleza nchini Tanzania

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii