Mzozo wa Kashmir: Pakistan imemtimua mwanadiplomasia wa India

Mpaka wa India na Pakistan (file photo) Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mpaka wa Wagah ni nembo ya uhasama uliopo kati ya India na Pakistan

Pakistan imetangaza hatua ya kumfurusha mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa India na kusitisha biashara kati yake na India kufuatia mzozo wa eneo la Kashmir.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa, UN umeelezea hofu yake kufuatia hatua ya hivi karibuni ya India kuiondolea Jimbo la Kashmir, mamalaka ya kujitawala ikisema "itachangia ukiukwaji wa haki za binadamu".

Msemaji wa UN amegusia hatua ya kukatiza huduma za mawasiliano, kuwazuilia viongozi wa jimbo hilo na kupiga marufuku mikutano ya kisiasa baadhi ya mambo yanayoweza kuchangia hali ya taharuki katika eneo hio.

maelfu ya maafisa wa usalama wamekuwa wakishika doria katika barabara za eneo hilo.

Visa vya maandamano na makabiliano ya mawe vimeripoti, licha ya kukatizwa kwa mawasiliano na kuwekwa kwa amri ya kutotoka nje.

Wakashmir katika maeneo mengine nchini humo wamesema kuwa hawana njia ya kuwasiliana na familia zao. Baadhi ya viongozi wa eneo hilo pia wamezuiliwa

India na Pakistan - huko nyuma zilishawahi kupigana vita kutokana na mzozo wa eneo hilo, je dunia inaelekea kushuhudia tena mapambano ya nchi hizo ambazo tayari zinajihami na silaha nzito za nyukilia?

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waandamanaji Pakistani wakipinga hatua ya India

Kwanini Kashmir ni eneo tata?

Kashmir ni eneo lililopo kwenye safu za milima ya Himalaya na nchi zote mbili India na Pakistani zinadai kuwa ni eneo lao.

Katika kipindi cha ukoloni wa Mwingereza jimbo la Jammu na Kashmir lilikuwa na hadhi ya kujitawala kupitia kiongozi wa makabila, lakini likajiunga na India mwaka 1947 katika kipindi ambacho Bara Hindi lilipatiwa uhuru na kugawanywa katika mataifa mapya ya India na Pakistani.

Nchi hizo mbili huenda zikatumbukia vitani na kujikuta kila mmoja akishikilia sehemu ya eneo hilo baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano yalipoafikiwa.

Kumekuwa na ghasia katika upande wa jimbo hilo utakaotawaliwa na India kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Makundi ya wanaharakati wanaotaka kujitenga na India yamekuwa yakishinikiza kupewa uhuru wao.

Huwezi kusikiliza tena
Mataifa ya India na Pakistan yalivyoundwa

Mwanzoni mwa mwezi wa Agosti, kulikuwa na dalili kuwa kuna jambo kubwa lingetokea katika jimbo la Kashmir.

Makumi ya maelfu ya wanajeshi wa ziada wa India yalipelekwa kwenye eneo hilo.

Shughuli kubwa ya kuhiji ya kihindu ilikatazwa na mamlaka, shule na vyuo viliamriwa kufungwa.

Watalii waliamriwa kuondoka mara moja na huduma za simu na mtandao wa intaneti kufungwa.

Viongozi wote maarufu wa kisiasa wa eneo hilo waliwekwa katika vizuizi kwenye nyumba zao.

Lakini wakati hayo yote yakiendelea, hofu kubwa ilikuwa ni kwamba ibara ya 35A ya katiba ya India ingelifutiliwa mbali.

Ibara hiyo ndiyo inayoipa Kashmir upekee na hadhi ya kujitawala.

Serikali ikashangaza kila mmoja kwa kufuta ibara nzima ya 370 ambapo 35A ni ibara ndogo, na sehemu hiyo ya katiba ndiyo imekuwa mwongozo wa sera za nchi hiyo juu ya Kashmir kwa miongo saba iliyopita.

Pakistani yapaza sauti

Pakistan imesitisha mikataba yote ya kibiashara kati yake na India.

Waziri Mkuu wa Pakistani Imran Khan ameapa kulifikisha suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN).

Bw Khan amesema uamuzi huo unavunja sheria ya kimataifa, na kudai kuwa anahofu kuwa uamuzi huo unaweza kutokomeza jamii moja (ya waisilamu).

"Ninahofu... (India) wanaweza kujaribu kuwafurusha wenyeji na kuingiza watu wapya ili wawe wengi zaid, hivyo wenyeji hawatakuwa na sauti na kubakia kuwa watumwa tu," Khan ameliambia bunge la nchi hiyo.

Kumekuwa na maandamano nchini Pakistani ambapo raia wa nchi hiyo wanapaza sauti zao dhidi ya hatua hiyo ya India.

Pakistan pia aimetoa wito kwa Baraza la uslama la umoja wa mataifa kutangaza mzozo katika eneo hilo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan

Ibara ya 370 ina umuhimu gani?

Kwa kupitia ibara hiyo, Kashmir iliweza kuwa na katiba yake, bendera na uhuru wa kujitungia sheria zake. Mambo ya nje, ulinzi na mawasiliano zilibaki kuwa sekta ambazo zinaongozwa na serikali kuu ya India.

Kifungu hicho cha katiba kimekuwa kikipingwa na baadhi ya wananchi wa India hususan wahafidhina wa Kihindu.

Kashmir ndio jimbo pekee ambalo lilikuwa na Waislamu wengi lililojiunga na India wakati Bara Hindi lilipogawanywa.

Waziri Mkuu wa sasa Narendra Modi anaongoza chama chenye mrengo wa kihafidhina wa kihindu, na kuifutilia mbali ibara ya 370 ya katiba ilikuwa ni moja ya ahadi za kampeni za chama chake katika uchaguzi wa mwaka huu.

Viongozi wa chama tawala walidai kuwa jimbo hilo linabidi kuwa sawa katika kujiendesha na majimbo mengine yote ya India na baada ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika mwezi Aprili-Mei chama hicho kimetekeleza ahadi yake bila kupoteza muda.

Hata hivyo wakosoaji wanasema uamuzi huo unatumiwa na serikali ili kujificha kutokana na mdororo wa kiuchumi ambao India unaupitia hivi sasa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kumekuwa na ghasia kwenye upande wa Kashmir unaotawaliwa na India kwa miaka 30 sasa

Jamii ya kimataifa imepokelea vipi hatua hiyo?

Taifa jirani la China limepinga vikali hatua ya India nakusema kuwa "halikubaliki".

Waziri wa mambo yanje wa Uingereza Dominic Raab ameripotowa kuzungumza na mwenzake wa India na "kuelezea hofu yake kuhusiana na suala hilo na kuomba busara itumike kusuluhisha mzozo huo".

Afisa wa idara ya masuala ya ndani wa Marekani amekanusha ripoti kuwa taifa hilo lilikuwa na ufahamu kuhusu njama ya India katika jimbo la Kashmiri.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii