Si kila asali ni tamu, je asali chungu hupatikana vipi?

Asali
Image caption Asali chungu inapatikana vipi?

Asali ni zao la nyuki ambalo miaka yote linasifika kwa utamu wake. Lakini hivi sasa mambo yameanza kubadilika.

Usishangae kula asali ambayo ladha yake inaweza kuwa chungu kama shubiri.

Unaweza kuuliza je hii inasababishwa na nini? Sio mabadiliko ya nchi bali ni ubunifu na jitihada za binadamu katika kutafuta tiba.

Kushamiri kwa biashara ya asali kumeanza kuwapunguzia soko wafanyabiashara, hivyo, ili kuvutia wateja zaidi, wameanza kuwa wabunifu katika bidhaa zao.

Levina Swai ni mmoja wa wabunifu hao.

Yeye, mbali na kuuza asali ya kawaida, lakini pia anauza asali ambayo ni chungu kama muarubaini.

Na hii inatokana na kuweka mizinga yake ya nyuki katika miti yenye asili ya uchungu kama vile miarubaini na hata alovera, hivyo kwa sababu asili ya maua ya miti hii ni michungu, na asali inayovunwa nayo inakuwa chungu.

Lakini hiyo sio sifa pekee ya asali hiyo. Levina anasema, asali hii inasaidia kutibu maradhi kama vile malaria, ngiri na hata chango.

Asali hii ingawa haijafanyiwa vipimo vya kitaalamu kuthibitisha ubora wake katika kutibu maradhi mbalimbali, lakini Levina anasema kuna ushuhuda mbalimbali.

"Bado hatujaifanyika vipimo lakini mimi nafanya kupitia wateja, nimefanya kwa zaidi ya miaka mitano, na wateja kila mara wanajirudia," amemwambia mwandishi wa BBC Aboubakar Famau katika maonesho ya Nanenane mkoani Dodoma.

Andrei Kikoti ambae ni mmoja wa wateja ambae amenunua asali hiyo chungu, amekiri kuwa tofauti na asali ya kawaida, lakini ameonyesha matumaini ya watu kuizoea baadae.

Image caption Levina Swai akiwa kwenye maonesho ya Nane Nane mjini Dodoma ambapo asali chungu ni moja ya kivutio.

"Ukweli ni kuwa ina ladha ya uchungu, najisikia tofauti nikionja, tulivyofundishwa tumeambiwa asali tamu, lakini hii ni tofauti. Nahisi itakubalika kutoka na maelezo ya muulizaji kwamba imetokakan na miti mbalilmbali."

Baltazari Lymo, kutoka Arusha ambae alikuwa na maumivu ya tumbo, anathibisha kupata nafuu baada ya kula asali hiyo.

Kwa upande wake, Francis Singaele, Afisa Nyuki kutoka Shamba la Miti Sao Hill, anakiri ubora wa asali chungu katika matibabu.

"Ni kweli asali ambayo inatokana na miarubaini na mikatani inaweza kutibu kutokana nay ale maua nyuki wanayochukua katika hiyo miti, inaweza kuleta mchanganyiko unaotibu maradhi mingi," anasema Francis.

Ingawa asali chungu haijathibitishwa kitaalamu kwamba ina uwezo wa kutibu maradhi kama ilivyoelezwa, lakini, asali yenyewe imekuwa ni tiba ya jadi katika maradhi mbalimbali.

Mada zinazohusiana